Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Moja ya vitu vyenye nguvu sana ambavyo nimewahi kujifunza na ndiyo vimeleta mapinduzi makubwa kwangu na wote mnaofuatilia kazi zangu ni uhusika wetu kwenye matokeo tunayopata.
Nimejifunza na kuamini kwamba matokeo tunayoyapata, ni sisi wenyewe tumeyasababishe, iwe kwa kujua au kutokujua. Tunaweza kulalamika na kulaumu vyovyote tunavyotaka, lakini inaporudi kwenye chanzo hasa, sisi wenyewe ndiyo wahusika namba moja.
Kujua, kuamini na kuishi kwa msingi na mwongozo huo kunakupa nguvu na uhuru mkubwa. Kunakufanya ushike hatamu ya maisha yako na kuchukua hatua za tofauti ili upate matokeo ya tofauti.
Lakini hilo huwa siyo rahisi kama wengi wanavyodhani. Kwani kuna vitu vidogo vidogo ambavyo huwa vinaendelea kwenye maisha yetu na kuwa kikwazo kwetu kuyabadili.
Tunajua jinsi ambavyo fikra zina nguvu kwenye maamuzi tunayofanya, hatua tunazochukua na matokeo tunayopata. Tunakuwa vile tunavyofikiri kwa muda mrefu. Yaani kile kinachoonekana kwako sasa, ni matokeo ya fikra ambazo umekuwa nazo.
Tunafundishwa sana kuhusu kuwa na fikra chanya na za uwezekano mara zote. Tunapewa njia mbalimbali za kuhakikisha fikra hizo chanya zinakuwepo na kudumu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, fikra hasi huwa zina njia ya kujipenyeza na kuingia kwenye akili zetu. Kwa bahati mbaya sana, fikra moja hasi, tena ndogo sana, inaweza kufuta fikra 100 chanya ambazo umekuwa nazo.
Kama ambavyo tone moja la sumu linaweza kuharibu pipa zima la maji, ndivyo fikra moja hasi inavyoweza kuharibu akili yako yote na kuwa kikwazo kwako kupata mafanikio unayoyataka.
Pamoja na madhara hayo makubwa ya fikra hasi, hata ambazo zipo kwa udogo sana, bado wengi hatuna kinga ya fikra hizo hasi, zinazojipenyeza.
Na fikra hasi huwa zinajipenyeza kwetu kwa njia ambazo hatuzitegemei. Njia kama utani, ambao unaweza kuonekana wa kawaida tu, zina nguvu ya kuharibu kabisa fikra zetu na kutukwamisha.

Usiruhusu Fikra Hasi Hata Kwa Utani.
Rafiki, kuna watu wengi wanaoelewa madhara ya fikra hasi na kuziepuka, lakini bado zinawaathiri kwa sababu wanakosa ukali unaohitajika kwenye kuziondoa fikra hasi.
Aliyekuwa mpiganaji na mwigizaji Bruce Lee amewahi kuwa na nukuu yenye nguvu sana juu ya hili. Alisema; “Kamwe usijiongelee hasi, hata kama ni kwa utani. Mwili wako haujui tofauti. Maneno yana nguvu ya kuumba. Badili jinsi unavyojiongelea na utaweza kuyabadili maisha yako.”
Maneno hayo yana nguvu kubwa sana ya kuyabadili maisha yako, kama utayachukua na kuyaishi kwenye maisha yako.
Kwenye barua hii tunaenda kuongeza ukali wetu kwenye kuondoa kila aina ya fikra hasi zinazojipenyeza kwetu na kutukwamisha kufanya makubwa.
1. Futa Kabisa Fikra Hasi.
Kumekuwa na mjadala mkali iwapo inawezekana mtu kufuta kabisa fikra hasi kwenye akili yake. Hiyo inatokana na hali yetu binadamu, ambapo kuna mambo yakitokea yanachochea fikra hasi yenyewe.
Ukweli ni kwamba, hatuwezi kudhibiti nini kinatokea kwenye maisha yetu, lakini tunaweza kudhibiti jinsi tutakavyopokea hicho kitakachotokea. Mambo mabaya yatatokea kwetu, hilo hatuwezi kulizuia. Lakini kuruhusu mambo hayo mabaya yaibue fikra hasi ndani yetu, hilo lipo ndani ya uwezo wetu kudhibiti.
Hivyo, inawezekana kabisa kufuta fikra zote hasi tunazokuwa nazo kwa kudhibiti namna tunavyochukulia yale yanayotokea. Hilo linaanza na maandalizi kabla hata ya jambo lolote halijatokea. Ukisubiri mpaka jambo litokee ndiyo ukabiliane nalo, unakuwa umeshachelewa.
Moja ya maandalizi bora unayoweza kuwa nayo juu ya lolote linaloweza kutokea na kuzuia lisiibue fikra hasi ndani yako ni kuamini kwamba kila jambo linalotokea ni zuri na lenye manufaa kwako. Ndiyo, kila kinachotokea, hata kama kinaonekana ni kibaya kiasi gani, jibu lako la kwanza linapaswa kuwa ni kushukuru kwa sababu ni kitu chenye manufaa kwako.
Huenda unajiuliza, vipi kama ni msiba wa mtu wa karibu unayempenda sana? Jibu unalo, ni kitu kizuri na chenye manufaa kwako. Kama unashangaa kwa hilo, huenda hujaelewa gharama ya kupata mafanikio makubwa na kwa nini barua hii ni ya kuongeza ukali kwenye kuziondoa fikra hasi.
Kuchukulia kila jambo kama zuri na lenye manufaa kwako siyo kitu cha kujidanganya au kujifurahisha. Bali ndiyo uhalisia, hata kama umepoteza kitu cha thamani kiasi gani, kuna namna hilo linakuwa na manufaa kwako. Utayaona manufaa hayo pale utakapotaka kuyaona.
Umekuwa unaona yanayokutokea kama mabaya, kwa sababu tayari unayafikiria ni mabaya. Unaweza kupoteza kazi au biashara ikafa, ukiona ni jambo baya, itakuzuia hata kupata kazi nyingine au kuanzisha biashara nyingine. Lakini ukichukulia ni kitu kizuri, inakuweka huru kutumia kama fursa ya kufanya vitu vya tofauti.
Kadhalika hata kwenye kuwapoteza watu. Unaweza kupoteza watu ambao ni wa muhimu sana kwako na kuona maisha hayawezi kwenda bila wao. Lakini unapochukulia kama kitu kizuri, unatumia kujenga maisha bora kupitia ule uzuri watu hao walikuwa nao kwako.
Najua hili siyo zoezi rahisi, kwa sababu kwa maisha yako yote umefundishwa na kuzoeshwa kupokea kwa fikra hasi mambo yote ambayo ni tofauti na matarajio yako.
Hiyo ndiyo kazi yako kubwa ya kwanza kuifanya, kufuta kabisa kila aina ya fikra hasi ambazo umezoea kuwa nazo kutokana na hali unazokuwa unapitia.
2. Utani Una Nguvu Kuliko Unavyodhani.
Huwa tunachukulia utani kama kitu cha juu juu tu na kisicho na madhara yoyote. Hivyo tunajiambia mambo hasi sisi wenyewe kwa kuona ni utani au masihara tu. Lakini pia tunawaruhusu watu wengine kutuambia mambo hasi kwa sababu ni utani.
Sikiliza rafiki, hapa naenda kukufundisha kitu ambacho kitakufanya uonekane ni wa ajabu na usiyependa utani. Lakini kama tunavyojua, mafanikio siyo rahisi, ndiyo maana wachache ndiyo wenye nayo.
Kuanzia sasa kataa kabisa aina yoyote ya utani ambayo inahusisha mambo hasi. Hilo unaanza kulikataa kwako mwenyewe. Hutajitania au kujichukulia kwa namna yoyote hasi, hata kama ni vitu vidogo. Hata kama kuna kosa ambalo umefanya, hupaswi kujilaumu kwa kujichukulia hasi, badala yake unapaswa kujiadhibu kwa kufikiria chanya.
Kama umechelewa mahali, usijiambie wewe ni mchelewaji, badala yake jipe adhabu ya kuhakikisha mara zote unawahi. Hata kama huna pesa kabisa, usijiite masikini, bali jiite tajiri ambaye uko kwenye mchakato. Usiruhusu kabisa fikra na maneno hasi kukuhusu wewe na yale unayofanya.
Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kufanya kwa wengine. Usimruhusu mtu yeyote yule akuambie jambo ambalo ni hasi, hata kama anasema ni utani. Usuwaruhusu kabisa watu kukuambia wewe ni mjinga, mpumbavu, masikini, uliyeshindwa na mengine ya aina hiyo.
Kwanza hakikisha huwapi watu sababu ya kukuita maneno hayo, kwa kuhakikisha unajituma sana kwa upande wako. Ukiahidi unatimiza, unatekeleza kile unachopaswa na mara zote unapambana kuwa bora zaidi. Ukishawanyima watu sababu halali ya kukuita majina hasi, unawakataza kukupa majina hayo hasi kwa utani. Maana watu watakuita maneno hayo kwa kivuli cha utani, hupaswi kuruhusu hilo kabisa.
Epuka pia kukubali kauli hasi zinazotolewa kimakundi. Jitenge na kundi lolote linalojivunia kwenye hali hasi au kuzikubali. Unaposikia watu wanatumia kauli kama; ‘sisi wanyinge’, epuka kabisa kuwa mmoja wa hao. Wewe siyo mnyonge, hizo ni fikra hasi ambazo ukiziruhusu, unakuwa mnyonge kweli.
Unaweza kuona ni utani tu na hauna madhara yoyote, lakini siyo kweli. Kila neno na fikra unayoipa nafasi, inaacha athari fulani kwako.
Huwa kuna kauli; ‘Ukitaka kumuua mbwa, mpe kwanza jina baya.’ Unaporuhusu kauli yoyote hasi kwako, iwe inaanzia kwako au kwa wengine, hata kama ni ya utani, inaenda kukukwamisha kwenye mafanikio unayoyatak.
Kuwa mkali na kataa chochote hasi, hata kama ni kwa utani. Hupaswi kuwa na utani na mafanikio yako makubwa. Yatengeneze na yalinde kwa gharama yoyote ile, hasa inapokuja kwenye fikra unazokuwa nazo.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha kuna mambo ya ziada matatu ya kuzingatia kwenye kuhakikisha unaondokana kabisa na utani hasi ambao umekuwa unakukwamisha. Soma barua hiyo ili usijiwekee vikwazo kwenye mafanikio yako mwenyewe.
Isome barua hiyo hapa; #033; Usiruhusu Kitu Hiki Kitokee Hata Kwa Utani Kwenye Maisha Yako.
Kocha