Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kama ni msomaji mzuri wa barua hizi, utagundua kuna vitu viwili ambavyo navirudia rudia sana kwenye hizi barua; kuchukua hatua na kuweka kazi kwa juhudi kubwa. Kama umechoka kusikia vitu hivyo, naamini utakuwa umeshapata matokeo makubwa unayoyataka. Kama bado hujayapata, basi jua unahitaji kuvisikia mara maelfu huko, kwa sababu ndiyo vitu viwili vinavyowakwamisha watu kwenye zama hizi.

Kwa sababu, ukiangalia, hakuna tena kitu kikubwa kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Wewe hapo, na bilionea namba moja duniani mnaweza kutumia akili mnemba (AI) na mkapata majibu yanayofanana kwenye jambo moja. Bilionea akapata matokeo makubwa kwenye majibu hayo, wewe usipate matokeo.

Kwa sasa maarifa siyo kikwazo tena, yanapatikana kwa yeyote bila ukomo. Ujuzi pia siyo kikwazo tena, mtu anaweza kupata huduma yoyote ya kitaalamu hata kama hana elimu au uwezo wa kulipa wataalamu.

Kwenye zama hizi ambazo uwanja wa mapambano umewekwa sawa kwa wote, tofauti pekee ni utayari wa kuchukua hatua na kuweka kazi kwa juhudi kubwa na kwa muda mrefu bila kuacha. Kwa hiyo basi, nielewe na nivumilie ninaporudia rudia mambo hayo, kwa sababu ndiyo muhimu zaidi. Na sisi binadamu, tunahitaji zaidi kukumbushwa kuliko kufundishwa.

Ninapokutana na taarifa za mtu ambaye anaweka juhudi kubwa za kazi na kupata matokeo makubwa, huwa zinanisisimua sana. Na huwa napenda kujifunza kutoka kwenye hizo juhudi, ili na mimi niweze kuboresha juhudi zangu na kuleta matokeo makubwa.

Hivi karibuni nimekutana na taarifa za mwamba mmoja wa kazi, ambazo zilinifanya ninyooshe mikono juu kwa kuona mimi bado nacheza. Mwamba alikuwa anaweka kazi hasa na matokeo yalikuwa yanaonekana wazi. Kwenye barua hii tunaenda kumwangalia mwamba huyo, tumpe maua yake na kujifunza kutoka kwake.

Napoleon Bonaparte, Mwamba Wa Kazi Aliyeibadili Dunia.

Napoleon Bonaparte aliyekuwa jenerali wa jeshi na mtawala wa Ufaransa, alikuwa ni mchapakazi wa kipekee sana kuwahi kuwepo hapa duniani. Alikuwa na nguvu za kipekee sana, nidhamu binafsi ya hali ya juu na alikuwa mtu wa kuchukua hatua, mwenye msukumo wa ndani wa kufanya makubwa.

Kujitoa kwake kikamilifu kwenye kila alichofanya, kulimpa matokeo makubwa sana, kuweza kuwa jenerali wa jesho katika umri mdogo, na pia kuwa mtawala wa Ufaransa licha ya kutokutokea familia za watawala. Kwa kipindi cha miaka 22, alipigana kwenye zaidi ya mapambano 70, huku akishinda mengi ambayo haikutegemewa ashinde.

Napoleon ndiye aliyebadili kabisa mikakati ya kivita, yeye kama jenerali akiwa mstari wa mbele wa mapambano badala ya kukaa eneo salama na kutuma wanajeshi wake. Aliweza kufanya hayo hata wakati akiwa mtawala wa Ufaransa, kitu ambacho hakikuwahi kushuhudiwa.

Kwa kujitoa huko na matokeo hayo makubwa ambayo mwamba aliyapata, ikanilazimu kuchimba ndani zaidi ili kujua aliwezaje kuweka kazi kiasi hicho. Na haya ni mambo ambayo nimejifunza kutoka kwa huyu mwamba moja kwa moja, ambayo na sisi tunapaswa kuyafanyia kazi ili tupate matokeo makubwa tunayoyataka.

Wakati Napoleon alifanya hayo kushinda vita na kuangusha wapinzani, sisi tunayafanya kujenga mafanikio makubwa na yenye manufaa kwetu na watu wengine.

1. Kufanya Kazi Masaa Mengi.

Hatua ya kwanza ya kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni kwenye muda ambao mtu anaweka kwenye kazi. Napoleon aliweka masaa mengi kwenye kazi, yeye mwenyewe alikuwa anakiri kuweka masaa 16 ya kazi kwa siku, kila siku. Msaidizi wake wa karibu anasema alifanya kazi mpaka masaa 18. Na hapo ni kipindi cha amani.

Wakati wa vita, hakuwa analala kabisa, alikesha usiku kucha akipanga mashambulizi na mchana akiyaongoza. Inaelezwa kwamba alikuwa akitenga muda wa kusinzia kwa dakika chache, hata kama ni katikati ya mapambano makali.

Napoleon anaandika: “Mara zote niko kwenye kazi…. Nafanya kazi muda wote, muda wa kula, wa kupumzika. Naamka usiku ili kuendelea na kazi.”

Napoleon anaposema alifanya kazi muda wote, anamaanisha kweli. Maana inaripotiwa alikuwa anaamka saa moja asubuhi na siku nzima ilikuwa imepangiliwa kwa kazi. Hata wakati anaoga, alikuwa na mtu anamsomea habari za siku. Alikuwa na dakika 15 tu za kula mchana. Alifanya kazi mpaka usiku, na hata alipolala, aliamka tena usiku wa manane kuendelea na kazi.

Wakati wa vita na safari, alikuwa anatembea na ofisi yake nzima. Akiwa na vitabu na ripoti mbalimbali za kupitia na kufanya maamuzi. Alikuwa mtu wa kuandika sana barua na alikuwa akiongea huku wasaidizi wake wakiandika.

Ili kuweza kufanya kazi kwa tija kwa masaa yote, Napoleon aliepuka sana kufanya jambo zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Anaeleza kwamba alikuwa anachukulia majukumu yake kama madroo ya kabati. Analifungua na kufanyia kazi, kisha anafunga na kufungua jingine. Alipokuwa kwenye juhuku moja, aliweka umakini wake wote hapo. Akihamia kwenye jukumu jingine, hilo analifunga na kufungua hilo jingine.

Hata kulala, anasema alipoamua muda wa kulala, alifunga macho na kulala hapo hapo. Hakuwa na mawazo yanayomzonga na kumzuia kufanya. Na hilo lilimwezesha kufanya kazi sana, kwa sababu pale alipopumzika, alipumzika hasa badala ya kuendelea kufikiria kazi.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha sifa nyingine 5 za Napoleon ambazo zilimfanya apate matokeo makubwa sana kupitia uchapakazi wake. Ni mambo ya msingi kwako kuyajua ili usiishie kuweka kazi ambayo haina tija.

Soma barua hiyo hapa; #BZK066; Mwamba Wa Kazi Huyu Hapa, Tumpe Maua Yake, Na Kujifunza Kutoka Kwake