Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Hivi karibuni nimekutana na mjadala mmoja mkali sana mtandaoni, ambao ulinifanya nitafakari sana namna tumekuwa tunachukulia fedha na utajiri.
Aliyeibua mjadala huo alianza na swali; ‘Nini kinasababisha umasikini?’ Kisha akajibu; ‘Hakuna. Umasikini ni hali ya awali, sehemu ya kuanzia.’ Akamalizia kwa kusema; ‘Swali sahihi ni nini kinasababisha utajiri?’
Mjadala huo ulinikumbusha mjadala mwingine mkali sana uliowahi kuibuka kipindi cha nyuma, ambapo kiongozi wa nchi, akiwa ziarani kwenye nchi za nje, aliulizwa swali na majibu yake yakaibua mjadala huo mkali.
Kiongozi aliulizwa kwa nini wananchi wako ni masikini, ili hali nchi ina rasilimali nyingi za kuiwezesha kuwa na utajiri mkubwa? Kiongozi akajibu, hata mimi nashangaa, sijui kwa nini bado tumebaki kuwa masikini.
Majibu hayo yalitushangaza wengi, na mimi nikiwa mmoja wao. Tuliona kama kiongozi wetu hajui kwa nini taifa ni masikini, tuna matumaini yoyote ya kutoka kwenye umasikini huo? Mengi sana yalisemwa juu ya majibu hayo.
Kwa mijadala hiyo miwili, nimetafakari na kuona wote wako sahihi. Kiongozi aliyesema hajui kwa nini wananchi wake ni masikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi alikuwa sahihi. Na hiyo ni kwa sababu hakuna kinachosababisha umasikini, hiyo ni hali ambayo watu wanaanzia.
Na kama ambavyo mjadala wa karibuni umeeleza, swali sahihi siyo nini kinasababisha umasikini, bali nini kinasababisha utajiri? Hilo ndiyo swali tunalopaswa kulipatia majibu ili tuweze kujenga utajiri mkubwa na kuwa na uhuru kamili wa maisha yetu.

Kwenye barua hii tunaenda kujadili kwa kina na kuondoka na hatua za kwenda kuchukua ili kuimarisha mikakati yetu ya kujijengea utajiri, bila kukwamishwa na umasikini ambao wengi tunaanza nao.
1. Umasikini Ni Kitu Ambacho Hakipo.
Asili huwa ina upacha wa vitu, yaani kila kitu kina pande mbili. Upande wa kwanza ni uwepo wa kitu na upande wa pili ni kutokuwepo kwa kitu hicho.
Chukua mfano wa mwanga na giza, giza ni kutokuwepo kwa mwanga. Hivyo tuna pande mbili, mwanga na giza, lakini giza ni kitu ambacho hakipo. Unaweza kupima mwanga, lakini huwezi kupima giza. Kwa sababu giza ni kitu ambacho hakipo.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye utajiri na umasikini, umasikini ni kutokuwepo kwa utajiri. Unaweza kupima utajiri, lakini huwezi kupima umasikini. Hata viwango vya umasikini vinavyotumika, bado inapimwa kwa kukosekana kwa utajiri.
Huu ni msingi wa kwanza kabisa kwenye kuondokana na umasikini, kwa kujua ukweli huu kwamba umasikini ni kitu ambacho hakipo. Na kitu ambacho hakipo, ambacho mtu huwezi hata kukipima, huwezi kujua nini kinachosababisha.
Wajibu wetu ni kuhangaika na kile kilichopo, ambacho tunaweza kukiathiri na kuleta mabadiliko. Kwa mfano, ukiingia kwenye chumba chenye giza, hata uhangaike kiasi gani, huwezi kubadili hali hiyo ya giza. Ni mpaka utakapowasha mwanga ndiyo giza litapotea lenyewe.
Tukihangaike na kile kilichopo, ambacho kinaweza kupimika, tunaweza kuondokana na kile kisichokuwepo ambacho kimekuwa kinatukwamisha.
2. Utajiri Ni Kitu Ambacho Kinatengenezwa.
Kama hakuna kitu kinachosababisha umasikini, kwa sababu ni hali ya awali, na utajiri ndiyo unaoondoa umasikini, ni dhahiri kwamba utajiri ni kitu ambacho kinatengenezwa.
Hii ndiyo inajibu swali la kiongozi aliyeulizwa kwa nini nchi yake ni masikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi. Kwa sababu umasikini ni hali ya kuanzia, na inaondolewa na utajiri, ambao ni lazima utengenezwe.
Ardhi inaweza kuwa na madini na mafuta, lakini hayawezi kutoka yenyewe huko ardhini na kuleta utajiri. Ni lazima utajiri utengenezwe, kwa kutumia kila kinachopatikana.
Hakuna utajiri unaotokea tu, hata kwa wanaorithi utajiri, kuna watu waliutengeneza. Na hao wanaourithi wataweza kuutunza kama wanajua jinsi ya kuutengeneza.
Ukiangalia mataifa yote ambayo kwa sasa yana utajiri mkubwa, yalianzia kwenye hali ya umasikini, yakiwa hayana utajiri kabisa. Ni kupitia mikakati mikubwa ya kujenga utajiri ndiyo mataifa hayo yameweza kubadilika.
Ukiangalia watu wengi ambao wameweza kujenga utajiri mkubwa, walianzia kwenye umasikini. Ni kupitia kujenga utajiri ndiyo wameweza kuondokana na umasikini huo. Hata wanaorithi utajiri, kuna kizazi kilichotangulia ambacho kilijenga utajiri huo.
Kuna namna watu wengi wamepumbazwa kwamba utajiri unaweza kutokea tu, labda kwa maombi au utegemezi kwa watu fulani. Lakini ukweli mchungu ni utajiri lazima utengenezwe. Na inapokuja kwa mtu binafsi, ni lazima ujue jinsi ya kujenga na kutunza utajiri.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza mambo 7, ambapo hapa umeyapata mawili. Kupata mambo matano yaliyosalia, ambayo ni ya muhimu sana, karibu usome barua ya kocha.
Isome hapa; #BZK042; Hakuna Kinachosababisha Umasikini.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.