Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tunazaliwa tukiwa tunajua vitu viwili tu kwa uhakika, kunyonya na kulia. Na hata mkunga anayezalisha, hivyo ndiyo vitu vya kwanza kabisa anavyopima kwa mtoto. Ndiyo maana mtoto anapozaliwa huwa anaguswa mgongoni ili aweze kulia, maana hilo ndiyo litamweka hai. Baada ya kulia anawekwa kwenye ziwa la mama au kusogezewa kidole mdomoni kuona kama anaweza kunyonya.
Mtoto mchanga anayeweza hayo mawili kwa uhakika, amekamilika kwa ajili ya maisha. Anayeshindwa hayo inabidi apatiwe msaada kwanza. Baada ya hayo mawili, mengine yote tuliyonayo sasa kwenye maisha, tumejifunza hapa duniani.
Nimeanza na mfano huo halisi kabisa kwetu, kwa sababu tunachokwenda kujifunza kwenye barua hii kinaenda kinyume na kile ulichofundishwa na kuaminishwa kwa maisha yako yote.
Baada ya mtoto kuzaliwa, anaanza hatua za ukuaji. Atajifunza kukaa, kisha kutambaa, kutembea na mengine. Kwenye kila hatua anayopiga, huwa haiwi rahisi kwa mara ya kwanza. Mtoto hasimami mara moja na akawa ameweza, bali atasimama na kuanguka, atasimama tena na kuanguka. Atarudia hivyo kwa muda mrefu mpaka pale anaposimama bila kuanguka.
Kadhalika kwenye kutembea, kuongea, kuandika na mengine. Yanachukua muda kwa mtoto kuweza kuyafanya kwa usahihi. Je tumewahi kusema mtoto ameshindwa kwenye hizo harakati zake za kujifunza vitu vya msingi kwenye maisha? Je mtoto anajali pale anapotaka kusimama lakini anaanguka?
Kabla hatutajibu hayo, twende miaka 30 baadaye, kwa mtoto yule yule ambaye alianguka mara nyingi alipojaribu kusimama, lakini hakuacha, aliendelea mpaka akaweza. Sasa amekuwa mtu mzima na kupata wazo la kuanzisha biashara. Anaanzisha biashara yake, lakini hapati wateja, anapata hasara na biashara inakufa. Mtu mzima huyu anachukuliaje hali hiyo?
Katika makundi hayo mawili, utaona tofauti kubwa sana, ambayo maisha yameitengeneza hapo katikati. Mtoto mdogo alijifunza kila kitu kwa kuanguka, lakini hakukata tamaa, aliendelea mpaka akaweza. Mtu mzima anapoanguka kidogo, kwenye jambo ambalo hakuwa anajua, anakata tamaa na kusema ameshindwa na hawezi.
Sijui unaona hapo jinsi ambavyo kitu kimoja kimekuwa na tafsiri mbili tofauti na zenye madhara kwa watu? Mtu akimwangalia mtoto anayejifunza kutembea, kila anapoanguka anamtia moyo ajaribu tena. Hakuna mtu anamcheka mtoto mdogo kwa sababu hawezi kutembea vizuri au hawezi kuongea vizuri.
Lakini inapokuja kwa mtu mzima, ambaye anaanza kufanya kitu ambacho hajawahi kufanya, akianguka anachekwa na kubezwa. Anaambiwa yeye hawezi kitu hicho na aachane nacho. Na hivyo ndivyo safari ya mafanikio ya wengi imeshindikana. Siyo kwa sababu hawawezi au wameshindwa, bali kwa sababu ya tafsiri mbaya waliyofundishwa kwenye jamii.

Kwenye barua hizi, kazi yangu ni kunyoosha mambo yote kwako, ili usikwamishwe na kitu chochote kwenye safari yako ya kujenga mafanikio makubwa, utajiri na biashara inayojiendesha bila kukutegemea moja kwa moja.
Hapa tunaangalia vizuri hili swala linaloitwa kushindwa, ambalo kiuhalisia halipo kabisa. Tunaenda kumalizana nalo leo ili lisiwe tena kikwazo kwetu.
1. Hakuna Kushindwa.
Kama tulivyoona mfano wetu binadamu, tangu tulipokuwa watoto, ni dhahiri kwamba hakuna kushindwa. Ingekuwa kuna kushindwa, leo hii wote tusingekuwa tunaweza kutembea, kuongea au kufanya yote tunayoyafanya.
Lakini tumeaminishwa kwamba kuna kushindwa, na sisi tumeamini hilo, kitu ambacho kimetukwamisha kabisa kwenye kujenga mafanikio makubwa tunayoyataka.
Imani ya kwanza tunayopaswa kuijenga na kuiimarisha ni kwamba hakuna kushindwa. Na hatujiambii hivi kujifariji, bali ndiyo uhalisia, ndivyo asili ilivyo.
Chochote tunachochukulia kama kushindwa ni kwa sababu tumeaminishwa hivyo. Yale yote yaliyo ndani ya asili yetu kufanya, tunaweza kuyafanya. Huwezi kuruka angani kama ndege, kwa sababu siyo asili yako. Na kushindwa kuruka kama ndege hakujawahi kuhesabiwa ni kushindwa.
Lakini kutokupata matokeo ambayo mtu anataka, hasa baada ya kufanya anachopaswa kufanya kunahesabiwa ni kushindwa. Wewe unaona hiyo imekaa sawa kweli? Ingekuwa kuna kushindwa, usingeweza hata kufanya. Lakini kama umeweza hata kujaribu, hujashindwa, umejifunza ambacho hakifanyi kazi na hivyo unapaswa kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.
Futa kabisa kushindwa kwenye fikra zako, ni kitu ambacho hakipo kabisa kwenye asili wala uhalisia. Kushindwa ni fikra ulizopandikiziwa na wale wasiokuwa na nia njema na mafanikio yako makubwa.
2. Wanaokuambia Umeshindwa Wanataka Kukutawala.
Ukiwachunguza watu wote wanaokazana kukuambia umeshindwa, utashindwa au huwezi, utaona wana sifa kuu mbili; moja ni hawajafanikiwa kwa viwango ambavyo wewe unataka kufika, hivyo hawajui na kutokujua kwao wanaona haiwezekani hivyo ukijaribu utashindwa.
Mbili ni wale ambao hawataki wewe upige hatua za mafanikio kwa sababu wanataka waendelee kukutawala. Wanajua ukifanikiwa utakuwa huru na kutoka chini ya utawala wao. Hivyo wanatumia njia ya kukujaza fikra za kushindwa ili uendelee kuwasikiliza wao na wakutumie.
Kuondokana na hayo yote, wewe futa kabisa fikra za kushindwa kwenye akili yako. Jitangazie wazi kwamba hakuna kushindwa. Ondoa kabisa kila aina ya fikra za kushindwa ndani yako.
Na wote wanaokuambia umeshindwa, utashindwa au huwezi, wapuuze haraka sana. Usiwape muda wa kuendelea kukupa maelezo kwa nini utashindwa, unajua hicho kitu hakipo, hivyo hutaki maelezo ya kitu ambacho hukitambui.
Njia ya uhakika ya kutokusumbuliwa na kitu ni kutotambua uwepo wa kitu hicho. Kataa kutambua uwepo wa kushindwa ili kusiwe na kikwazo chochote kwako kupata mafanikio unayoyataka.
Rafiki, umeona jinsi ambavyo ulikuwa mjanja ulipokuwa mtoto kwa kutowasikiliza watu, ila sasa umekuwa mtu mzima, unasikiliza sana watu mpaka unakubali kushindwa.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekueleza mambo matano ya kufanyia kazi ili ufute kabisa dhana ya kushindwa kwenye maisha. Ukishaweza kufuta dhana hiyo, kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako, hakuna tena kitakachoweza kukukwamisha.
Soma barua hiyo hapa; #BZK043; Hakuna Kushindwa, Futa Kabisa Hilo Neno Kwenye Maisha Yako.
Rudi kwenye akili zako za utoto, wapuuze wote wanaokuambia umeshindwa au huwezi na endelea kufanya chochote ulichochagua. Hiyo ndiyo njia ya uhakika ya kujenga mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.