Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kitu kimoja ninachokipenda kuhusu wewe ni unajua kabisa kwamba tabia ulizonazo sasa haziwezi kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

Ndiyo maana mara kwa mara umekuwa unapanga kubadili tabia hizo. Unapanga kuachana na tabia mbaya ulizonazo sasa na kujijengea tabia sahihi za mafanikio makubwa.

Kila mwanzo wa mwaka umekuwa unaweka malengo ya mwaka husika, mengi yakiwa ni ya kubadili tabia ulizonazo. Kila unapojifunza, iwe ni kupitia kusoma, kusikiliza au kuangalia, unatoka na maazimio ya kubadili tabia ulizonazo.

Iwe ni tabia ya kuamka asubuhi na mapema, kutenga muda wa kujifunza, kusimamia vizuri fedha zako, kuweka muda wa kutosha kwenye kazi zako na kudhibiti ulaji wako, umekuwa unapanga mambo mengi mazuri ya kubadilisha kwenye maisha yako.

Lakini kwa bahati mbaya, matokeo yamekuwa ni tofauti na matarajio. Kila tabia ambayo unapanga kuachana nayo, inakuwa ngumu mno kuvunja. Tabia usizozipenda ulizonazo zinakung’ang’ania kama kupe. Wakati huo pia tabia mpya unazopanga kujenga zikiwa ngumu kujengeka.

Matokeo yake umekuwa mtu wa kupanga kila wakati, lakini utekelezaji unakosekana. Hilo limepelekea ufike hatua ya kukata tamaa na kuona kama tabia ulizonazo huwezi tena kuzibadili.

Kama unavyonijua mimi rafiki yako, nimejipa jukumu la kuhakikisha wewe unafanikiwa. Ndiyo maana huwa naangalia maeneo yote unayokwama na kukusaidia kujikwamua ili kupata matokeo bora.

Kwenye eneo hili la kuvunja tabia mbaya na kujenga tabia nzuri za mafanikio, nimeona ni wapi umekuwa unakwama. Na kwenye barua hii nakupa njia ya kujikwamua, ili uweze kupata matokeo ambayo umekuwa unayataka.

Karibu ujifunze hapa jinsi ya kuvunja tabia mbaya usizozipenda na kujenga tabia nzuri zitakazokupa mafanikio makubwa.

1. Elewa Mzunguko Wa Tabia; Kichocheo, Mazoea, Zawadi.

Kosa kuwa sana ambalo umekuwa unalifanya kila unapojaribu kubadili tabia ni kukimbilia kubadili tabia yenyewe, yaani kile unachofanya. Kwa mfano, kama unataka kuacha kunywa pombe, unakazana kuacha kunywa pombe. Unajitahidi sana, lakini baada ya muda unajikuta umesharudi kwenye tabia hiyo.

Huenda umekuwa unajilaumu sana kwamba huna nidhamu ya kutosha kubadili tabia. Lakini siyo kweli, kubadili tabia hakuhitaji nidhamu zaidi, bali kunahitaji mkakati sahihi.

Tabia huwa haitokei tu moja kwa moja, bali huwa ina mzunguko ambao unajirudia mara zote. Mzunguko wa tabia una hatua kuu tatu; Kichocheo, Mazoea, Zawadi. Tabia ni kile unachokuwa unarudia kufanya, yaani mazoea. Lakini hakitokei tu, kunakuwa na kichocheo na zawadi.

Kichocheo ni kile kinachofanya kile kilichozoeleka kifanyike. Ni kama kitu kinachofungua mlango wa tabia husika kufanyika. Kwa mfano wa matumizi ya vilevi, inaweza kuwa ni mtu kuwa na msongo, au mtu kuwa pamoja na marafiki wanaotumia vilevi.

Mazoea ni kile ambacho mtu anafanya baada ya kupata kichocheo. Hiyo ndiyo tabia yenyewe ambayo mtu anaifanya, kutokana na hali anayokuwa kwa wakati huo. Kwa mfano wa matumizi ya vilevi, ni kile kitendo cha kutumia kilevi.

Zawadi ni yale matokeo mazuri ambayo mtu anayapata baada ya kufanya mazoea yaliyochochewa na kichocheo. Zawadi huwa ni matunda ya tabia na ndiyo inafanya mtu kurudia tabia hiyo kila wakati. Kwa mfano wa matumizi ya vilevi, ni ile hali ya kujisikia vizuri baada ya kutumia.

Kwa mzunguko huo, mtu kutaka kuacha kufanya mazoea ambayo ndiyo tabia haiwezi kufanya kazi. Badala yake ni lazima ajue mzunguko mzima wa kichocheo, mazoea na zawadi.

Ni muhimu mtu ujue nini ambacho huwa kinachochea tabia unayotaka kuivunja. Bila kujua hicho, utajikuta kila wakati unarudi kwenye tabia hiyo. Ukishajua kichocheo, unaweka mkakati wa kuchukua hatua ya tofauti pale kichocheo kinapokuwepo. Badala ya kwenda kwenye mazoea ambayo umeshakuwa nayo, ukipata kichocheo, unafanya tabia mpya uliyopanga.

Ukishabadili unachofanya, unahakikisha unapata zawadi ambayo itakufanya urudie tabia mpya unayojenga.

Kwa kutumia mzunguko huo wa tabia na kuufanyia kazi, unakuwa umeingia kwenye kiini cha tabia na kuweza kubadili bila kurudi kwenye tabia unazovunja. Kwa kujua kichocheo cha kila tabia, unakuwa makini pale kinapokuwepo ili usije ukarudi kwenye tabia za zamani.

2. Epuka Msongo Wa Aina Yoyote.

Kichocheo kikubwa cha tabia mbaya ulizonazo na unataka kuzibadili huwa ni msongo. Hivyo kwenye mchakato wako wa kubadili tabia, unapaswa kuhakikisha unaepuka msongo usikurudishe kwenye tabia hizo.

Unaweza kupanga vizuri tabia mpya unayotaka kuijenga na kuanza kuifanyia kazi. Inakuwa rahisi pale mambo yanapokuwa sawa. Unapokuwa kwenye hali ya msongo, akili yako inakimbilia kurudi kwenye tabia ambazo imeshazizoea. Mara nyingi hizo ndizo tabia zinazokufanya ujisikie vizuri.

Hivyo unapokuwa kwenye zoezi la kubadili tabia, epuka hali zinazoweza kukuweka kwenye msongo. Na hata unapojikuta kwenye msongo, jipange sana ili usiishie kurudi kwenye tabia unazopangana kuachana nazo.

Kuwa na njia mbadala za wewe kupambana na msongo bila kurudi kwenye tabia unazoachana nazo. Pata muda wa kutosha wa kupumzika, kwa sababu uchovu unachochea msongo na kurudi kwenye tabia za nyuma.

Eneo muhimu ambalo linashauriwa sana kwenye kujenga tabia mpya ni kupata muda wa kutosha wa kulala. Kukosa muda wa kutosha wa kulala huwa inaongeza msongo na kupelekea mtu kurudi kwenye tabia mbaya anazotaka kuachana nazo.

Hata kama huwezi kujizuia kuingia kwenye msongo, hakikisha unajizuia jinsi unavyokabiliana na msongo huo. Tumia njia za utulivu za kukabiliana na msongo badala ya kurudi kwenye mazoea ya tabia unazopambana kuzivunja.

Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza mambo matano ya kukuwezesha kujenga tabia sahihi na zitakazokupa mafanikio makubwa. Hapa tumeziangalia hizo mbili ambazo zimekufungua sana. Isome barua kupata zote tano kwa ukamilifu ili usikwamishwe na tabia kufanikiwa.

Isome barua hapa; #BZK029; Umekuwa Unajaribu Kubadili Tabia Unashindwa? Tumia Njia Hii Rahisi Na Ya Uhakika Kujenga Tabia Sahihi Za Mafanikio.

Huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga. Badala ya kuhangaika sana na mafanikio, hangaika kujenga tabia za mafanikio, kisha tabia hizo zitakujengea mafanikio ya uhakika.

Elewa mchakato sahihi wa kujenga tabia na ufanyie kazi ili ujijengee tabia zitakazokupa mafanikio kwa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.