Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio ni rahisi na pia ni magumu.

Hiyo ni kauli inayoweza kukuchanganya, kwa sababu inaleta pamoja vitu vinavyokinzana.

Lakini ni kauli sahihi, kwa sababu mafanikio yanakupokea kama unavyoyaendea.

Ukiyaendea mafanikio kwa urahisi, hasa pale unapokuwa unatafuta njia za mkato, yanakuwa magumu sana kwako.

Lakini ukiyaendea mafanikio kwa ugumu, kwa kufuata michakato sahihi, yanakuwa rahisi kwako.

Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho kwako wewe rafiki yangu ni hiki, kama unasoma hapa, ungeweza kuwa mbali zaidi ya hapo ulipo sasa.

Namaanisha hapo ulipo sasa siyo unakopaswa kuwa. Ulipaswa kuwa mbali zaidi ya hapo. Lakini kuna namna umejikwamisha ndiyo ukajikuta hapo.

Sasa mimi rafiki yako nimekataa wewe kubaki hapo ulipo, kwa sababu najua unaweza kwenda mbali zaidi ya hapo.

Na hutaenda mbali kwa kubahatisha, bali kwa kufuata mchakato sahihi unaoweza kukupa matokeo ya uhakika.

Wanafunzi shuleni, hasa kwenye madarasa ya awali, huwa wanapimwa kwa K Tatu; Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Mwanafunzi akishajenga misingi hiyo mitatu, ataweza kujifunza masomo mengine makubwa yanayokuja mbeleni.

Haina maana kumfundisha sayansi mwanafunzi ambaye bado hajajua kusoma wala kuandika. Itakuwa ni kujisumbua tu. Lazima kwanza ya msingi yawepo, ndipo mengine yafuate.

Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wanajipoteza kwenye safari ya mafanikio. Watu wanakazana kutafuta siri zilizofichwa za mafanikio, wakati kuna mambo ya msingi kabisa ambayo bado hawajayakamilisha.

Kwenye mafanikio kuna K Tatu ambazo mtu anapaswa kuzikamilisha ndiyo aweze kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu. Wengi wanapuuza K hizo tatu kwa sababu hazionekani kuwa na umuhimu mkubwa.

Lakini wewe rafiki yangu umechagua kunisikiliza, hivyo sikiliza kwa makini na ufanyie kazi.

K ya kwanza ni Kusoma.

Kama hujapata matokeo unayoyataka, sababu ya kwanza ni kuna vitu ambavyo huvijui. Na kama hutajifunza na kuvijua vitu hivyo, utahangaika sana, ila utaishia kubaki hapo ulipo.

Kwenye safari yako ya mafanikio makubwa, kusoma hakukwepeki. Na huku siyo kusoma kama kwa shule, kusoma ili ujibu na kufaulu mtihani. Huku unasoma ili ujifunze vitu ambavyo huvijui.

Safari ya mafanikio ina vitu vingi sana usivyovijua kiasi kwamba kujifunza linakuwa zoezi la maisha yako yote.

Soma, soma, soma. Kuna vitu vingi bado huvijui, unyenyekevu wa kujifunza ndiyo utakaokufikisha kwenye kile unachotaka.

K ya pili ni Kuandika.

Huenda umefurahi sana uliposikia kuhusu kusoma hapo juu. Na ukaona kama ni kusoma tu nifanikiwe, nipo tayari kusoma sana. Hilo ndiyo kosa limekuwa linafanywa na wasomaji wengi na kukwama kufanikiwa.

Watu wamekuwa wanashirikisha orodha za vitabu vingi ambavyo wamesoma, lakini hakuna hatua wanapiga. Hiyo ni kwa sababu wanasoma ili kumaliza na siyo kuelewa.

Kitakachokusaidia kwenye kusoma siyo ulichosoma, bali kile ulichoelewa. Kwa sababu ulichoelewa ndiyo utakachofanyia kazi na kupata matokeo.

Kujua kama umeelewa ulichosoma, unapaswa kuandika. Unapoandika unatoa kile ambacho umetoka nacho kwenye usomaji.

Unapoandika pia unaweka mkazo kwenye yale uliyojifunza, kiasi kwamba huwezi kusahau. Kuandika kunafanya yale uliyojifunza yaingie ndani yako na kuwa wewe.

Hivyo usiishie tu kusoma, andika pia. Andika wka ajili yako, andika kwa ajili ya wengine na andika kama njia ya kushawishi wengine wakupe unachotaka.

Kadiri unavyoweza kuandika vizuri, ndivyo unavyokuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine kukupa unachotaka.

K ya tatu ni Kufundisha.

Umesoma kujifunza,

Ukaandika ili kuelewa na kueleweka.

Kingine muhimu hapo ni Kufundisha.

Unapofundisha unapata viti viwili,

Cha kwanza ni wewe kubobea kwenye kile ulichojifunza. Huwezi kuwafundisha watu wengine kitu ambacho wewe mwenyewe hujakielewa na kukibobea. Na zaidi, kila unapofundisha, wewe unaelewa zaidi.

Kitu cha pili unachopata kwa kufundisha ni kujenga ushawishi. Wale unaowafundisha wanakuamini na kuwa tayari kukubaliana na wewe.

Hivyo kama unataka ushawishi kwa wafanyakazi wako, wafundishe. Kama unataka ushawishi kwa wateja wako, wafundishe. Hata kwa watu wako wa karibu, wafundishe na watakuwa wanakusikiliza mara zote.

Kufundisha haimaanishi uwe mwalimu au uandae madarasa. Bali pale unapojifunza kitu chochote chenye manufaa, unatafuta mtu ambaye unaweza kumfudnisha na yeye akaelewa na kunufaika.

Hicho ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukifanya na wote wanaohusika wakanufaika.

Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha nimefafanua kwa kina zaidi K hizi Tatu kwa namna ambayo unaweza kuzitumia kujenga mafanikio makubwa.

Isome barua hapa; #BZK022; Soma, Andika, Fundisha. Msingi Wa Ubobezi, Uongozi Na Ushawishi.

Jipime sasa kwenye K hizo tatu, ni vitabu gani unavyosoma sasa? Kwa yale unayojifunza, umekuwa unayaandika wapi? Ni watu gani unaowafundisha na tayari wanakuamini na kukusikiliza?

Jitathmini kwa maswali hayo hapo juu na uchukue hatua sahihi kwenye hizo K tatu ili uweze kujenga mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.