Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tabia zinazohitajika mtu kuwa nazo ili aweze kujenga na kudumu kwenye mafanikio makubwa ni nyingi na zipo wazi. Wengi wanazijua zile tabia za moja kwa moja ambazo zinahusisha kufanya au kutokufanya vitu.
Tabia kama za kutunza muda, kuweka umakini kwenye jambo moja na kutoa thamani kubwa kwa wengine huwa zipo wazi kwa kila mtu. Tabia hizo na nyingine zinazofanana na hizo zinaonyesha wazi nini ambacho mtu anatakiwa kufanya ili kupata matokeo bora.
Lakini pia zipo tabia nyingine ambazo zinahusisha zaidi sifa anazokuwa nazo mtu, zinazokuwa muhimu sana kwenye kujenga na kudumu kwenye mafanikio. Tabia hizo hazihusishi kufanya au kutokufanya moja kwa moja, bali zinahusisha namna mtu anavyochukulia mambo anayokabiliana nayo.
Moja ya tabia hizo, ambayo ina thamani kubwa na muhimu sana kwenye mafanikio ni kuwa na uvumilivu kwenye hali ya kutokuwa na uhakika. Hii ni tabia ambayo siyo maarufu sana kama tabia nyingine za mafanikio, lakini inahitajika sana kwenye kujenga mafanikio makubwa.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia umuhimu wa tabia hii na jinsi unavyoweza kuijenga na kuitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
1. Ni Rahisi Kuonekana Matokeo Yanapokuwa Ya Uhakika.
Nikikuambia upige simu kwa watu 100 na baadhi ya watu hao watanunua unachouza, itakuwa vigumu sana kwako kupiga simu hizo zote. Hiyo ni kwa sababu utakachokutana nacho hakitakuwa kinakupa uhakika sana.
Kuna ambao utawapigia hawatapatikana, kuna watakaopatikana ila hawatapokea. Wapo watakaopokea na kukuambia hawana muda uwatafute wakati mwingie. Na watakaokuwa na muda wa kukusikiliza watakuambia hawana uhitaji. Itakuchukua muda mpaka kuwapata kweli wenye uhitaji, na hapo hakuna uhakika kama hata utawapata.
Lakini nikikupa watu 10 ambao watanunua kwa uhakika na wajibu wako ni kuwapigia tu, utawapigia bila shaka. Kitendo cha kuwepo kwa uhakika kwamba watu hao wanahitaji na kinachohitajika kwako ni kuwapigia tu, kinakupa nguvu kubwa ya kufanya.
Ukiangalia kwa undani, mifano miwili niliyoshirikisha hapo juu ni kitu kimoja. Tofauti ipo kwenye kuwepo na kutokuwepo kwa uhakika. Kwenye mfano wa kwanza, ukiongea na watu 100, kuna uwezekano mkubwa wa kupata 10 wenye uhitaji, ila huna unahika. Kwenye mfano wa pili, ni watu 10 wenye uhakika.
Tunatamani sana maisha yatupe mfano wa pili, mambo ambayo ni ya uhakika. Lakini uhalisia wa maisha ni kinyume, yanatupa zaidi mfano wa kwanza, kuwepo kwa uwezekano mkubwa la kukosekana kwa uhakika.
Sehemu kubwa ya mafanikio inatokana na kuonekana, yaani kuwepo kwenye uwanja wa mapambano yanayokupa mafanikio. Sasa, huwa ni rahisi sana kuonekana pale matokeo yanapokuwa ni ya uhakika. Pale kila kitu kinapoeleweka na njia ni ya wazi, kila mtu anaichukua.
Hata kinachowafanya watu kuhangaika na fursa mpya kila wakati ni kutafuta hali ya uhakika. Mara nyingi watu huomba ushauri lakini kinachokuwa kimejificha nyuma ya mahitaji yao ni uhakika. Wengi huwa wanauliza ni biashara gani wakifanya watapata faida nzuri kwa uhakika.
Uhakika huwa ni hitaji kubwa sana la binadamu kwenye maisha. Na kila tunachofanya, ni kuhakikisha tunakuwa na uhakika zaidi. Lakini hayo ni matamanio yetu, maisha yana namna yake ya kwenda, ambayo haitegemei kabisa kile ambacho sisi tunataka.
2. Safari Ya Mafanikio Haijanyooka.
Licha ya sisi kutaka sana uhakika, maisha hayajanyooka, kwenye jambo lolote lile. Huwa kuna kauli ya utani inayosema, vitu pekee vyenye uhakika kwenye maisha ni viwili, kodi na kifo. Kwamba ni lazima utatozwa kodi, hata iweje na hakuna atakayeweza kukikwepa kifo, hilo ndiyo hitimisho la uhakika kwetu.
Kwenye sayansi na asili kuna kanuni kabisa ya kutokuwa na uhakika (uncertainity principle). Ambapo kanuni hiyo inasema, hata kutokuwa na uhakika nako hakuna uhakika. Kwa kifupi ni maisha hayana uhakika, hakuna kitu chochote ambacho kimenyooka kama tunavyotaka.
Safari ya jambo lolote kwenye maisha huwa ni ndefu kuliko ambavyo mtu anategemea. Hata ujipange na kujiandaa kiasi gani, kila kitu huwa kinachukua muda mrefu kuliko mategemeo ambayo mtu unakuwa nayo.
Kila safari pia huwa inakuwa na gharama kubwa kuliko ambavyo mtu anategemea. Kwa sababu ya urefu wa safari, gharama nazo huwa ni kubwa. Na hata mtu ujiandae na kujipanga kiasi gani, gharama huwa haziendi kama unavyokuwa umetegemea.
Kuna vipindi virefu ambavyo safari itaonekana kama imesimama. Licha ya mtu kuweka juhudi kubwa na kupambana sana, hakuna matokeo mapya yanayokuwa yanaonekana. Hakuna hatua kubwa ambazo mtu unakuwa umepiga. Unaonekana ukikimbia sana, lakini unakuwa umebaki pale pale.
Kadiri safari inavyokosa uhakika, ndivyo mtu unavyokuwa na wasiwasi mkubwa juu yako mwenyewe na safari nzima. Ndiyo unaanza kushawishika huenda njia uliyochagua siyo sahihi. Na hapo ndipo unaposhawishika kuiacha njia na kukimbilia vitu unavyodhani ni vya uhakika zaidi.
Huwa tunaona hali hii ya kukosa uhakika kama kikwazo na kukubali kuiacha safari. Lakini hayo yote yana mchango kwenye matokeo unayokwenda kuyapata. Ukitaka kujua umuhimu wa hilo, angalia watu wote waliopata matokeo ya haraka, iwe ni mafanikio au utajiri. Huwa wanaishia kupoteza kwa haraka pia.
Kumbe unapopitia ugumu na hali ya kutokuwa na uhakika, inakujenga na kukuandaa kupokea matokeo makubwa ya baadaye. Unaona kama unapoteza muda na kuchelewa, kumbe unaimarishwa uweze kuhimili mambo makubwa unayokwenda kuyapokea.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimeshirikisha mambo matano ya kukupa nguvu ya kujijengea tabia hii muhimu sana kwenye mafanikio yako. Hakikisha unayasoma na kuyafanyia kazi mambo yote matano ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Isome barua hiyo hapa; #BZK032; Uvumilivu Kwenye Kutokuwa Na Uhakika – Tabia Ya Thamani Kubwa Kwenye Kujenga Mafanikio.
Kocha