Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Tunaishi kwenye zama zenye ushindani mkali sana. Hiyo ni kwa sababu mahitaji ya kuingia kwenye kitu chochote yameshuka sana. Kwenye zama hizi, mtu yeyote anaweza kuingia kwenye kazi au biashara yoyote anayotaka na kuweza kufanya vizuri.

Ujio na ukuaji wa kasi wa Akili Mnemba (Artificial Intelligence), umeondoa kabisa vikwazo vilivyokuwa vinawazuia wengi kuingia kwenye kazi au biashara mbalimbali.

Kabla ya akili mnemba, mtu alihitaji kuwa na ujuzi mkubwa na kuwa na timu kubwa ili kutekeleza majukumu yanayompa matokeo makubwa. Lakini uwepo wa akili mnemba umemwezesha mtu yeyote kuweza kutekeleza majukumu mengi akiwa peke yake.

Watu walianza kwa kukataa kwamba akili mnemba haiwezi kuchukua kazi zao. Lakini kadiri muda unavyokwenda, kila mtu anaona dhahiri teknolojia hii ikitikisa eneo ambalo yupo. Kwani hata kama haitaondoa kabisa watu, bado itapunguza sana idadi ya watu wanaohitajika kukamilisha majukumu kwenye eneo hilo.

Hali hii inazidisha ushindani kwenye pande mbili. Upande wa kwanza ni kwenye utendaji, ambapo watu wachache zaidi watahitajika kutekeleza majukumu mbalimbali. Hili litafanya nafasi za kazi kuwa chache na ushindani kuwa mkali.

Upande wa pili ni kwenye biashara, ambapo kila mtu anaweza kuingia kwenye biashara anayotaka. Hili linafanya biashara kuwa nyingi na ushindani kuwa mkali.

Ili kuvuka ushindani huo mkali na kupata mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka, ni lazima uweze kujitofautisha kabisa na wengine wote waliopo kwenye kile unachofanya.

Ni lazima uweze kujitofautisha wewe na kile unachofanya ili usisumbuliwe na hizi teknolojia mpya kama akili mnemba. Linaweza kuonekana zoezi gumu, lakini ugumu wake ndiyo unafanya liwe na thamani zaidi.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekupa mambo matano ya uhakika ya kufanyia kazi ili uweze kujitofautisha na kushinda kwenye zama hizi za Akili Mnemba. Hizo ni njia ambazo kila aliye makini na mafanikio yake anapaswa kuzijua na kuzifanyia kazi.

Kwenye makala hii ya #AmkaNaKocha nitakushirikisha njia mbili kati ya hizo tano, ambazo zitakufungulia njia ya kuanza kujitofautisha ili kuweza kufanya makubwa kwenye zama hizi za ushindani mkali. Baada ya kuanza na njia hizi mbili, utaenda kwenye #BaruaYaKocha kukamilisha zilizobaki ili uweze kuwa bora sana na usiyeweza kubadilishwa na mtu au teknolojia yoyote.

1. Kuwa Bora Sana Kwenye Unachofanya Kiasi Cha Kuwa Vigumu Kubadilishwa.

Kitu kimoja ambacho kinaendelea kujidhihirisha kwenye zama hizi za akili mnemba ni kila anayeweza kubadilishwa, atabadilishwa. Tena siyo atabadilishwa kwa mtu, bali atabadilishwa kwa akili mnemba.

Tunaona jinsi ambavyo akili mnemba inakuwa na uwezo wa kufanya majukumu ambayo awali yalikuwa yanafanyika na binadamu pekee. Na kadiri muda unavyokwenda, uwezo wa akili mnemba unaongezeka.

Kuna watu bado wapo kwenye hali ya kukataa kwamba akili mnemba haiwezi kuwaondoa kwenye kazi na biashara zao. Lakini hicho ni kitu ambacho kimekuwa kinakuwepo kila teknolojia mpya inapokuja. Kuna wengi walidhani ujio wa kompyuta hautaathiri kazi zao. Lakini leo hii kila kazi inahusisha kompyuta.

Badala ya kukazana kukataa kwamba akili mnemba haiwezi kuathiri kazi au biashara yako, kazana kuwa bora sana kwenye kile unachofanya kiasi cha kuwa vigumu kubadilishwa. Tafuta kitu au eneo ambalo utakuwa bora sana, utazalisha matokeo makubwa sana kiasi kwamba hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo.

Na kwa zama hizi za akili mnemba, hakikisha unakuwa bora sana kwenye kujitofautisha na kuwa halisi. Kujitofautisha unaweka nguvu zako kwenye yale unayofanya kwa ubora kuliko wengine. Na kuwa halisi unakuwa wewe, kama binadamu na siyo kuwa unayeiga au kufanya kama mashine.

Kitu kimoja ambacho kimeanza kutokea, ambacho kimechochewa na akili mnemba ni watu kurudi kwenye uhalisia wa kibinadamu. Hivyo kama wewe utakuwa bora kwenye kuwa binadamu, utakuwa salama kwenye mabadiliko makubwa yanayoendelea.

Kuwa bora siyo kitu cha mara moja, ni zoezi endelevu. Hivyo wajibu wako ni kila wakati kukazana kuwa bora zaidi ya ulivyo, ili mabadiliko yanayoendelea yasikufanye uwe rahisi kubadilishwa.

2. Kuwa Bora Sana Kwenye Mawasiliano.

Moja ya vitu vinavyotufanya sisi kuwa binadamu, na hata kutofautiana na viumbe wengine ni uwezo wetu wa mawasiliano. Tumekuwa na uwezo wa kuwashawishi wengine kukubaliana na sisi na kutupa tunachotaka, kupitia mawasiliano.

Wakati teknolojia zinaanza kuja, eneo lililorahisishwa zaidi ni la mawasiliano. Kutoka maongezi ya ana kwa ana mpaka ya simu na hata kuonana kwa video. Kutoka ujumbe wa kutuma kwa mtu mmoja mmoja mpaka kutuma kwa wengi.

Hata akili mnemba ilivyoanza kuja, watu wamekimbilia kuitumia kwenye kurahisisha mawasiliano. Watu wamekuwa wanaitumia kupata majibu sahihi ya kutoa kwa watu ili kuwa na ushawishi.

Matokeo yake sasa, mawasiliano yamekuwa mabovu na yaliyokosa ile hali ya ubinadamu na inayoleta ushawishi mkubwa. Jumbe nyingi ambazo watu wanatumiana, ni za kutokana na akili mnemba.

Akili mnemba imefanya kila mtu kuonekana ana ushawishi mkubwa, lakini matokeo yake ni ushawishi huo umepotea kwa sababu mawasiliano ya watu karibu wote yanafanana.

Ili kujitofautisha, kuwa bora sana kwenye mawasiliano, kama binadamu. Jijengee uwezo wa kuwasiliana na watu vizuri, kwa kuweka uhalisia na ubinadamu kwenye mawasiliano yako. Iwe ni mawasiliano ya ana kwa ana, simu, au maandishi, hakikisha wewe binadamu ndiye unayewasiliana.

Utaweza kutumia akili mnemba kufanya tafiti na kupata taarifa sahihi unazohitaji. Ila inapokuja kwenye kuwasilisha taarifa hizo, hakikisha unafanya wewe binadamu.

Na unapowasiliana kama binadamu, hakikisha unaweka hali za kibinadamu. Gusa hisia za watu wakati unawasiliana nao. Wasiliana nao kwa kile ambacho tayari kipo kwenye fikra zao. Na zaidi, jiweke kwenye nafasi zao na hakikisha unachowapa kina manufaa kwao.

Tunakoenda, akili mnemba zitakuwa zinawasiliana zenyewe na kukamilisha majukumu ya msingi. Lakini kwa mambo makubwa na yanayohusisha maamuzi muhimu, yatategemea zaidi mawasiliano ya kibinadamu. Hakikisha unakuwa bora kwenye hilo ili unufaike na fursa hizo.

Rafiki, umeona jinsi njia hizo mbili tu zilivyo na nguvu kubwa ya kukutofautisha kama utazifanyia kazi. Sasa unapaswa kuingia kwenye #BaruaYaKocha na kukamilisha kusoma zilizobakia ili ukamilishe kifurushi chako cha ushindi.

Soma barua hiyo hapa; #BZK027; Jinsi Ya Kujitofautisha Kwenye Zama Hizi Za Akili Mnemba (Artificial Intelligence).

Mapinduzi makubwa ya teknolojia yanayoendelea yanatuweka kwenye hatari ya nafasi zetu kuchukuliwa na teknolojia hizo mpya. Njia pekee ya kuzuia hilo ni kuhakikisha tunakuwa bora kwenye kile ambacho hakuna mwingine anayeweza kukifanya kama sisi.

Weka juhudi kubwa kwenye kuwa wewe na kufanya kwa ubora sana yale yanayokutofautisha ili uwe salama kwenye zama hizi za ushindani mkali.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.