Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Ni mimi ambaye nimekuwa nakuambia uhangaike na uimara wako na kuachana kabisa na madhaifu. Na mimi huyu huyu, leo tena nakuambia mafanikio yako yanaamuliwa zaidi na madhaifu uliyonayo kuliko uimara wako.
Je nakuchanganya? Je hujui ushike lini na uache lipi? Twende taratibu kwenye barua hii na utanielewa vizuri na utaona jinsi ambavyo yote mawili ni sahihi. Yaani kutokuhangaika na madhaifu yako, lakini pia kuyatumia ili kupata mafanikio makubwa.
Kuna kauli inasema; “Uimara wa mnyororo unaamuliwa na kiungo chake kilicho dhaifu zaidi.” Hii ni kauli yenye maana kubwa sana kwenye kila eneo la maisha. Kunaweza kuwa na maeneo ambayo yana uimara na maeneo yenye madhaifu. Pale maeneo yenye madhaifu yanapokuwa ya kutegemewa zaidi, hayo ndiyo yanayoamua matokeo.
Tutumie mfano wa mnyororo, kama kwenye usemi hapo. Tuseme una gari limekwama na linatakiwa kuvutwa na gari jingine. Unaenda dukani kununua mnyororo wa kuvuta gari hilo. Unapewa mnyororo, ambao ni imara kweli kweli. Lakini katika kuukagua, unagundua moja ya kiungo chake, tena cha katikati, kina kutu na kimeshaanza kusagika. Je utachukua mnyororo huo?
Vipi kama muuzaji akikuambia; “Angalia, huu mnyororo una viungo zaidi ya 100, vyote ni imara, ni hiki kimoja tu kina shida, hakina athari sana.” Je utamsikiliza na kumwamini? Najua hutamwamini kwa sababu unajua uimara wa mnyororo mzima hauna maana kama kuna kiungo kimoja tu ambacho ni dhaifu.
Sasa rafiki yangu, hivyo ndivyo umekuwa unayaendesha maisha yako kwa kipindi kirefu, ndiyo maana umekuwa unakwama kufanikiwa licha ya kuwa na kila kitu kinachohitajika ili uweze kufanikiwa.

Ni mara ngapi umepata mafunzo au hamasa ya kubadili maisha yako, ukatoka na msukumo mkubwa na kwenda kuanza kubadili maisha yako? Najua ni mara nyingi sana. Lakini umekuwa unaishia wapi? Wewe mwenyewe unajua jinsi ambavyo msukumo unaoanza nao huwa haudumu muda mrefu, hasa pale unapokutana na uhalisia.
Tunapopata mafunzo au hamasa, huwa tunaangalia uimara wetu na kuanza nao. Lakini tunapuuza kabisa udhaifu tulionao, kwa kudhani hamasa tuliyonayo itayashinda madhaifu hayo. Nimewahi kukuambia hili na narudia tena, unayaita madhaifu kwa sababu huyapendi, ila yana uimara wa kukukwamisha kuliko hata uimara ulionao wa kupata unachotaka.
Unapanga kuchukua hatua fulani kila siku, labda ni kusoma, kufanya mazoezi, kuandika au kuweka akiba. Una hamasa kubwa ya kufanya na kweli unaanza kufanya. Mambo yanaenda vizuri tu, lakini sasa, uhalisia unaingia kwenye picha. Inakuja siku ambayo umebanwa kweli kweli na hupati kabisa nafasi ya kufanya kile ulichopanga.
Kwa bahati mbaya sana, kwenye mipango yako yote huwa unaziangalia siku nzuri tu. Unakuwa huna kabisa mpango wa siku mbaya, siku ambazo huwezi kabisa kutekeleza yale uliyopanga. Na hizo ndizo siku zinazoamua matokeo utakayoyapata.
Inapotokea mara moja, unadhani ni bahati mbaya tu, na wakati mwingine utaweza kufanya vizuri zaidi. Lakini huwa zinajirudia na hivyo ndivyo mipango yako mingi mizuri imekuwa inakwama bila kukupa matokeo.
Ninaposema mafanikio yako yanaamuliwa zaidi na madhaifu kuliko uimara wako namaanisha ni jinsi unavyoweza kuvuka hizo hali ambazo haziendani na mipango uliyoweka. Hali zinaweza kuwa za nje au za ndani, cha msingi ni jinsi unavyoweza kuzizuia zisiharibu mipango uliyoweka.
Kwenye barua hii, unakwenda kujifunza jinsi ya kuhakikisha unavuka nyakati zinazoenda kinyume na mipango yako bila kukwama kwenye kutekeleza mipango hiyo. Hapa ndipo unapoyanyima madhaifu yako nguvu ya kukuzuia kupata mafanikio makubwa.
1. Tengeneza Mzunguko Wa Mipango Na Utekelezaji.
Kuweka mipango mizuri ya mafanikio haijawahi kumshinda mtu yeyote yule. Tena kwa zama hizi za Akili Mnemba, hata kama huwezi kuamua nini cha kufanya, kuiuliza AI inakupa mpango kabisa.
Umekuwa unafurahia ubora wa mipango mizuri unayoiweka, lakini bado umekuwa hupati matokeo. Na unajua kwa nini.
Unapoanza kutekeleza mipango uliyoweka, unakutana na mambo ambayo hukutegemea kukutana nayo. Huenda ni ugumu ambao hukutegemea au matokeo yanakuja tofauti na matarajio.
Ni kwenye hali hiyo ndipo udhaifu mkubwa unapokuzuia kupata mafanikio. Kwa hali unayokuwa umekutana nayo, unaamua kubadilisha mipango uliyoweka. Na huo ndiyo unakuwa mwisho wa safari, kwani hata ubadilishe mipango kiasi gani, bado mambo usiyotegemea yatatokea.
Njia ya kukabiliana na huu udhaifu ni kutenganisha mipango na utekelezaji. Unajipa muda wa kuweka mipango, na unapitia kwa kina, pamoja na changamoto unazoweza kukutana nazo.
Ukishaweka mipango, unaenda kwenye hatua ya utekelezaji. Na hapo, utatekeleza kama ulivyopanga bila kujali umekutana na nini. Hata ushawishike kiasi gani kubadili mipango, usifanye hivyo. Tekeleza kwanza kama ulivyopanga kabla ya kubadili.
Kisha rudi kwenye meza ya mipango, tathmini utekelezaji, ona maboresho yanayopaswa kufanyika, boresha mipango na kisha nenda tena kwenye utekelezaji. Mzunguko huo utakuwezesha kupiga hatua kubwa kuliko kubadili mipango katikati ya utekelezaji.
Unapoweka mipango, jipe kabisa hatua za utekelezaji na muda wa kujitathmini katika utekelezaji huo. Na usikimbilie kubadili mambo katikati ya utekelezaji, tekeleza kwanza, kuna mengi utakayojifunza na ukifika wakati wa tathmini utaweza kuboresha.
Kwa kifupi, panga na tekeleza kama ulivyopanga bila kubadilika mambo yanapokuwa tofauti na matarajio. Hilo lina nguvu ya kukupa matokeo makubwa kuliko ambavyo umekuwa unapata kwa kuhangaika kubadili mipango kila wakati.
2. Tengeneza Mazingira Ya Madhaifu Kushindwa Bila Kupambana Nayo.
Unataka upate umakini mkubwa wa kutekeleza majukumu muhimu kwako. Lakini simu yako inakuwa usumbufu kwako, kila wakati inaita au kuna ujumbe unaingia. Mbaya zaidi ni pale unaposema uchungulie kwenye mitandao ya kijamii na unapotelea huko kabisa. Siku inaisha, uliyopanga kufanya hujayafanya, unailaumu simu. Kesho tena unarudia hivyo hivyo. Na bado unalalamika kwa nini unashindwa kupata mafanikio unayoyataka.
Unataka utozwe gharama kiasi gani kuambiwa kwamba ‘hutoboi’ kwenye umakini kama chanzo kikuu cha usumbufu kipo na wewe muda wote? Yaani umeandaa mazingira ambayo udhaifu wako una nguvu ya kukuzuia.
Na tiba hapo ni rahisi, badili mazingira yako. Tengeneza mazingira ambayo madhaifu yako yanakosa nguvu ya kukukwamisha, bila hata kupambana nayo moja kwa moja.
Kwa mfano wa usumbufu wa simu, tenga muda na aeneo ambalo utafanya kazi kwa umakini bila kuwa na simu karibu. Na kuwa na vipindi ambavyo umakini wako wote unaenda kwenye kile unachofanya bila hata kuiona kabisa simu yako.
Ni rahisi kupeleka umakini wako kwenye kitu unachofanya, kama kile kinachokusumbua hakipo kabisa, kuliko kupambana kukataa kitu hicho. Kama unadhani unaweza kujizuia kushika simu yako ukiwa unaiona, au kupuuza kuipokea wakati inaita, basi hujajua kwa nini mpaka sasa unakwama.
Narudia tena, madhaifu yana nguvu kuliko uwezo wako wa kuyakabili, usihangaike hata kushindana nayo, wewe tengeneza mazingira ambayo madhaifu hayo hayapati nafasi kabisa.
Karibu kwenye #BaruaYaKocha ujifunze kikamilifu mambo matano ya kufanyia kazi ili kuzuia madhaifu yako yasiwe kikwazo kwako kufanikiwa.
Soma barua hapa; #BZK048; Mafanikio Yako Yanaamuliwa Zaidi Na Madhaifu Kuliko Uimara Wako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.