Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa nasema, watu wanazo sababu tayari, kinachosubiriwa ni matokeo tu. Ukitaka kudhihirisha hilo, angalia kunapokuwa na ushindani wa pande mbili, iwe ni kwenye michezo, biashara, siasa na mengine.
Kama kuna pande A na B zinazoshindana, upande A ukishinda, utakuwa na sababu kwa nini umeshinda. Kadhalika upande huo huo ukishindwa, utakuwa na sababu kwa nini umeshindwa.
Huwa haitokei upande ulioshindwa ukasema haujui kwa nini umeshindwa. Badala yake sababu zinakuwepo, na hazitokei baada ya kushindwa, bali ni sababu zilizokuwepo hata kabla.
Timu mbili zinaingia uwanjani kucheza, timu A inashinda na kusema ilikuwa na kikosi kizuri. Timu B inashindwa na kusema haikuwa na muda wa kutosha wa kufanya mazoezi.
Hiyo timu iliyoshindwa, iliingia uwanjani ikijua kabisa kwamba haikuwa na muda wa kutosha wa kufanya mazoezi. Kama ingetokea timu hiyo ikashinda, usingeisikia hiyo sababu. Badala yake ingetolewa sababu nyingine tofauti kabisa ya kwa nini ushindi umepatikana.

Hilo linatufundisha nini? Somo kubwa hapo ni kwamba, kushinda au kushindwa ni maamuzi ambayo mtu anakuwa nayo tangu awali. Kama umeshindwa, ni kwa sababu tayari ulishakubali kushindwa, hata kabla hujaingia kwenye ushindani.
Naweza kusema, wengi wanashinda kwa kubahatisha, ila wanashindwa kwa makusudi. Japo wengi wamekuwa wanafikiria kinyume na hilo, wanaona kushindwa ni bahati mbaya. Lakini tunapoangalia jinsi watu wanavyokubali kushindwa, tunaona dhahiri ushindi ambao wengi wanaupata ni wa kubahatisha.
Kwa mtu ambaye anashindwa na anaona ni sawa tu, hakuna namna anaweza kushinda kama siyo kwa kubahatisha. Na ndiyo maana ushindi wa wengi huwa haudumu na wala hawawezi kuurudia.
Njia pekee ya kupata ushindi kwa makusudi na kwa uhakika, ni kukataa kata kata kushindwa. Ndiyo, unakataa kabisa kushindwa. Hakuna namna unakubali hali ya kushindwa kwenye chochote unachofanya.
Hali hiyo ya kukataa kushindwa ndiyo inayokusukuma kuendelea kupambana bila ya kujali ni mambo gani unakabiliana nayo. Mapambano makubwa unayoyafanya ndiyo yanayokupa ushindi.
Na hata ikitokea hujapata matokeo uliyotegemea, huhesabii hilo kama kushindwa. Badala yake unachukulia ni mrejesho wa kuhitaji kuboresha zaidi kile unachofanya.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekuonyesha jinsi unavyohitaji kitu kimoja muhimu ili usikubali kabisa kushindwa. Kitu hicho ni TUMAINI. Kinachofanya watu wakubali kushindwa ni kukosa matumaini.
Hiyo ndiyo sababu ya mimi rafiki na Kocha wako kujipa cheo cha MUUZA MATUMAINI. Kwa sababu najua tumaini ndiyo kitu unachokihitaji sana kwenye safari yako ya mafanikio. Unaweza kuwa na rasilimali zote unazohitaji, ila ukikosa tumaini, huwezi kupata ushindi.
Kwenye barua hiyo nimeshirikisha utafiti uliofanywa kwa kutumia panya. Panya waliwekwa kwenye chupa ya maji ambayo hawawezi kutoka na ndani ya wakika 15 wakawa wamezama na kufa.
Lakini jaribio hilo liliporudiwa, kwa panya kuokolewa kabla hawajafa na kurudishwa tena kwenye maji, ilichukua masaa 60 kwa panya kuzama maji na kufa.
Unajua tofauti ya zoezi la kwanza la panya kuwekwa kwenye maji na kuachwa mpaka wafe na zoezi la pili la panya kuokolewa kabla ya kufa na kurudishwa tena ni nini?
Jibu ni TUMAINI. Panya waliowekwa mara moja, walipambana kujiokoa, lakini hawakuona wakifanikiwa, hilo lilipelekea wakate tamaa na kufa. Panya waliookolewa kabla ya kufa, walijifunza kwamba ukombozi unakuja, hilo liliwapa tumaini la kuendelea kupambana zaidi. Na hiyo ndiyo ilisababisha waweze kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Hicho ndiyo kinachohitajika kwenye safari yako ya mafanikio. Unapaswa kuwa na tumaini kubwa kwamba ushindi upo, ni wewe kuupambania. Hata pale mambo yanapokuwa magumu kiasi gani, usipoteze kabisa hilo tumaini.
Najua swali lako litakuwa ni unajengaje tumaini imara kiasi hicho? Kwenye barua ya kocha nimekushirikisha njia tano za kujenga tumaini ambalo haliwezi kutetereshwa na chochote. Zijue na uzitumie njia hizo tano kupata mafanikio ya uhakika.
Isome barua hiyo hapa; #BZK019; Kwa Nini Kamwe Siwezi Kushindwa. Tumaini La Uhakika Kwako Kufanikiwa
Rafiki, kama ulikuwa hujui, sasa unajua. Kushindwa ni kuchagua, na njia ya kawaida kwenye maisha ni ya kushindwa. Kama unataka ushindi, ni lazima ubadili maisha yako na kuchagua ushindi.
Hilo linaanza na tumaini lisiloyumbishwa kwamba utashinda. Kisha kufanya mambo yako yote ukijua ushindi ni kitu cha uhakika kwako. Usiruhusu kwa sababu au namna yoyote ile kukubali kushindwa.
Na pale mambo yanapokuwa magumu kabisa, usisahau mimi rafiki na kocha wako, pia ni mtu ninayekuuzia matumaini. Karibu tuambatane pamoja kwenye safari hii ya kujenga mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.