Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Najua kabisa kwamba unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Hongera sana kwa matamanio hayo makubwa, ni mazuri na unaweza kabisa kuyafikia.

Ili upate mafanikio hayo, ni lazima uweke malengo na kuyafanyia kazi ili kuyatimiza. Kwa kuwa mafanikio unayotaka ni makubwa, na malengo pia yanapaswa kuwa makubwa.

Na hapo ndipo watu wengi huwa wanakwama, wanaweka malengo makubwa, lakini wanashindwa kuyafanyia kazi. Hiyo ni kwa sababu malengo yanakuwa makubwa sana kiasi cha kushindwa kujua wapi pa kuanza kuyafanyia kazi.

Huwa kuna kitendawili kinachoelezea vizuri hali hii, ambacho kinauliza unawezaje kumla tembo? Jibu likiwa ni kumkata vipande vidogo vidogo na kumla kwa vipande hivyo.

Kitendawili hicho kinaonyesha nguvu ya kugawa malengo makubwa kwenye hatua ndogo ndogo ambazo mtu unaweza kuzifanyia kazi. Pamoja na hilo kuwa linaloeleweka, bado wengi huwa hawalifanyi. Wanabaki na malengo yao makubwa, wakiamini kuna namna wanaweza kuyafanyia kazi na kupata matokeo makubwa kwa haraka.

Watu wengi wanashindwa kuyagawa malengo yao makubwa kwenye hatua ndogo ndogo kwa sababu hawajui ni nguvu gani inayofanya kazi kwenye hilo.

Kanuni Ya Mwendo Ya Newton.

Mwanasayansi Isaac Newton aligundua kanuni tatu za mwendo, ambapo ya kwanza ilihusisha hali ya kitu. Kanuni hiyo inasema; ‘Kitu huwa kinabaki kwenye hali ambayo kipo, kilichosimama kinaendelea kusimama na kilicho kwenye mwendo kinaendelea na mwendo mpaka nguvu ya nje itakapobadili hali hiyo.’

Kwa kanuni hii ya mwendo, tunaiona nguvu ya kugawa malengo makubwa kwenye hatua ndogo ndogo ili kuweza kuyafikia kwa uhakika.

Pale lengo linapokuwa kubwa, tunakuwa hatuna pa kuanzia, hivyo tunabaki kwenye hali ya kusimama. Ni mpaka tunapogawa lengo kubwa kwenye malengo madogo madogo, ambayo tunaweza kuyafanyia kazi ndiyo tunaweza kwenda kwenye hali ya kufanya bila kuacha.

Kama hatua za kuchukua ni ndogo sana na zilizo ndani ya uwezo wako, utaweza kuendelea kuzichukua kwa msimamo bila kuacha. Kuchukua hatua hizo kwa mwendelezo na msimamo bila kuacha ndiko kunakupa uhakika wa kutimiza malengo yoyote makubwa unayokuwa nayo.

Kemikali Ya Raha Kwenye Akili.

Kama ambavyo tumeshajifunza kwenye barua za nyuma, akili zetu huwa zinapenda raha. Na kemikali ya dopamini ndiyo huwa inaachiliwa kwenye akili na kuleta hali ya raha.

Kemikali hiyo huachiliwa pale mtu unapokuwa umekamilisha jukumu fulani. Hivyo unapokuwa na malengo madogo madogo unayofanyia kazi, kila unapotimiza, kemikali hiyo inaachiliwa na unajisikia vizuri.

Akili huwa inavunja kemikali hiyo haraka, hivyo raha unayopata haidumu. Unalazimika kufanya tena ulichofanya ndiyo upate tena raha. Na hapo ndipo unaposukumwa kuendelea kuchukua hatua kwenye malengo yako ili kuendelea kupata raha.

Kuyagawa malengo makubwa kwenye hatua ndogo ndogo ni njia ya kujenga uraibu chanya badala ya akili kuingia kwenye uraibu hasi kama wa mitandao ya kijamii.

Kinachofanya mitandao ya kijamii iwe na uraibu mkubwa ni uharaka wake wa kutoa raha. Unapoingia kwenye mitandao ya kijamii, inakuchukua muda na juhudi kidogo sana kuanza kupata raha. Kupitia vitu vya wengine unavyoona na vitu vyako unavyoshirikisha na wengine wakavipenda, unajisikia raha sana.

Tukiweza kuhamisha chanzo chetu cha raha kikawa kutekeleza malengo yetu, tunakuwa tumekamilisha mambo mawili kwa wakati mmoja. Tunakuwa tumeyafanyia kazi malengo na pia tunakuwa tumepunguza upotevu wa muda.

Ili kuweza kuyagawa malengo yoyote makubwa kwenye hatua ndogo ndogo na kufanyia kazi kwa uhakika, hapa kuna mambo matano ya msingi ya kufanyia kazi.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha kwa kina mambo hayo na jinsi unavyoweza kuyafanyia kazi kwenye malengo yako mwenyewe na malengo unayofanya na timu yako.

Soma barua hiyo na ujifunze mambo hayo na kuyafanyia kazi ili usikwame kutekeleza malengo makubwa uliyonayo na kufikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Soma barua hapa; #BZK044; ‘Dogosha’ Malengo Yako Uyafikie Kwa Uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.