Soma hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Hongera sana, tayari umeshafanikiwa.

Nimeanza kwa pongezi hizo, siyo kwa sababu nakutania, ila kwa sababu ndiyo ukweli ulivyo. Hapo ulipo sasa, tayari umeshafanikiwa kabisa. Maisha uliyonayo sasa ni utabiri binafsi uliotimia.

Hakuna chochote kinachotokea kwenye maisha yako ambacho ni bahati au ajali. Bali kila kinachotokea ndivyo ulivyoamini na kufikiri kwa muda mrefu. Hata kama unaona bado hujafika unakotaka, hapo ulipo sasa tayari ni sehemu uliyoichagua wewe mwenyewe.

Sisi binadamu huwa tunavutia na kuvumilia yale yanayoendana na fikra na imani zetu. Kile kinachoonekana kwa nje, tayari kinakuwa kimevutiwa au kinaaminika kwenye fikra zetu.

Matokeo ya nje yanapokuwa tofauti na kile tunachoamini ndani, huwa hatuwezi kutulia kabisa. Tutahangaika kwa kila namna mpaka matokeo ya nje yaendane na fikra za ndani.

Ndiyo maana nimeanza barua hii kwa kukupa pongezi za hapo ulipo sasa, kwani ni mafanikio ambayo umeshayapata.

Nimekupongeza siyo kwa sababu nataka ubaki hapo, la hasha. Najua unasoma barua hizi kwa sababu una kiu ya kupiga hatua kubwa zaidi ya hizo ulizopiga sasa. Lakini huwezi kwenda sehemu yoyote bila kutoka pale ulipo sasa. Na kutoka ulipo, lazima upaelewe kwanza.

Kubadili Imani Kunaanza Na Kubadili Ushahidi.

Kinachowakwamisha watu wengi kubadilika ni kutaka kubadili yale wanayofanya kabla ya kubadili kile wanachoamini. Na hata wanapojaribu kubadili imani walizonazo, wanashindwa kwa sababu wanapuuza nguvu ya ushahidi kwenye imani walizonazo.

Kinachojenga na kuimarisha imani zetu ni ushahidi tunaoupata. Tunazidi kuamini kitu pale kinapotupa matokeo yale yale tunapokifanya. Kama unaamini ukivaa nguo nyekundu unakutana na bahati, na ukavaa kweli ukapata bahati, utaamini zaidi hivyo.

Akili zetu huwa zinatafuta kila aina ya ushahidi wa kukazia kile tunachoamini. Ni kama ubongo unakuambia; ‘Unaona? Nilikuambia hiki ndiyo sahihi.’

Kwa mfano, unaamini mfanyakazi mwenzako hakupendi na anakula njama ili ufukuzwe kazi. Siku unafika kazini asubuhi na kumsalimia, ila haitiki. Hilo linaongeza imani yako kwamba hakupendi. Lakini huenda hajakusikia, huenda ana mawazo yake yamemtinga. Huenda kuna mambo mengi yamemfanya asikusikie na kukujibu. Lakini wewe umechagua ushahidi unaolinda imani yako.

Hivi ndivyo waganga wanavyotumia imani na ushahidi kuonekana wanajua kinachokusumbua. Watakuuliza maswali mengi, watakusanya taarifa zako nyingi, kisha watakupa maelezo ambayo tayari wewe una ushahidi nayo. Hapo utaona wana nguvu za kujua yanayokusumbua, kumbe wanakupa ushahidi ambao wewe umewapa.

Kazi yetu kubwa binadamu huwa ni kulinda imani tuliyoijenga kupitia ushahidi tunaoupata. Kuna mstari wa Biblia huwa unatumika sana kwenye misiba, unaosema; ‘Vita umevipiga, imani umeilinda….’ Hata kama mtu siyo mtu wa imani, kwa kipindi chote uko hai, kuna imani umezilinda sana, hasa za uwezo wako na yale unayofanya.

Unapotaka kupata mafanikio makubwa, lazima ubadili kile unachoamini. Kubadili unachoamini kunaanzia kwenye ushahidi unaoutumia. Hapo kwenye ushahidi ndiyo tunapata kanda tatu za kifikra ambazo tunapaswa kuzielewa na kuzitumia kujenga mafanikio makubwa.

Ukanda Wa Faraja (Comfort Zone)

Huu ni ukanda ambao mtu umezoea kuwepo. Ni kwenye ukanda huu ndiko unapata ushahidi wako wa sasa. Na unajisikia faraja kukaa kwenye ukanda huu, kwa sababu unapata matokeo ambayo tayari umezoea kuyapata.

Ukanda huu hauna hatari ya kukosea au kupoteza, kwa sababu hakuna kitu kipya ambacho mtu unakifanya. Ni ukanda usiokuwa na gharama kubwa kwa mtu.

Lakini pia ndiyo ukanda ambao hauwezi kujenga mafanikio makubwa. Hiyo ni kwa sababu mtu anakuwa anafanya yale yale aliyozoea kufanya.

Huu ndiyo ukanda uliowameza wengi na kuwazuia kufanikiwa. Kwenye ukanda huu watu wanajisikia vizuri, hawana msongo wowote unaowafanya wajisukume zaidi. Wanaridhika na matokeo ya kawaida wanayoyataka na hilo linawazuia kupata matokeo makubwa zaidi.

Wapo watu wanaoanzia chini na kuwa na msukumo wa kupiga hatua. Wanafanya mambo ya tofauti na kupata matokeo mazuri. Lakini ghafla wanabaki pale walipofika na kushindwa kwenda mbali zaidi.

Hilo linasababishwa na watu kufika kwenye ukanda wa faraja. Walipokuwa chini hawakuwa na faraja, walihofia vile walivyokuwa wamekosa. Lakini baada ya kupata matokeo, wanabadilika na kuhofia kupoteza kile ambacho tayari wamepata.

Hofu ya kuwapoteza inawafanya wasijaribu vitu vipya na hilo kuwafanya wabaki kwenye huo ukanda wa faraja.

Kwenye safari yako ya kujenga mafanikio makubwa, unatakiwa kuanza kuachana na ukanda wa faraja. Usiridhike na ushahidi unaoupata sasa. Taka kupata ushahidi mkubwa zaidi ili uweze kufanya makubwa zaidi.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina kanda nyingine mbili na kukuonyesha ukanda sahihi unaopaswa kuwa ili upige hatua kubwa zaidi ya hapo ulipo sasa.

Kwa sasa umekwama kwenye ukanda wa faraja, ambapo unafanya hivyo ulivyozoea kufanya na kuishia kupata matokeo ambayo umekuwa unayapata.

Ili kupata matokeo ya tofauti, lazima utoke kwenye huo ukanda wa faraja uliopo sasa. Karibu usome barua hiyo muhimu kwako kupiga hatua kubwa.

Isome barua hapa; #BZK024; Kanda Tatu Za Kifikra Na Jinsi Ya Kuzitumia Kujenga Mafanikio Makubwa.

Rafiki, mafanikio unayotaka hayapo mahali fulani unakopaswa kwenda ndiyo uyapate. Bali yapo ndani ya fikra zako, ambazo bado hujaweza kuzifikia kwa sababu upo kwenye ukanda wa faraja.

Wajibu wako mkubwa kwenye safari ya mafanikio ni kutoka kwenye ukanda wa faraja uliopo na kwenda kwenye ukanda sahihi utakaokupa mafanikio. Tekeleza wajibu huo kwa usahihi ili upate mafanikio unayotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.