Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Huwa kuna dhana kwamba ukiwacheka au kuwadhihaki watu wenye changamoto fulani, basi na wewe utaipata changamoto hiyo. Ni imani kali tuliyojengewa, huenda kwa nia nzuri ya kuondoa hali ya unyanyapaa kwa watu wenye changamoto mbalimbali.

Watu wamekuwa wanaleta utani kwenye hilo, kwamba kama ukiwacheka watu unapata hali walizonazo, basi ukiwacheka wenye mafanikio pia unapaswa kupata mafanikio yao. Yaani watu hutania kwamba wanawacheka matajiri na utajiri wao, ili na wao wawe matajiri kama wao.

Watu wanachukulia hilo kama utani, lakini kiuhalisia ni kitu ambacho kinawezekana kabisa. Kama tunaamini kwamba tunaweza kuyapata mabaya ya wengine kwa kuwacheka, kwa nini isiwezekane kupata mazuri ya wengine kwa kuwacheka?

Dhana ya laana ipo sana kwenye jamii zetu. Kwamba tunaposhindwa kuwajali watu wetu wa karibu, hasa wale waliotuzidi umri na wenye ukaribu sana kama wazazi, wanaweza kutuachia laana na maisha yetu yakawa magumu. Watu wengi wanaamini kweli kwenye dhana hiyo ya laana na kujikuta wanabaki kwenye maisha magumu, ambayo hao wanaowaachia laana walikuwa nayo pia.

Lakini watu hawaamini kwenye upande wa pili wa laana, wa kuachiwa laana ya kupata ushindi na mafanikio. Wapo wanaoamini kwenye baraka, kwamba ukiwatendea vizuri watu wa karibu na wakakubariki, utapata ushindi na mafanikio kwenye maisha.

Lakini huwa ni vigumu sana watu kutoa baraka zao kwa urahisi. Na hata pale wanapotoa baraka hizo, zinaweza zisiwe za milele, kwani wanaweza kubadili baraka kuwa laana kama utashindwa kutimiza matakwa yao mengine.

Rafiki, mara zote mimi huwa nakupa wewe njia za uhakika za kupata ushindi na mafanikio na zisizomtegemea mtu mwingine yeyote ila wewe mwenyewe. Na kwenye hili la laana na baraka, nataka pia uweze kulitumia wewe mwenyewe bila kumtegemea mtu yeyote. Na hata kwa wale wanaotumia laana na baraka kama njia ya kukufanya uwategemee wao na kutokuwa huru, tunakwenda kuvunja hilo leo.

Jipe Laana Ya Ushindi.

“Mara zote huwa nashinda, nimelaaniwa kushinda” ni nukuu ya Silvio Berlusconi, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Italy kwa vipindi vitatu na mfanyabiashara mkubwa. Silvio alikuwa na imani kali juu ya ushindi wake mwenyewe na ilimwezesha kupata mafanikio makubwa kwenye mambo mengi aliyojihusisha nayo.

Kupitia nukuu hii anatupa somo na uhuru mkubwa sana, kwamba mtu unaweza kulaaniwa kushinda. Kama ambavyo watu wanaamini wamelaaniwa kushindwa na hilo linawapelekea kushindwa kweli, ukiamini umelaaniwa kushinda, utashinda kweli.

Kwa kuwa ni vigumu kupata mtu ambaye atakupa laana ya ushindi, unapaswa kujipa wewe mwenyewe hiyo laana. Unajipa laana ya ushindi kwa kuamini, bila shaka yoyote kwamba unakwenda kushinda. Unafuta kabisa wasiwasi wowote unaokuwa nao juu ya ushindi wako. Na hata kama mambo yataonekana magumu kiasi gani, bado unaendelea kuamini kwenye ushindi wako.

Imani hiyo kali inapoanzia ndani yako, na unapokataa kabisa kuyumbishwa kwenye imani hiyo, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kupata ushindi na mafanikio makubwa unayoyataka.

Ili kujipa na kuimarisha laana yako ya ushindi, fanya haya yafuatayo;

1. Anza Na Ushindi Kwenye Fikra Zako.

Laana au baraka ni kitu kinachoanzia kwenye fikra zetu kabla ya kutokea kwenye uhalisia. ‘Unakuwa kile unachofikiri kwa muda mrefu,’ ni maandiko yenye nguvu na yanayoonyesha uhalisia.

Ikiwa unafikiria kushindwa mara zote, hicho ndiyo kitakachotokea, hata kama umezungukwa na mazingira ya ushindi. Fikra zako ndiyo zinazovuta kile kinachotokea kwenye maisha yako.

Ili kujipa na kuimarisha laana yako ya ushindi, hakikisha mara zote unakuwa na fikra za ushindi. Jione ukishinda, fikiria kupata matokeo mazuri unayoyataka, hata kama unachopata ni tofauti kabisa na unachotaka.

Kamwe usiruhusu fikra zozote hasi kukaa kwenye akili yako hata kwa dakika chache. Kila zinapokuja ziondoe kwa kuhamia kwenye fikra chanya. Tumia kila kitu kizuri ulichonacho kama ushahidi wa ushindi kwako.

Hata kama unapitia mambo magumu, tumia mazuri uliyonayo kama tumaini la kupata ushindi. Na usije ukafikiria huna mazuri yanayoendelea, kuwa hai na mwenye afya njema ni moja ya ushindi mkubwa ambao tayari unao.

Laana kubwa ya ushindi unayoweza kujipa, ambayo pia ni baraka ya ushindi ni kufikiria ushindi mara zote. Hata kama huoni kabisa njia ya kupata ushindi unaotaka, wewe amini na fikiria kuhusu ushindi huo kwanza.

Fikra unazokuwa nazo juu ya ushindi zitafungua njia nyingi za ushindi kwako. Usisubiri uone njia ndiyo ufikirie ushindi. Anza kufikiria ushindi ili fikra hizo zikuonyeshe njia nyingi za ushindi zinazokuzunguka.

2. Futa Kabisa Hofu Na Wasiwasi.

Kuwa na fikra za ushindi ni rahisi na wengi huwa wanapata fikra hizo. Lakini bado wengi hawapati ushindi kwa sababu wanaruhusu sumu ya kifikra kuzuia wao kupata ushindi. Sumu hiyo ni hofu na wasiwasi ambao mtu unakuwa nao.

Hofu ni kinyume cha imani, ni kutengeneza ushahidi mbaya ambao haupo. Hofu ni imani ya kushindwa, ambako bado hakujatokea. Hofu ni matumizi mabaya ya fikra na taswira unazojipa. Ni kuona kushindwa kabla hata hakujatokea. Unapohofia kitu, unakipa nguvu kubwa ya kutokea.

Wasiwasi ni kuwa na imani dhaifu juu ya ushindi wako. Unakuwa na fikra za ushindi, lakini unaona kuna vitu vinavyokuzuia kupata ushindi huo. Unapoamini kwenye vitu kukuzuia, unapunguza nguvu ya imani yako na kujizuia kupata ushindi.

Una wajibu wa kufuta kabisa hofu na wasiwasi kuhusu ushindi na mafanikio. Unapokuwa na fikra za ushindi, hakikisha hicho ndiyo kitu pekee unachofikiria na kuamini. Hata kama utaona kabisa ushahidi wa kushindwa, usiupe kabisa nafasi kwenye fikra zako.

Mara zote fikiria na ona upande wa ushindi. Jipe ushahidi wa ushindi, ambao umekuzunguka. Chukua hatua za ushindi, hata pale matokeo unayoyapata siyo uliyotegemea kupata.

Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha kwa ukamilifu mambo matano ya kufanya ili ujipe laana ya ushindi itakayokupa mafamikio makubwa unayoyataka. Ni lazima utambue kwamba mafanikio makubwa unayoyataka hayataweza kuja kwa kuendelea kuwa kawaida.

Soma barua hiyo hapa ili uchukue hatua sahihi; #BZK031; Jipe Hii Laana Ya Ushindi Ili Ufanikiwe Kwa Uhakika.

Geuza nguvu ya laana mbaya kuwa nguvu ya laana nzuri itakayokupa mafanikio makubwa unayoyataka. Usikubali kuelewa kitu kingine chochote isipokuwa mafanikio makubwa unayoyataka. Kadiri akili yako inavyotawaliwa na kitu kimoja tu, ushindi, ndivyo unavyoupata kwa uhakika.

Najua mafanikio makubwa unayoyataka yanawezekana kabisa kwako. Lakini hayatakuja kirahisi kama unavyodhani. Ndiyo maana unajifunza mambo makali na yasiyo ya kawaida, yatakayokuwezesha kutoka ulipokwama sasa. Chukua hatua stahiki ili upate matokeo tofauti.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.