Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Pamoja na watu wengi kutamani sana kupata mafanikio makubwa, yamebaki kuwa kitu kinachotokea kwa wachache. Hilo halisababishwi na mafanikio makubwa kuwa magumu kupatikana. Bali linasababishwa na watu kutokujua njia sahihi za kupata mafanikio makubwa.

Mafanikio makubwa kwenye maisha yetu ni matokeo ya kujaza kwa usahihi ndoo tano ambazo tunazo. Wale waliofanikiwa sana, wamezijaza kabisa ndoo hizo tano. Huku walioshindwa wakiwa hawajajaza ndoo hizo, kwa chache au zote kabisa.

Watu wengi wanahangaika na siri za mafanikio na hawapati matokeo. Wakati kama wangekazana na kujaza ndoo hizi tano, wangepata matokeo ya tofauti.

Kwenye makala hii unakwenda kujifunza ndoo hizo tano za kujaza ili upate mafanikio makubwa.

Ndoo Ya Kwanza; Kujifunza.

Matokeo unayopata kwenye maisha yako yanaamuliwa zaidi na nini unachojua. Unachojua ndiyo kinachokuongoza unachofanya na kukupeleka kwenye mafanikio unayoyataka.

Kujenga mafanikio makubwa na imara, fanya kujifunza kuwa sehemu ya kudumu ya maisha yako. Kamwe usijione kama tayari umeshajua kila kitu. Badala yake kuwa tayari kujifunza kila wakati na kuwa tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu.

Ndoo Ya Pili; Ujuzi.

Huwa kuna tofauti kubwa sana kati ya kujifunza na kuburudika, tofauti ambayo wengi wamekuwa hawaielewi na hivyo kujikuta wanabaki pale pale licha ya kuona wanajifunza.

Ndoo ya pili ya kujaza ni ujuzi, ambao unatokana na kufanyia kazi yale uliyojifunza. Ujuzi ni maarifa yaliyowekwa kwenye vitendo na hivyo kubadili namna ambavyo mtu anafanya mambo.

Wajibu wako mkubwa ni kutumia maarifa unayopata kuboresha vile unavyofanya. Unapaswa kujijengea ujuzi wa thamani kubwa kwenye safari yako ya mafanikio. Ujifunze kufanya vitu ambavyo vinakupa matokeo makubwa kuliko unayopata sasa.

Ndoo Ya Tatu; Mtandao.

Unaweza kujifunza na ukajua mengi, na ukajenga ujuzi unaokuwezesha kutoa thamani kubwa, lakini bado usipate mafanikio makubwa. Hilo litatokea kama utashindwa kujenga mtandao sahihi unaoweza kukupa mafanikio unayotaka.

Baada ya kuwa na MAARIFA na UJUZI, kinachofuata ni kujenga MTANDAO sahihi kwa ajili ya mafanikio yako. Mtandao sahihi ni watu wanaokujua na kujua thamani unayoweza kutoa na ikawanufaisha. Hili ni lazima ulijenge wewe mwenyewe, ili uweze kupata matokeo unayoyataka.

Rafiki, hapa tumeziangalia ndoo tatu kati ya tano. Ndoo hizi tatu zinajenga msingi imara wa kukuwezesha kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Kuna ndoo nyingine mbili za ziada, ambazo zinafanya mafanikio yoyote unayoyapata yaweze kudumu kwa muda mrefu. Bila ndoo hizo mbili, chochote utakachopata kwa ndoo tatu za mwanzo kitapotea haraka sana.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekueleza kwa kina barua hizo mbili za ziada na jinsi ya kuzitumia kudumisha mafanikio unayoyapata. Hizo siyo ndoo za kukosa kama kweli umedhamiria kujijengea mafanikio makubwa na yanayodumu.

Karibu usome barua hiyo hapa; #BZK021; Tatizo Lako Ni Unajenga Msingi Wa Mafanikio Kwenye Mchanga.

Umehangaika sana na siri nyingi za mafanikio. Umekimbizana na kila mbinu ya mafanikio uliyoweza kujifunza. Lakini mara zote unajikuta umerudi hapo ulipo.

Sasa ni wakati wa kubadili hilo, badala ya kukimbiza upepo ambao huwezi kuukamata, jaza ndoo ulizonazo. Kila ndoo tupu uliyonayo ndiyo inakugharimu mafanikio unayoyataka.

Kwa kujaza ndoo zako kwa ukamilifu, utaweza kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu kwa muda mrefu. Hakuna unachokosa sasa kinachopelekea usifanikiwe. Unachohitaji ni wewe ujaze ndoo zako tano na upate kila unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.