Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Hatua muhimu sana kwenye safari ya mafanikio makubwa ni kuepuka kuwa mpumbavu. Hiyo ni kwa sababu upumbavu ni mzigo ambao ni vigumu sana mtu kuutua. Wakati ujinga inawezekana kuutua kwa kujifunza, upumbavu huwa unamganda mtu kwa muda mrefu.
Huwa kuna aina mbili za upumbavu. Ya kwanza ni ule upumbavu wa msingi ambao mtu anakuwa nao. Huu huwa ni mgumu kutoa kwa sababu mtu anajiona yupo sahihi. Kwa bahati nzuri wewe huna upumbavu huo, maana ungekuwa nao usingekuwa unasoma hapa.
Aina ya pili ni upumbavu wa kujitakia. Huu huwa unatokana na kitu ambacho mtu unafanya kwa nia njema, lakini matokeo yake inakuweka kwenye upumbavu. Mara kwa mara, kwa kutokujua, umekuwa unajiingiza kwenye aina hii ya upumbavu.
Kwenye makala hii, tutaangalia aina hiyo ya upumbavu wa kujitakia na jinsi ya kuuepuka kwa kutumia ili uache kujikwamisha kufanikiwa. Upumbavu huu unatokana na vitu ambavyo tumezoea kufanya, bila kujua vinatukwamisha.
Unapata nafasi ya kujifunza vitu hivyo ili visiwe kikwazo kwako kujenga mafanikio unayoyataka.

1. Epuka Watu Wanaoongozwa Na Hisia.
Sisi binadamu wote ni viumbe wa hisia, maamuzi yoyote tunayofanya, huwa yana sehemu ambapo hisia inaingia. Lakini maamuzi bora ni yale ambayo mantiki imetumika na siyo hisia pekee.
Kuna watu ambao maamuzi yao yanaongozwa zaidi na hisia kuliko mantiki. Hao huwa ni watu wagumu sana kubadili kile walichoshikilia, kwa sababu hakuna mantiki utakayowapa wakaelewa.
Kama mtu hakufanya maamuzi yake kwa mantiki, huwezi kuyabadili kwa mantiki. Unakuwa unaongea lugha ambayo mtu haielewi, kwa sababu siyo iliyomfikisha pale alipo.
Kabla hujaendelea kujadiliana na mtu, jua kwanza huwa anafanya maamuzi yake kwa namna gani. Na hilo litajidhihirisha kwenye maeneo mengi ya maisha yake. Hata kwa kumwuliza tu maswali ya kimantiki, utajua ni jinsi gani mtu alifikia maamuzi yake.
Kundi lingine la kuepuka hapa ni watu wenye itikadi kali. Watu wa itikadi huwa hawabadiliki hata uwaonyeshe kwamba hawapo sahihi. Watu wakishashika itikadi, haiwezekani kabisa ukawashawishi kinyume na wanavyoamini.
Ndiyo maana mabishano ya dini, kabila, timu ambazo watu wanashabikia, hayaishiagi kwa upande wowote kubadilika. Watu watabishana kwa muda mrefu, lakini kila upande utabaki vile vile ulivyokuwa.
Usije kamwe ukajisumbua kubishana na watu wanaofanya maamuzi kwa hisia au walioshikilia itikadi. Utakuwa umejitakia upumbavu wewe mwenyewe na utapoteza muda na nguvu bila ya tija.
2. Wakati Mwingine Ni Mtego.
Kuna watu wanabishana na wewe na kukukatalia, siyo kwa sababu hawataki kubadilika, bali kwa sababu wanakutega ili uingie kwenye mipango yao. Watu wanapokuwa wanakuwinda kwenye mambo fulani, wanaweza kutumia njia ya kutofautiana na wewe kwenye kile unachojua ni sahihi.
Lengo lao ni kukuweka kwenye hali ya msongo, ili ufanye maamuzi ya kukosea na wao wanufaike na maamuzi hayo. Wanajua kabisa kwamba hutakubaliana na upande wanaokupa, na wataung’ang’ania upande huo ili tu kukuvuruga wewe. Ukishavurugwa unashindwa kufanya maamuzi sahihi.
Jua nia ya mabishano ambayo watu wanaleta kwako, angalia manufaa ya kila upande kwenye mabishano yao. Ukiona jambo halina tija yoyote kwako, usiendelee kuhangaika nalo.
Kuwa na wasiwasi pale unapojadiliana na watu na wakasimamia upande wao, kisha baada ya hapo wakaja na mpango mwingine. Jua kabisa mjadala wa awali ulitengenezwa ili kukuvuruga kwanza, na ukishavurugwa hutafanya vizuri kwenye mpango mwingine.
Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina mambo mengine matatu ya wewe kuacha kufanya ili uepuke upumbavu wa kujitakia. Kama ambavyo umeona haya mawili uliyojifunza hapa yana nguvu, hayo yaliyobakia yana nguvu zaidi.
Unapaswa kuyaelewa yote na kuyafanyia kazi kwa kina ili uache kujikwamisha wewe mwenyewe kufanikiwa.
Soma barua kamili hapa; #BZK026; Tumia Hii Kanuni Ya Punda Kuepuka Upumbavu Wa Kujitakia.
Rafiki, huenda unalalamika na kulaumu watu na hali mbalimbali zinazokukwamisha kufanikiwa. Lakini nataka nikuambie kitu kimoja, wewe mwenyewe ndiye unayejikwamisha kwa sehemu kubwa.
Na unajikwamisha bila hata kujua, kwa sababu ya upumbavu wa kujitakia unaokuwa umezama. Kwa kuujua upumbavu huo na kuukwepa, unaondoa vikwazo ambavyo umekuwa unajiwekea wewe mwenyewe kufanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.