Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Bado haina upinzani kwamba mafanikio makubwa yanatokana na mtu kupenda sana kile anachofanya. Mtu anaweza kupata matokeo kwenye chochote anachofanya, kama atakuwa na maarifa sahihi na kuweka juhudi kubwa.
Lakini inapokuja kwenye mafanikio makubwa sana, yale ambayo hayajawahi kuonekana na walio wengi, ni lazima mtu awe anapenda sana kile anachofanya.
Hapa natumia neno kupenda, kwa sababu ndiyo neno rahisi kueleweka kwa Kiswahili. Lakini neno sahihi linapaswa kuwa ni KUHUSUDU (Passion) na KUZIMIA (Obsession) kile unachofanya.
Nasisitiza sana hii maana, kwa sababu wengi bado hawapati uzito wa hili kwenye kujenga mafanikio makubwa, ambayo hayajawahi kuonekana.
Hiyo safari ni ngumu, ndefu na iliyojaa kila aina ya vikwazo. Kuna kutokukubalika na wengi, halafu kuna kushindwa kwenye yale unayofanya. Na wakati huo, kuna mambo mengine yanayoonekana ni rahisi zaidi kufanya na wengine wanapata matokeo mazuri.
Kama hujahusudu na kuzimia kile unachofanya, hutaweza kumudu hayo yatakayokukabili. Na hivyo ndivyo safari ya mafanikio ya wengi ilivyoshindwa. Siyo kwa sababu hawana uwezo wa kufanikiwa, bali kwa sababu hawana kiwango sahihi cha mapenzi kwenye kile wanachofanya.
Kuna watu wachache sana ambao kitu wanachopenda kufanya ndiyo pia kinachoendana na mafanikio makubwa wanayoyajenga. Hao wachache wenye bahati, bado nao huwa wanashindwa kuitumia vizuri.
Kwa walio wengi, kile tunachopenda kufanyanya siyo kinachoweza kutupa mafanikio tunayotaka. Hivyo tuna wajibu wa kuhakikisha tunatengeneza mapenzi kwenye kile kitakachoweza kutupa mafanikio makubwa.
Hili ni jukumu ambalo watu wengi hawajui jinsi ya kulifanya. Kwenye barua kadhaa nimeshalieleza hili, jinsi unavyopaswa kupenda chochote unachochagua kufanya ili ujenge mafanikio makubwa.

Barua hii inaenda kuzama kwa kina zaidi, kutusaidia kujenga mapenzi hayo makubwa kwenye kile tulichochagua kufanya ili mafanikio makubwa yawe uhakika kwetu.
Jifunze mambo haya na uyafanyie kazi ili uweze kujenga na kudumu kwenye mafanikio makubwa yaliyo ndani ya uwezo wako.
1. Upendo Hukua Pale Nishati Inapoenda.
Ukiangalia watu wote ambao upo nao kwenye mahusiano ya kila aina leo, mwanzo hamkuwa mnajuana wala kupendana. Inaweza kuwa mwenza, marafiki, washirika wa kikazi na kibiashara.
Mlipokutana kwa mara ya kwana, hakukuwa na kitu kinachowaleta pamoja. Lakini baada ya kukaa karibu kwa muda mrefu na kujuana, mliona kuna vitu mnaendana na hilo kufanya muwe na mahusiano.
Unaona hapo, hamkuwa mnapendana mlipokutana, lakini baada ya kuwa karibu kwa muda, upendo umejengeka ndani yenu. Hiyo ni kwa sababu upendo huwa unakua pale nishati inapoenda.
Kwa kile kitakachokupa mafanikio, usiumie pale ambapo mwanzoni unakuwa hukipendi. Wewe endelea kukifanya, endelea kuwa nacho karibu na endelea kukifikiria bila kukoma. Kadiri muda unavyokwenda, utaona upendo ukijengeka kidogo kidogo.
Wajibu wako ni kupeleka nishati kwenye kile kitakachokupa mafanikio na hiyo itajenga upendo wa kukifanya kwa ukubwa ili ufanikiwe. Mapenzi kwenye kitu unachofanya yanatokana na ukaribu na muda ambao mtu umeweka kwenye kitu hicho. Hilo lipo ndani ya uwezo wako, hivyo lifanye kikamilifu.
2. Huhitaji Motisha Kuanza, Bali Msimamo Ili Kuendelea.
Sihitaji sana kukueleza hili, kwa sababu najua unao ushahidi halisi kabisa. Kuna mambo mengi ambayo umeyaanza kwa motisha mkubwa mwanzoni, lakini hukufika nayo mbali.
Hiyo ni kwa sababu ulidhani unachohotaji ni hamasa tu ndiyo uweze kupata matokeo makubwa. Hamasa ni kitu cha muda mfupi sana, huku mafanikio yakitaka mbio za muda mrefu.
Kinachohitajika kwenye mafanikio ni kuweza kufanya kitu kwa msimamo kwa muda mrefu bila kuacha. Unapofanya kitu kwa muda mrefu, ndiyo unazidi kukielewa, kukizoea na hata kukipenda.
Watu wengi wamekuwa wanakata tamaa na kuishia njiani kabla hawajatengeneza mapenzi ya kutosha kwenye kitu. Wewe usiwe kama hao wengi, hakikisha unaendelea kufanya kwa muda mrefu kile unachojua kitakufikisha kwenye mafanikio makubwa.
3. Anza Na Uaminifu, Siyo Tamaa.
Mahusiano ya aina yoyote ile, huwa yanajengwa kwa msingi wa uaminifu au tamaa. Uaminifu ni pale mahusiano yanapotokana na kitu chenye manufaa kwa pande zote. Tamaa ni pale mahusiano yanapojengwa kwa kitu chenye manufaa kwa upande mmoja, hasa ule ambao unatamani.
Watu wengi wanajenga mahusiano yasiyo sahihi na kile wanachofanya, kwa sababu wanasukumwa na tamaa na siyo uaminifu. Wanachoangalia ni wao watapata nini, hivyo wanapochelewa kupata wanaacha na kwenda kwenye kitu kingine.
Uaminifu kwenye kile unachofanya ni pale unapoangalia na wewe unatoa nini. Ni pale unapoona una mchango wa kutoa kwa wengine kupitia hicho unachofanya. Kwa kuona mchango huo, unapata sababu ya kuendelea kufanya, hata kama hupati kile ulichotaka haraka.
Ukitaka kujenga mapenzi ya dhati na kile kitakachokupa mafanikio makubwa, usijiangalie tu wewe unapata nini, angalia pia wengine wananufaikaje kupitia wewe kufanya kitu hicho. Na pale unaposhawishika kuacha, angalia jinsi ambavyo watu hao wataathirika.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimeshirikisha mambo 10 ya kuzingatia ili uweze kujenga mapenzi ya dhati kwenye vitu sahihi vitakavyokupa mafanikio. Huhitaji tena kupoteza muda na mambo yasiyokupa matokeo.
Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK030; Hii Ni Njia Ya Uhakika Ya Kupenda Chochote Ili Kujenga Mafanikio Makubwa.
Mapenzi ya dhati hayakwepeki kwenye mafanikio makubwa. Ulichojifunza hapa na utakachojifunza kwa kina zaidi kwenye Barua kaweke kwenye matendo ili upige hatua kubwa kadiri unavyotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.