Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Kama unapambana sana kufanikiwa lakini huyaoni mafanikio kama ulivyotarajia, siyo kwamba mafanikio hayawezekani kwako. Bali hujatumia vizuri rasilimali za msingi ulizonazo, ambazo zinaweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka.
Unaweza kudhani hufanikiwi kwa sababu kuna rasilimali umezikosa. Kama ambavyo huwa ni maarufu watu kusema wamekosa mtaji au vitu vingine. Lakini ukweli ni siyo ukosefu wa rasilimali unaokukwamisha, bali ni kushindwa kutumia vizuri rasilimali ambazo tayari unazo.
Kama umehangaika muda mrefu bila kufanikiwa, hilo linaenda kukoma leo kwa sababu utajifunza kutumia rasilimali tatu muhimu ulizonazo kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Rasilimali Ya Kwanza Ni Hamasa.
Safari ya mafanikio ni ngumu na yenye changamoto na vikwazo vingi. Wengi wanaianza safari hiyo, lakini wanakwama na kuishia njiani.
Wengi sana wangeweza kupata wanachotaka, kama wangeendelea na safari waliyoianza kwa muda mrefu zaidi. Lakini wengi wanaishia njiani kabla hawajaona matokeo waliyotarajia.
Kinachowakwamisha watu hao ni kushindwa kutumia vizuri rasilimali ya hamasa iliyo ndani yao. Mafanikio yanataka mtu kutumia vizuri hamasa ya ndani ili kuendelea na safari ya kile ambacho amechagua.
Bila hamasa ya ndani, vikwazo na changamoto vinamchosha mtu na kumfanya akate tamaa kwa kuona anachotaka hakiwezekani. Lakini kwa kuwa kutumia hamasa ya ndani, mtu anaweza kuvuka magumu hayo na kuendelea.
Siyo kwamba kuna watu wana hamasa na wengine hawana. Watu wote wana hamasa, tofauti inakuja kwenye kuijua na kuitumia.
Ukitaka kuthibitisha hilo, mchukue mtu unayemwona ni mvivu kabisa na jaribu kumzamisha kwenye maji. Mtu huyo atapambana kwa kila namna asizame, kwa sababu anataka kuendelea kuwa hai. Hiyo ni ishara ya hamasa kubwa iliyo ndani ya kila mtu.
Tatizo ni watu wanakimbilia kufanya mambo ya kuiga kwa nje, ambayo hayatokani na hamasa zao za ndani. Hivyo wanakuwa wanategemea kupata hamasa na msukumo wa nje, ambao huchoka haraka pale mambo yanapokuwa magumu.
Ukitaka kujua na kutumia vizuri rasilimali hii ya hamasa, fanya kile ambacho una msukumo mkubwa wa kukifanya ndani yako. Usifanye chochote cha kuiga kwa nje, bali sikiliza sauti yako ya ndani na fanya hicho.
Mara nyingi kile unachosukumwa kukifanya kwa ndani ni tofauti na mambo yaliyozoeleka na wengi. Wewe usiache kwa sababu wengi hawakuelewi, badala yake endelea kufanya kwa msimamo bila kuacha, hapo ndipo mafanikio yako makubwa yalipo.
Rasilimali Ya Pili Ni Jasho.
Nikikuuliza sasa hivi kwa nini hujapiga hatua ambazo umepanga, kwa nini hujaanza au hujakuza biashara, utanipa jibu la rasilimali ulizokosa. Utaniambi huna mtaji, huna koneksheni na mengine ya aina hiyo.
Kitu ambacho hutaniambia ni unatumiaje rasilimali kubwa uliyonayo, ambayo ni jasho. Rasilimali jasho ni kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Kufanya kazi kwa ukubwa na kwa muda mrefu bila kuchoka. Hiyo ni rasilimali ambayo inaweza kumfikisha yeyote kwenye kile anachotaka.
Unaweza kukosa vitu vingi unavyovihitaji ili ufanikiwe, lakini kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni kitu ambacho unacho. Ukiweza kukitumia, lazima utatoka hapo ulipo sasa.
Kubali kuweka kazi kubwa kwenye chochote unachofanya na utapata matokeo makubwa kuliko unavyopata sasa.
Rasilimali Ya Tatu Ni Hatari.
Kuchukua hatua za hatari ni rasilimali nyingine muhimu ambayo watu wamekuwa wanashindwa kuitumia. Watu wamekuwa wanafanya yale waliyozoea kufanya, kwa sababu yanawapa matokeo ya uhakika.
Lakini matokeo ya uhakika hayaleti mafanikio makubwa. Mafanikio makubwa yanayotaka na kujaribu vitu vipya, ambavyo pia ni hatari. Kuwa tayari kufanya vitu hatari, ambavyo vinaweza kushindwa ndiyo kunaleta matokeo ambayo mtu hujawahi kuyapata.
Iko ndani yako kufanya vitu ambavyo hujazoea kufanya. Unachohitaji ni ujasiri na kuendelea kujifunza kupitia matokeo unayopata. Kwa kuendelea kuwa bora zaidi, utaweza kufanya mapya na makubwa zaidi.
Rafiki, kwenye #BaruaYaKocha, nimeshirikisha mfano wa Trilionea Elon Musk, ambaye alimpima mtu aliyeanza naye biashara kwa rasilimali hizo tatu. Kupitia kipimo hicho, mtu huyo hakupata utajiri mkubwa kwa sababu alikosa rasilimali moja muhimu. Isome barua hiyo kujua na kuhakikisha huikosi rasilimali hiyo muhimu.
Isome barua hapa; #BZK020; Hamasa, Jasho Na Hatari – Mapacha Watatu Wasioweza Kutenganishwa Kwenye Mafanikio Makubwa.
Rafiki, ninachoamini ni kwamba, unaweza kupiga hatua kubwa zaidi ya hapo ulipo sasa. Unachohitaji ni kutumia hamasa yako ya ndani, kuweka kazi kwa juhudi kubwa na kujaribu mambo mapya ambayo hujawahi kuyafanya.
Je utakuwa tayari kufanya hayo matatu ili upige hatua kubwa?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.