Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Mwaka 1930, mchumi wa Uingereza, John Maynard Keynes alitabiri kwamba ndani ya karne moja, masaa yanayohitajika kufanya kazi kwa wiki hayatazidi 15. Alionyesha kwa jinsi teknolojia ilivyokuwa inaenda kwa kasi, kazi nyingi sana zitarahisishwa na hivyo watu kutohitajika kuhangaika na mengi.
Sasa tunakaribia kukamilisha hiyo karne, teknolojia imekua kwa kasi sana, kazi zimerahisishwa mno, lakini bado masaa ya kazi hayajapungua, ila yameongezeka zaidi. Kuna kitu kimoja mchumi huyo hakukizingatia, tabia yetu binadamu kutaka zaidi na zaidi.
Tabia hiyo siyo mbaya, lakini pale inaposhindwa kudhibitiwa vizuri, inakuwa mzigo badala ya manufaa. Tabia hiyo ya kutaka zaidi na zaidi ndiyo imeleta maendeleo makubwa kwa mtu mmoja mmoja na dunia kwa ujumla. Lakini pia ni tabia ambayo imewaingiza wengi kwenye msongo kwa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kabisa kwao.
Akili Mnemba (AI) Inatuvuruga Zaidi.
Kwa sasa tupo kwenye zama za teknolojia ya tofauti na teknolojia nyingine, ambayo ni akili mnemba (AI). Tofauti ya teknolojia hii ni inamwezesha kila mtu kufanya chochote kile, hata kama hana ujuzi au uzoefu. Akiweza tu kuuliza vizuri, anaweza kupata majibu na kutengeneza kitu chochote.
Tungeweza kudhani kwamba teknolojia hii ndiyo ingetimiza utabiri wa Keynes, kwamba kwa uwezo wa teknolojia hii kufanya mambo mengi, watu hawatalazimika sana kufanya kazi.
Lakini kwa tunachokiona mpaka sasa, mambo yatakuwa tofauti kabisa. AI haipunguzi kazi kama ambavyo inategemewa, badala yake inaongeza kazi zaidi kwa watu. Hiyo ni kwa sababu watu wanajikuta wakifanya mambo mengi kuliko awali, maana sasa teknolojia imewawezesha kufanya hata ambayo hawakuwa wanaweza kuyafanya.
AI imewafanya watu wajipe majukumu ambayo yalikuwa yanafanywa na watu wengine. Pamoja na AI kurahisisha majukumu hayo, bado yanakuwa ni kazi inayoongezeka kwa mtu anayechagua kuyafanya, kama siyo majukumu yake makuu.
Kwa mfano kama wewe ni mfanyabiashara na unataka kuwa na tovuti, huko nyuma ungempa mtaalamu wa kutengeneza tovuti afanye kazi hiyo. Lakini kwa zama hizi za AI, unaweza kuiambia ikutengenezee tovuti ya biashara na ikaweza kutengeneza.
Lakini sasa, mpaka uweze kupata tovuti iliyo bora, itakuchukua muda mrefu kuliko ambavyo mtaalamu angechukua. Ndiyo, unaweza kupata matokeo, ila itakuchukua kazi na muda mpaka kuyapata.
Hivyo, uwepo wa AI unakuwa umeongeza kazi kwako kuliko kupunguza.

Upande Binafsi Hali Ni Mbaya Zaidi.
Hapo juu tumeangalia upande wa kazi na biashara tunazofanya, kwa jinsi maendeleo ya teknolojia yameongeza kazi badala ya kupunguza. Inapokuja kwenye upande binafsi, hali imekuwa mbaya zaidi badala ya kurahisishwa na teknolojia.
Tukirudi kwenye asili ya binadamu, umbeya ni kitu ambacho kimekuwepo tangu enzi na enzi. Na japo watu huwa wanaona umbeya ni kitu kibaya, ni kitu kilichokuwa muhimu kwenye jamii zetu binadamu, kama njia ya kupeana taarifa mbalimbali zinazowahusu watu. Na mara nyingi taarifa hizo zilikuwa muhimu, hasa pale watu wanapokuwa na tabia zisizo na manufaa kwa jamii husika.
Kwa sasa, teknolojia imewezesha mawasiliano kwa watu wengi na waliopo eneo lolote duniani. Tabia yetu ya umbeya, ya kutaka kupata taarifa za wengine imetugeuza kuwa waraibu wa mitandao ya kijamii na kupata habari.
Tunaiona mitandao ya kijamii kama njia ya kuwasiliana na kupashana habari, lakini ni chombo kikubwa cha umbeya. Wewe mwenyewe unajua jinsi ambavyo umekuwa unafuatilia maisha ya wengine kupitia yale wanayoweka kwenye mitandao hiyo ya kijamii.
Na kwa bahati mbaya sana, watu wametumia mitandao hiyo kudanganya, wanaweka picha na taarifa zinazowafanya waonekane wako vizuri kuliko ilivyo kwenye uhalisia.
Hili limeleta madhara makubwa kwa wengi, kwa kulinganisha maisha yao na yale wengine wanaweka kwenye mitandao. Wapo wanaojiona wapo nyuma kwa sababu maisha yao hayafanani na ya wengine yanavyoonekana mtandaoni. Wasijue kwamba kinachowekwa mtandaoni siyo uhalisia.
Tiba Pekee Ni Kupandisha Kodi Kwenye Akili Yako.
Wewe mwenyewe unajua, maeneo ambayo kodi za nyumba ni bei rahisi, huwa zinakuwa na watu wengi na uswahili mwingi pia. Kadiri wengi wanavyoweza kumudu kodi, ndivyo wanavyokaa kwa wingi kwenye eneo. Na maeneo yenye gharama kubwa ya kodi, wanakaa wachache ambao pia wana uwezo mkubwa.
Hivyo pia ndivyo akili zetu zilivyo, kadiri inavyokuwa gharama rahisi kwa mambo kuingia, ndivyo mengi yasiyo na tija yanavyoingia. Mambo mengi yasiyo na tija yanapoingia, yanachukua nafasi ya yale machache ambayo yangeweza kuwa na tija.
Kwa kujua hilo, unapaswa kupandisha sana kodi kwenye akili yako. Kupandisha kodi kwenye akili maana yake ni kutokuruhusu mambo yasiyo na thamani wala tija kuingia kwenye akili yako. Mambo hayo yatakuja kwako, lakini kuyaruhusu yaingie ndiyo kitu ambacho hutafanya. Na hutaruhusu kwa sababu utakuwa na chujio la gharama kubwa sana kwenye kupima nini kinaingia na nini hakiingii.
Kwa kuwa wewe ndiye mwenye nyumba wa akili yako, unapaswa kuhakikisha kiwango cha kodi unachoweka kinachuja na kukataa mengi ili kutoa nafasi kwa machache ambayo ni bora zaidi. Kwa sababu nafasi ya akili yetu ni ya uhaba, una kila haki ya kupandisha kodi ili nafasi hiyo isijazwe na yasiyokuwa na tija.
Kwenye #BaruaYaKocha unakwenda kujifunza hatua TANO za kuchukua ili kuhakikisha kodi ya pango kwenye akili yako inakuwa kubwa sana, kiasi cha kuzuia yote yasiyo na tija kukukwamisha kufanikiwa.
Soma barua hiyo hapa; #BZK049; Pandisha Kodi Ya Pango Kwenye Akili Yako Uepuke Mengi Yanayokukwamisha.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.