Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Ukienda kwenye bustani na ukaona kipepeo mzuri, utavutiwa kumfuata na kumshika. Lakini utakapomkaribia, ataruka na kwenda kwenye ua jingine. Ukisogelea tena hilo ua, ataruka na kwenda mbali zaidi. Kila unapomsogelea kipepeo, anaruka kwenda mbali.
Lakini kama utaamua kukaa na ua zuri, ambalo linamvutia kipepeo, yeye mwenyewe atakuja kwako. Hutalazimika kumkimbiza ili kumkamata, badala yake atajileta kwako yeye mwenyewe.
Rafiki, hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kuwashawishi watu. Watu wengi hudhani wanaweza kuwashawishi na kuwabadilisha watu wakubaliane nao kwa kutumia maneno mengi. Lakini kila unapowapa watu maneno mengi ya kuwashawishi, ndiyo unawafanya wawe mbali zaidi na wewe.
Ukitaka kuwashawishi watu wabadilike na kukubaliana na wewe, unatakiwa kutumia hiyo mbinu ya kipepeo. Badala ya kutumia maneno mengi kuwashawishi, tafuta kinachowavuta kuja upande wako na watajishawishi wao wenyewe kubadilika.

Kwenye #BaruaYaKocha, nimeshirikisha mambo matano ya kufanya ili uweze kuwashawishi watu wakubaliane na wewe bila kuonekana unawalazimisha.
Kwenye makala hii nakupa mawili ambayo yana nguvu sana, ukiweza kuyatumia vizuri, hakuna atakayeweza kukukatalia unachotaka. Na utakwenda kuisoma barua ambayo nitakuwekea ili upate yote matano.
1. Kamwe Usipingane Na Watu.
Huwa tunasukumwa kupingana na watu pale wanachofanya au kuamini kinapokuwa tofauti na tunachofanya na kuamini sisi. Pale tunapoona tupo upande sahihi na wengine wanaenda kinyume na upande huo, tunasukumwa kuwapinga na kuwaleta kwenye upande wetu.
Lakini hilo la kuwapinga watu halijawahi kufanya kazi. Kwani watu wanaona wako sahihi kwa wanachofanya na kuamini. Hata uwape ushahidi kiasi gani kwa nini wewe upo sahihi na wao wamekosea, haitasaidia.
Ndiyo, unataka kuwabadilisha watu wakubaliane na wewe. Lakini kama utaanza kwa kupingana nao moja kwa moja, hutaweza kutimiza hilo.
Kitu cha kwanza unachopaswa kujua ni kwamba hupaswi kupingana na watu moja kwa moja, hata kama wewe upo sahihi na wao wanakosea. Watu wanapopingwa, huwa wanapambana kujitetea na kuonyesha kwa nini wapo sahihi.
Na hata kama utawashinda kwa hoja kwamba wewe upo sahihi, bado wataendelea kushikilia upande wao. Hivyo ushindi wowote unaokuwa umeupata, hauna manufaa kwako, haukusaidii kupata kile unachotaka.
Wajibu wako kwenye kuwafanya watu wakubaliane na wewe ni kutokupingana nao kwa namna yoyote ile. Lakini hilo halimaanishi ukubaliane na upande wao. Unaweza kutokukubaliana nao, bila kuwapinga moja kwa moja.
Na hapo ndipo hatua inayofuata inapokuwa muhimu kwenye mchakato wa kuwabadilisha watu.
2. Waambie Wanachotaka Kusikia.
Watu wanapenda kusikia vitu vizuri, watu wanapenda kusifiwa na kuthaminiwa. Katika harakati zako za kutaka kuwabadilisha watu na kuwafanya wakubaliane na wewe, hakikisha unawaambia wanachotaka kusikia.
Hilo linaanza kwa kuwasifia. Haijalishi unapingana na mtu kiasi gani, tafuta kitu unachoweza kumsifia nacho. Na kiwe ni kitu cha kweli kabisa ambacho kinaonyesha uwezo wake. Hata kama ni vitu vidogo kama kuwahi, kupangilia mambo yake vizuri n.k. Unapowasifia watu unawafanya wakuone unawaelewa na kuwathamini.
Waambie watu wapo sahihi kabisa, kwa kile wanachofanya au kuamini, hata kama unajua hawapo sahihi. Kwa sababu watu wanataka kusikia kwamba wako sahihi, hilo ndiyo unapaswa kuwaambia. Unapoanza kwa kuwaambia watu wapo sahihi, wanakosa cha kubishana na wanavutiwa kukubaliana na wewe.
Ni baada ya kuwa umewanyima cha kubishana na kuvutiwa kukubaliana na wewe, ndiyo unawaonyesha na upande mwingine wa hicho walichoshikilia. Kwa wakati huo wanakuwa tayari kukubaliana na wewe, kwa sababu walishaanza kwa kukubaliana.
Ukianza kwa kuwaambia watu wamekosea au hawapo sahihi, wanafunga kabisa sehemu za ubongo wao zinazohusika na kukubali kitu. Wewe unazuia hilo kutokea kwa kuanza kukubaliana na watu ili kuacha ubongo wao wazi. Ni ubongo ulio wazi ndiyo unaokuwa tayari kupokea mambo mapya.
Haya mawili unaweza kuanza kuyafanyia kazi mara moja na ukawa na ushawishi mkubwa wa kuwabadilisha wengine wakubaliane na wewe bila kuwalazimisha.
Kupata njia zote tano, soma barua hii; #BZK023; Njia Rahisi Ya Kuwabadilisha Watu Na Kuwafanya Wakubaliane Na Wewe.
Kila unachotaka, kipo kwa wengine. Uwezo wako wa kuwashawishi wengine wakubaliane na wewe ndiyo utakaoamua mafanikio utakayoyapata. Jifunze kuwashawishi watu bila kuwalazimisha, ili wengi wakubaliane na wewe na kukupa kila unachotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.