Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Dunia ina aina mbili za watu, watu wa kawaida na watu wasio wa kawaida. Kundi kubwa ni la watu wa kawaida, ambao wanafanya mambo ya kawaida na yaliyozoeleka na walio wengi.
Ni salama kuwa mtu wa kawaida na ndiyo maana hilo ndiyo kundi lenye watu wengi zaidi. Lakini huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kuwa mtu wa kawaida, na ndiyo maana wengi sana hawapati mafanikio makubwa.
Watu wasio wa kawaida ni kundi dogo sana la watu duniani. Hili ndiyo kundi la watu wenye mafanikio makubwa, kwa sababu wanafanya mambo ambayo ni ya tofauti.
Watu wasio wa kawaida siyo kwamba wana pembe kichwani au wana mikia, wana kila ambacho watu wengine wanacho. Na wala siyo kwamba wana akili nyingi sana kuwashinda walio wa kawaida.
Kitu pekee kinachowatofautisha watu wa kawaida na wasio wa kawaida ni jinsi wanavyoichukulia dunia. Watu wa kawaida wanabadilika ili kuendana na dunia, ndiyo maana wanafanya mambo yanayofanana na yanayokubalika na walio wengi.
Watu wasio wa kawaida huwa wanaibadili dunia iendane na wao. Ndiyo maana wanafanya mambo yasiyo ya kawaida na hayo ndiyo yanawapa matokeo ya tofauti.

Kwenye makala hii unakwenda kujifunza jinsi ya kuondoka kwenye watu wa kawaida na kuwa asiye wa kawaida ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
1. Wote Tunazaliwa Tukiwa Siyo Wa Kawaida.
Mwangalie mtoto yeyote mchanga na anayekua, na utagundua kwamba ni watu wabishi sana. Watoto huwa hawakubaliani na yale wanayoelekezwa na watu wazima. Waambie wasifanye kitu na hicho ndiyo watakachofanya. Na kwa kila wanachoambiwa, huwa wanahoji maswali.
Hicho kilichopo kwa watoto ndicho ambacho tumezaliwa nacho watu wote. Hali ya kutaka dunia iendane na sisi na siyo sisi kuendana na dunia. Hali ya kujaribu kila tunachokatazwa ili tujionee wenyewe. Na hali ya kuhoji kila kitu badala tu ya kupokea maelekezo kama yalivyo.
Kwa bahati mbaya, kadiri tunavyokua, kwa kulazimishwa pamoja na adhabu mbalimbali, tunajikuta tunaacha kutokuwa wa kawaida na kuchagua kuwa wa kawaida. Tunafanya hivyo kwa sababu wale wenye mamlaka wanatumia hilo kama njia ya kutupa kile tunachotaka.
Ni wakati sasa wa kukumbuka kwamba wewe hukuzaliwa ukiwa wa kawaida. Ndani yako kuna hali ya kutokuwa wa kawaida. Usikubali kuendelea kuzika hali hiyo kwa sababu tu dunia inakutaka uwe hivyo.
2. Ni Salama Kuwa Wa Kawaida.
Maamuzi yote ambayo binadamu tunayafanya, yana manufaa fulani. Inapokuja kwenye kuacha kutokuwa wa kawaida na kuwa wa kawaida ni kwa sababu za uhakika na usalama. Kuwa wa kawaida ni kitu salama, kwa sababu tunafanya mambo yaliyozoeleka na kukubalika na hivyo kupata matokeo sawa na ya wengine.
Kwa kuwa usalama ndiyo kitu tunachotaka sana, na kwa kuwa tunapenda kukubalika na wengine, inatulazimu kuwa watu wa kawaida.
Kuwa wa kawaida hakutuingizi kwenye migogoro na watu wengine. Kuwa kawaida hakutufanyi tujaribu vitu vipya na vya tofauti. Kupata matokeo ya kawaida kunatupa uhakika kuliko kujaribu vitu vipya ambavyo hatujui vitatupa matokeo gani.
Lakini usalama tunaouchagua kuwa wa kawaida, una gharama ya kukosa mafanikio makubwa tunayoyataka. Tunapotaka uhakika wa matokeo, tunakuwa tumeyakataa matokeo makubwa ambayo tungeweza kuyapata.
Ndiyo maana sehemu salama zaidi ya mtoto kuwa ni tumboni mwa mama yake, lakini hawi na maisha yake binafsi kwa njia hiyo. Sehemu salama zaidi ya mtu kuwa ni gerezani, lakini anakuwa hana maisha. Na sehemu salama zaidi ya meli kuwa ni ufukweni, lakini meli haikutengenezwa kukaa ufukweni.
Pamoja na kutaka sana usalama, hicho ndiyo kikwazo cha kupata matokeo makubwa yaliyo ndani ya uwezo wako.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo mengine matatu muhimu sana unayopaswa kufanyia kazi ili kuibadili dunia iendane na wewe badala ya wewe kubadilika na kuendana na dunia.
Mambo hayo ni Ni Hatari Kutokuwa Wa Kawaida, Usijitambulishe Kwa Kile Unachofanya, na Egemea Upande Usioeleweka.
Karibu ujifunze hayo kwa kina kwa kusoma barua hii; #BZK025; Usibadilike Kuendana Na Dunia, Ibadili Dunia Iendane Na Wewe.
Watu wa kawaida huwa wanaishia kuwa na maisha ya kawaida, kwa sababu wanabadilika kuendana na dunia.
Watu wasio wa kawaida huwa wanapata mafanikio makubwa, kwa sababu wanaibadili dunia iendane na wao.
Je wewe umechagua kuwa upande upi? Ndani yako una nguvu ya kuchagua upande wowote unaotaka, hivyo chagua kwa usahihi ili upate matokeo unayotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.