Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Moja ya vitu vinavyotukwamisha kwenye safari yetu ya mafanikio ni usumbufu. Na siyo tu usumbufu wa watu kutupigia kelele, bali usumbufu wa sisi kuhangaika na mambo yasiyo na tija kabisa.
Tatizo kubwa ni unaweza kudhani ni rahisi kujua usumbufu huo na kuachana nao. Lakini kwenye uhalisia siyo rahisi kiasi hicho. Sehemu kubwa ya mambo tunayohangaika nayo ni usumbufu kabisa. Lakini sisi tunaona ni mambo yenye tija na kuhangaika nayo.
Tunahangaika na usumbufu bila kujua kwa sababu hatuna vigezo sahihi vya kutenganisha usumbufu na mambo yenye tija. Matokeo yake ni tunajikuta tukihangaika na kila kitu kinachokuja kwetu, hasa pale kinapoonekana ni cha haraka au kimezoeleka kufanyika.
Watu waliofanikiwa wana sifa nyingi sana, na sehemu kubwa ya sifa hizo zinatofautiana baina ya watu. Lakini kuna sifa moja ambayo ipo kwa wote waliofanikiwa. Sifa hiyo ni kuweka umakini wao kwenye jambo moja au machache, kwa lugha rahisi ni kufokasi.
Ukiwaangalia wote ambao hawajafanikiwa, unaona dhahiri jinsi kukosa fokasi kunavyokuwa kikwazo kikubwa kwao. Unawaona wakihangaika na mambo mengi na mengi kati ya hayo hawakutakiwa kuyafanya kabisa.
Ndiyo maana zoezi hili la kuwa na vigezo vya kuchagua nini utahangaika nacho na nini utaachana nacho ni muhimu sana. Kwa sababu linakwenda kukuokoa kutoka kwenye upotevu mkubwa wa muda na nguvu usiokuwa na tija.

Kuna mambo mengi unayohangaika nayo, ambayo wewe binafsi unadhani ni ya muhimu, lakini kiuhalisia hayana mchango wowote kwenye mafanikio unayotaka kupata. Na unashindwa kujua hilo kwa sababu huna vigezo sahihi vya kupima.
Kukosekana kwa vigezo vya kupima umuhimu wa mambo tunayofanya, kunapelekea tufanye mambo kwa hisia na kwa mazoea. Tunafanya kwa hisia pale tunaposukumwa kwa tamaa ya kupata kitu fulani au hofu ya kupoteza. Na tunafanya kwa mazoea pale tunapofanya kitu kwa sababu ndivyo ambavyo tumekuwa tunafanya.
Kama unataka kujenga mafanikio makubwa kama unavyotaka, ni wakati sasa wa kupima umuhimu wa kila unachofanya ili kuweka umakini wako kwenye yale yenye tija pekee.
Kwenye barua hii unakwenda kujifunza vigezo vitatu vya kupima umuhimu wa kila unachofanya. Kwa kuvijua na kuvifanyia kazi, kamwe hutasumbuka tena na mambo yasiyokuwa na tija.
Mantiki – Ina Maana Gani?
Mara nyingi huwa tunapokea vitu kwa sababu tu tumepewa au vimekuja kwetu, bila hata kujua mantiki yake. Inaweza kuwa ni ushauri ambao watu wamekupa au sababu ambazo umekuwa unajipa wewe mwenyewe. Tunapokea na kufanyia kazi bila kujua maana halisi ya hicho tulichokubaliana nacho.
Mantiki, yaani kujua kitu kina maana gani ndiyo kigezo cha kwanza kabisa cha kuchuja vitu ambavyo tunajihusisha navyo. Ni lazima tujue mantiki ya kila kitu ambacho tunakikubali au kukifanya. Hata kama watu wengine wanaamini na kufanya, hata kama ndiyo tumekuwa tunafanya, haina maana kuendelea na kitu kama hatujui mantiki yake.
Ushahidi – Umejuaje Ni Kweli?
Baada ya kuwa na mantiki ya kila unachoamini na kufanya, hatua inayofuata ni kupata ushahidi wa mantiki hizo. Kile ambacho unakuwa umetoa kama maana ya unachoamini na kufanya, unapaswa kueleza umejuaje kwamba kitu hicho ni kweli.
Hii ni hatua muhimu sana ya kutenganisha hisia na uhalisia, kwa sababu ushahidi unahitajika. Vitu vingi tunavyohangaika navyo, hatuna ushahidi wa kuonyesha kwamba ni vitu vya kweli na sahihi kwa safari tuliyonayo. Ni vitu ambavyo tumeamini tu kwa hisia na mazoea.
Matumizi – Ina Manufaa Gani?
Ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka, kila unachoamini na kufanya ni lazima kiwe kina mchango kwenye mafanikio hayo. Ni jambo rahisi kueleweka, lakini inashangaza jinsi watu wanahangaika na mambo mengi ambayo hayana mchango wowote kwenye kile wanachotaka.
Kama ambavyo tumeshaona kwenye vigezo vilivyopita, mambo mengi watu wanafanya kwa hisia na mazoea. Hawakai chini na kujiuliza yale wanayofanya yana manufaa gani kwenye kile wanachotaka kufikia.
Manufaa ya kitu ndiyo kigezo cha tatu cha kupima kama unapaswa kuamini na kufanya kitu au la. Kitu kinaweza kuwa na mantiki na ukawa na ushahidi, lakini kama hakina manufaa, hakina mchango kwenye safari yako ya mafanikio.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeelezea vigezo hivi vitatu kwa kina zaidi na hatua za kuchukua kwenye kila kigezo ili kuhakikisha hakuna usumbufu unaokutoa kwenye mchakati wako wa mafanikio.
Isome barua hiyo hapa; #BZK028; Mantiki, Ushahidi Na Matumizi – Vigezo Vitatu Vya Kutokusumbuliwa Na Chochote Kwenye Safari Ya Mafanikio.
Kuna usumbufu mwingi umekuwa unajipenyeza kwenye mambo unayofanya na huo ndiyo umekuwa unakwamisha kupata matokeo unayotaka. Kwa kuwa na vigezo sahihi vya kuchuja, utaweza kuondokana na usumbufu huo na ukapata matokeo makubwa.
Vigezo vitatu ulivyojifunza hapa, vinachuja kwa usahihi sana yote unayojihusisha nayo na kujua yapi yenye tija na yasiyokuwa na tija. Vitumie vigezo hivi kwenye mambo yote ili uache kupoteza muda na kujikwamisha kufanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.