Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Mahusiano yetu na watu wengine huwa yanapitia changamoto mbalimbali zinazosababishwa na watu kukosa msimamo. Kile ambacho watu wanasema na wanachofanya mara nyingi huwa vinatofautiana.

Kwa bahati mbaya sana, sisi huwa tunachagua kuamini kile tunachotaka kuamini kuhusu watu na siyo uhalisia ambao watu wanatuonyesha. Na mara nyingi sana, tumekuwa tunaamini kile ambacho watu wanatuambia, hata kama wanachofanya ni tofauti kabisa.

Kwa sababu tunakuwa tunataka sana kile ambacho watu wanatuambia kiwe kweli, tunashindwa kuona ukweli halisi ambao wanatuonyesha kwa matendo yao. Ni mpaka kwenye nyakati ambazo hatutegemei, ndiyo zile tabia ambazo watu wametuonyesha zinakuja kutuumiza.

Maneno Na Matendo Yakitofautiana, Amini Matendo.

Huwa kuna kauli kwamba tusikilize maneno ya watu na siyo kuangalia matendo yao. Hiyo ni moja ya kauli zilizowapotosha watu wengi, kwani matendo yana nguvu kuliko kauli.

Kauli ni rahisi na kila mtu anaweza kusema, hata kama anachosema hamaanishi kabisa. Wengi wanasema mambo mengi, lakini inapokuja kwenye utekelezaji, mengi huwa hayatekelezeki.

Matendo ni magumu na ndiyo yanayoamua mtu atafanya nini kwenye nyakati fulani. Wengi huwa wanarudi kwenye mambo waliyozoea kufanya, hata kama walichoahidi ni tofauti.

Wewe umekuwa unaingia kwenye changamoto na watu, kwa sababu unawabishia wanapokuonyesha ukweli kuhusu wao. Wewe unakuwa unatamani sana kile wanachokuambia na kukuahidi kiwe kweli, kwa sababu ndiyo kitakupa unachotaka.

Lakini vitu haviwi kweli kwa sababu tunatamani hivyo, vinakuwa kweli kwa sababu ya mazoea yaliyopo.

Kunapokuwa na tofauti kati ya maneno na matendo, amini matendo na siyo maneno. Kama mtu anasema au kuahidi A, lakini anatekeleza B, wewe amini B. Haijalishi anasisitiza kiasi gani kile anachosema, ukweli wake uko kwenye kile anachofanya.

Huwa kuna kauli inasema; ‘Vitendo vyako vinapiga kelele sana, sisikii unachosema.’ Ni kauli inayoonyesha nguvu ya matendo kuliko maneno.

Kila tunapolalamika kwamba watu wametudanganya, tatizo siyo wao kutudanganya, bali tatizo ni sisi kuwabishia kwenye yale wanayotuonyesha. Watu wanaweza kusema mengi, kwa sababu maneno ni rahisi. Lakini matendo yao ndiyo yanayosema ukweli zaidi, na huwa yanajidhihirisha mara zote.

Watu wanaweza kufanganya sana kwa maneno, lakini matendo huwa yanaweka wazi kila kitu kuhusu wao. Ni vigumu mno kwa mtu kudanganya kwa matendo, hasa kwa muda mrefu.

Kwenye barua hii tunakwenda kuangalia matendo ya watu ambayo yanatuonyesha wazi ukweli wao kupitia vitu wanavyothamini. Tukiweza kuangalia vitu hivyo na kupuuza yale wanayosema, tutapunguza sana kuangushwa na kukwamishwa na wengine. Hiyo ni kwa sababu tutakuwa na matarajio sahihi kuhusu watu na siyo kujidanganya kwa maneno wanayotuambia.

1. Watu Wanakuonyesha Wanavyothamini Muda Kwa Kuchelewa.

Moja ya nukuu kali sana kuhusu muda niliyowahi kukutana nayo ni ya George Horace Lorimer kwenye kitabu: Letters from a Self-Made Merchant to His Son. Aliandika; “Mara zote tenga muda ambao utakutana na mtu, na kama atachelewa hata kwa dakika, usijisumbue naye. Mtu anayeweza kuchelewa wakati maslahi yake yako hatarini, ni uhakika atachelewa wakati maslahi yako yapo hatarini pia.”

Ukiitafakari kwa kina nukuu hiyo, unaona wazi kwamba mtu anapochelewa kwenye jambo lolote lile, anakuonyesha ukweli wa jinsi anavyothamini muda. Mtu anapochelewa kwenye kitu chochote kile, maana yake hathamini muda au pia hathamini kitu hicho.

Nikuulize, ni mara ngapi umevumilia watu wanaochelewa kwenye mambo mbalimbali na hilo limekuwa linakukwamisha? Umekuwa unadhani wamechelewa kwa sababu ya foleni, au kwa sababu ya changamoto mbalimbali wanazoeleza. Lakini ukweli uko dhahiri, watu wanachelewa kwa sababu hawajali.

Inapokuwa jambo ni muhimu sana, jambo la maisha na kifo, kila mtu anao uwezo wa kuwahi. Foleni zitaendelea kuwepo, changamoto zitakuwepo, lakini kuchelewa inapokuwa na gharama kubwa, watu huwa wanawahi.

Kuwa makini sana na watu wanaochelewa kwenye muda ambao mnakubaliana. Wanaweza kukupa sababu zinazoshawishi, lakini kuna ujumbe wanakutumia na wewe hutaki kuuelewa. Kuna kitu siyo muhimu kwao, muda au hicho mlichokubaliana kufanya.

Jua kwa haraka sana ukweli wa watu wanaochelewa ili msiendelee kupotezeana muda. Kwa sababu huwezi kujenga mafanikio makubwa na watu ambao muda kwao hauna thamani kabisa.

Wewe unajua jinsi muda ulivyo na thamani kubwa, kwa sababu kila dakika inayopita huwezi kuipata tena. Linda sana muda wako na jihusishe na watu wanaothamini na kulinda muda.

Rafiki, ulichojifunza hapa ni eneo moja la kujua ukweli wa watu kwa tabia zao badala ya kusikiliza maneno yao.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekuonyesha maeneo mengine manne ya kuangalia tabia za watu. Maeneo hayo yanahusu fedha, umakini, kazi na afya. Hayo ni maeneo muhimu sana ambayo ukidanganywa, unakwama.

Kwa mfano kwenye fedha, ni mara ngapi watu wamekuomba uwakopeshe fedha lakini wakati wa kukulipa wakakusumbua? Wakati wanakopa wanakuambia maneno mazuri, lakini kulipwa inakuwa utata. Nimekuonyesha jinsi ya kujua tabia halisi za watu kwenye fedha ili usiingie kwenye changamoto hizo.

Soma barua hapa; #BZK045; Tatizo Unawabishia Watu Wanapokuonyesha Ukweli Kuhusu Wao.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.