Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kama umenisoma na kunifuatilia kwa muda, unaujua wazi msimamo wangu inapokuja kwenye fedha. Fedha ni moja ya maeneo matatu tunayoyafanyia kazi kwa uhakika, mengine mawili yakiwa Mafanikio na Biashara.
Na kwenye fedha, lengo letu ni kujenga Utajiri na kufikia Uhuru wa Kifedha. Hilo halitakuja kubadilika, kwa sababu ni wajibu wa kila mmoja wetu kutimiza.
Lakini pia nimekuwa nakushirikisha kuhusu fedha kuweza kununua furaha. Nimekuwa napinga wazi wazi dhana kwamba fedha haiwezi kununua furaha. Na watu wanatumia hilo kubeza umuhimu wa fedha.
Nimekuwa nakueleza wazi jinsi ambavyo fedha ni muhimu kwenye maisha yetu. Ikitoka hewa tunayopumua bure, kinachofuata kwa umuhimu ni fedha, kwani kuna wakati unaweza hata kuikosa hiyo hewa na fedha zikakusaidia kuipata.
Hivyo kwa kifupi, fedha ni muhimu sana na tunao wajibu wa kimaadili kabisa wa kuhakikisha tunazipata fedha kwa kiasi cha kutosha.
Lakini sasa, fedha hizo hizo zinaweza kuwa mtego kwako kama hutaelewa na kujipanga vizuri. Watu wengi wameishia kukwama kwenye kupata fedha kwa sababu wanataka sana kupata fedha.
Sijui kama umenielewa vizuri hapo, yaani, kwa kutaka sana kupata fedha, unaishia kutokupata fedha hizo kwa kiwango ambacho ungeweza kufanya. Hiyo inamaanisha kwamba kuna watu wanakwama kupata fedha kwa sababu wanataka zaidi kupata pesa.
Hilo ndiyo nataka kukuambia kwenye barua hii, ulielewe bila kuruhusu likukwamishe kupata fedha. Naangalia njia nzuri ya kukueleza hili ili usije ukatoka na tafsiri tofauti kwamba fedha siyo muhimu au siyo kipaumbele.
Unaweza kuzipa fedha umuhimu na kipaumbele, na hilo lenyewe likawa kikwazo kwako kupata fedha. Lakini kuna namna ya kuweka umuhimu na kipaumbele hicho cha kifedha kwa namna ambayo hutajikwamisha wewe mwenyewe.

Kuangalia Kipato Pekee Kunavyoharibu Ubora.
Mitandao ya kijamii huwa inategemea watumiaji kuweka maudhui na kushirikiana na wengine. Ili kuhakikisha mitandao hiyo inapata watumiaji wengi na wanaotumia muda wao mwingi kwenye mitandao hiyo, kumekuwa na mpango wa kuwalipa watumiaji.
Mitandao yote mikubwa ya kijamii ina mpango wa kuwalipa watumiaji ambao wanakuwa na watumiaji wengi wanaofuatilia maudhui yao. Mitandao kama Youtube, Facebook, Instagram, Tiktok na X (Twitter) ina hiyo huduma ya kuwalipa watumiaji wenye wafuasi wengi.
Mtandao wa X (Twitter) ni moja ya mitandao ambayo imekuwa inawalipa vizuri wale wanaokidhi vigezo. Na kigezo chao kikubwa kikiwa idadi ya wafuasi ambao wanafuatilia maudhui ya mtu. Siyo tu idadi ya wanaomfuatilia (followers) bali idadi ya wanaojihusisha na maudhui yao (impressions).
Mtandao huo ulifanya jaribio moja ambalo lilitoa matokeo ya kushangaza. Walichukua watumiaji 30 wanaolipwa sana na kuzuia akaunti zao zisionekane kwa asilimia 3 ya watumiaji wa mtandao huo. Matokeo yake ni wale ambao hawakuonyeshwa akaunti hizo walitumia zaidi mtandao huo na kwa muda mrefu zaidi.
Twende taratibu hapo ili tuelewane; mitandao imekuja na mpango wa kuwalipa watumiaji wenye maudhui yanayofuatiliwa na wengi. Wale wanaolipwa sana, maudhui yao yakiondolewa, watumiaji wanatumia zaidi mtandao.
Unaona tena hapo jinsi fedha zinavyoharibu nia njema iliyowekwa. Kwa sababu mitandao inawalipa watu kwa maudhui yao kuangaliwa na wengi, watu hao wanaweka maudhui mengi yasiyo na tija, ila yanayonasa umakini wa watu (click bait). Watu wanapokutana na maudhui ya aina hiyo kwa wingi, wanapunguza kutumia mtandao husika. Hivyo lengo la kuweka fedha ili kuvutia watumiaji, linaleta matokeo ambayo ni kinyume kabisa, yanapunguza watumiaji.
Hapo tunaona jinsi ambavyo fedha zinachangia kuharibu ubora wa kitu, pale watu wanapokuwa wanaangalia fedha pekee. Na kuna maeneo mengi ambayo tunaharibu ubora kwa kuangalia tu fedha tunazopata.
Sheria Ya Goodhart (Goodhart’s Law).
Mwaka 1975, Charles Goodhart, aliyekuwa mchumi wa nchini Uingereza aligundua kwamba mifumo na tabia za binadamu huwa zinabadilika pale utendaji unapopimwa na malipo au zawadi kutegemea matokeo.
Alichogundua kinaitwa Sheria Ya Goodhart (Goodhart’s Law) ambayo inasema; “Pale kipimo kinapokuwa lengo, kinaacha kuwa kipimo kizuri”.
Sheria hiyo inajidhihirisha wazi pale fedha inapotumika kama kipimo, halafu kipimo hicho kinageuka kuwa lengo. Kwa mifano tuliyoangalia hapo juu, kote fedha iliwekwa tu kama kipimo, lakini ikageuka kuwa lengo na matokeo yake mambo yakawa mabaya.
Tunapaswa kuielewa sheria hiyo ya Goodhart vizuri sana na kuitumia kwenye maamuzi yote tunayofanya ili tunapojenga mafanikio na utajiri, yawe ya kweli kwetu na siyo kuwa kikwazo kinachotukwamisha.
Jinsi Ya Kuepusha Umuhimu Na Kipaumbele Cha Fedha Kuwa Kikwazo Kuzipata.
Kwa kuwa tumeiona hatari ya kufanya fedha kuwa kipaumbele inavyoweza kutuzuia kupata fedha zaidi, tunapaswa kuchukua hatua za kuzuia hilo lisitokee.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo matano ya kufanyia kazi ili kuhakikisha pesa inabaki kuwa kipaumbele kwako, lakini haiwi kikwazo kwako.
Hii siyo barua ya kukosa kusoma kama kweli umedhamiria kupata mafanikio makubwa, utajiri na kuwa na furaha. Mambo hayo matano unayoenda kujifunza ndiyo nguzo imara kwako kujenga utajiri utakaodumu na kuendelea kukua.
Karibu uisome barua hiyo hapa; #BZK034; Siamini Kama Nakuambia Hivi Kuhusu Fedha, Lakini Lazima Nikuambie.
Kocha