Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Hatuwezi kujua kila kitu na wakati wa kufanya maamuzi tunakuwa na mengi ambayo hatuyajua. Hilo linatusukuma kujifunza na kuomba au kuchukua ushauri kwa watu wengine.
Kutokana na uharaka wa maamuzi tunayopaswa kufanya, huwa tunakuwa kwenye hatari ya kupokea ushauri ambao unaishia kutupoteza kuliko kutusaidia. Na ushauri huo hauwi mbaya kwa sababu wanaotupa wanakuwa wamedhamiria kutupoteza, bali kwa sababu ambazo anayetoa na anayepokea hajui.
Unaweza kutoa au kupokea ushauri kwa nia njema kabisa, lakini kwenye utekelezaji mambo yakawa tofauti sana na ilivyotarajiwa. Ndiyo maana nimekuwa nakusisitiza na hapa naendelea kukusisitiza umuhimu wa kuwa makini na ushauri tunaopokea au kutoa kwenye safari yetu ya mafanikio.
Hili ni eneo muhimu ambalo utaona nalisisitiza sana, kwa sababu kwa zama hizi za mitandao ya kijamii na akili mnemba, ushauri ni mwingi na unaochanganya. Kwa sasa hupambani tu na ushauri wa watu, bali pia ushauri wa akili mnemba (AI).
Na ushauri wa akili mnemba ndiyo hatari zaidi kwa sababu haina majuto, yenyewe inakuambia kile ambacho kinakubalika na wengi na siyo kitakachofanya kazi kwako. Hilo linafanya hili eneo la kujifunza na kuchukua ushauri liwe hatari na linalohitaji umakini mkubwa.
Ili kuhakikisha hatupotezwi na ushauri usiokuwa sahihi, barua hii inaenda kugusa mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kutoa au kupokea ushauri kwenye jambo lolote. Iwe ni kwa binadamu wenzetu au akili mnemba, hakikisha mambo haya unayazingatia.

1. Watu Wengi Wanakupa Ushauri, Wakati Unachohitaji Ni Mwongozo.
Unapowaomba watu ushauri, wanakuambia kile ambacho wao wamewahi kufanya kwenye hali kama hiyo au wangefanya kama wangekuwa kwenye hali kama yako. Pamoja na kwamba wanachokushauri kinaweza kuwa sahihi, lakini wewe siyo wao, kilichofanya kazi kwao, hakiwezi kufanya kazi kwako.
Na hapo ndipo ushauri mwingi sana unapokuwa hatari. Kwa sababu hata mtu anayetoa ushauri, akirudia kile alichowahi kufanya huko nyuma, hakiwezi kumpa matokeo yale yale tena.
Kitu ambacho unahitaji ili utoke popote ulipokwama siyo ushauri bali ni mwongozo. Tayari unajua nini unapaswa kufanya, unachokosa ni mwongozo wa hatua gani uanze nayo na uendeje hatua kwa hatua mpaka upate matokeo.
Ushauri unatolewa kwa dakika chache, unamweleza mtu shida yako, na anatoa ushauri. Ndiyo maana wengi huwa wanakimbilia ushauri, hauhitaji kazi kubwa.
Mwongozo unahitaji muda kutolewa, kwa sababu siyo kama shuka ambalo linaweza kumfunika mtu yeyote. Bali ni shati ambalo mtu lazima apimwe na lishonwe ndiyo aweze kulivaa. Kwa ugumu huu wa mwongozo, watu wamekuwa wanauepuka.
Socrates, amekuwa akichukuliwa kama mtu mwenye hekima zaidi kuwahi kuwepo hapa duniani. Lakini unajua Socrates hajawahi kumshauri mtu kitu chochote? Ndiyo, mtu alikuwa akienda kwake kutaka ushauri, yeye alimuuliza maswali tu. Mtu alijijibu maswali yake na kupata majibu ya alichokuwa anataka kwenye kujibu maswali hayo.
Hilo ni zoezi linalohitaji muda wa kutosha, na wengi hawana muda, siyo mtoaji wala mpokeaji. Hivyo wanakimbilia njia ya mkato ya ushauri na matokeo yanakuwa siyo mazuri kwao.
Unapoangalia mfumo wa hizi barua na mafunzo mengine unayopata hapa, haijakaa kukuambia nini hasa ukafanye, bali ni mwongozo wa kukusaidia wewe uweze kujua nini unapaswa kufanya.
Hata barua hii ya kuhusu ushauri, haikuambii ni ushauri gani uchukue na upi usichukue, bali inakupa mwongozo wa namna ya kupata ushauri ulio sahihi.
Wengi hawafanyii kazi miongozo kwa sababu wanaona ni kazi kubwa, na hilo linaeleza kwa nini hawapati mafanikio makubwa. Wewe usiwe kama hao wengi, epuka sana ushauri na penda kupata miongozo, kwa sababu itakusaidia zaidi ya mara moja. Ukishapata mwongozo, unaweza kuutumia kwa maeneo mbalimbali, tofauti na ushauri unaolenga eneo moja na bado pia hausaidii.
Karibu usome #BaruaYaKocha ujifunze kwa kina tahadhari ya kuwa nayo inapokuja kwenye ushauri ambao watu wengi wapo tayari kukupa bure kabisa.
Soma barua hiyo hapa; #BZK065; Ushauri Mwingi Unakupoteza Kuliko Kukusaidia, Kuwa Makini