Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Tuna rasilimali nyingi kwenye maisha yetu, ambazo tunazitumia kujenga mafanikio makubwa tunayoyataka.

Katika rasilimali hizo, mbili ni za muhimu sana, lakini pia zina ukomo. Rasilimali hizo ni muda, ambao tuna masaa 24 tu kwa siku na nguvu ambazo zipo kwa kiasi tu kila siku.

Ili tuweze kujenga mafanikio makubwa kadiri tunavyotaka, ni lazima tuweze kudhibiti na kutumia vizuri rasilimali hizo muhimu.

Lakini cha kushangaza, huwa tunachagua kupoteza rasilimali hizo kwa kuhangaika na mambo yasiyo na tija.

Huwa kuna vitu ambavyo tumezoea kufanya, lakini ni vitu vinavyopoteza sana rasilimali zetu, kwa sababu havina mchango kabisa kwenye kile tunachotaka kujenga.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeshirikisha mambo sita ambayo unayafanya kila mara na yanakuwa upotevu wa rasilimali zako.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha moja ambalo unaweza usilidhanie sana, lakini linakukwamisha.

Acha Kujieleza Sana.

Kama kuna kitu unataka, au hutaki, unapaswa kufanya maamuzi yako na kuyatekeleza. Huwajibiki kujieleza sana kwa wengine ndiyo uweze kufanya maamuzi unayotaka. Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda kwenye kuelezea maamuzi waliyofanya, kitu ambacho hakileti tija yoyote kwao wala kwa wanaowaelezea.

Tatizo la kujieleza sana ni kwamba, haibadili chochote kwa wale unaojieleza kwao. Kwa wale ambao wanakubaliana na wewe, hawahitaji maelezo yako. Tayari wanajua unachofanya ni sahihi na wanakuunga mkono kwenye hilo.

Kwa wale ambao hawakubaliani na wewe, maelezo yako hayatabadili chochote kwao. Zaidi yataibua maswali na kutafsiriwa tofauti na unavyomaanisha. Tayari watu hao wameshachagua kwamba ulichoamua au unachofanya siyo sahihi, hakuna kiasi cha kujieleza ambacho kitabadili hilo.

Hili ni gumu kueleweka kwa sababu huwa tunaona tunawajibika kuwaeleza watu sababu ya yote tunayoamua kufanya, lakini kujieleza hakujawahi kufanya kazi.

Sehemu ambayo hili linahitajika zaidi ni pale unapowapa wengine jibu la HAPANA. Pale watu wanapokutaka ufanye kitu ambacho hutaki kufanya, unaona unawajibika kuwaeleza kwa nini hutafanya. Na ukishafanya hivyo tu, unafungua mjadala ambao kwa sehemu kubwa utaishia kushindwa.

Kama mtu amekuomba au kukutaka ufanye kitu fulani ambacho hupo tayari kufanya, unatakiwa tu kujibu HAPANA au HAITAWEZEKANA. Jibu hilo linajitosheleza kabisa na halihitaji maelezo mengine mengi.

Ukianza tu kueleza sababu za hapana yako, unafungua uwanja wa mjadala, ambao utaishia wewe kubadili maamuzi yako. Watu watatafuta udhaifu wako kwenye maelezo yako na kuutumia kubadili maamuzi yako.

Kwa kifupi, kadiri unavyojieleza sana ndivyo unavyowapa watu maeneo ya kukushinda kwenye kile wanachotaka na wewe haupo tayari kwa ajili hiyo. Epuka kupoteza nguvu na muda kwenye maelezo, ambayo yatapelekea urudi kwenye kile ambacho haupo tayari kufanya.

Fanya maamuzi, yasimamie na songa mbele. Hakuna kiwango cha kujieleza kitakachobadili namna watu wamechukulia maamuzi yako. Wakukuelewa wameshakuelewa na wakutokukuelewa wameshakaa upande wako. Maelezo yako hayatabadili upande wowote kati ya hizo mbili.

Rafiki, hiki ni kitu kimoja ambacho kwa mazoea huwezi kuona kikikukwamisha. Lakini unapokuja kujitathmini na kuona muda na nguvu unazopeleka kwenye kitu hicho na matokeo unayopata, unauona upotevu wazi wazi.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza mengine unayopaswa kuwa na tahadhari nayo. Ni barua ya kusoma ili uweze kulinda rasilimali zako na kuzitumia kwenye mambo yenye tija.

Isome barua hiyo hapa; #BZK018; Okoa Muda Na Nguvu Unazopoteza Bure Zikusaidie Kwenye Mafanikio.

Rafiki, una mambo mengi ya kufanya na muda wako ni mchache. Usipoteze muda huo wa thamani na nguvu zako kuhangaika na mambo ambayo hayana mchango kabisa kwenye mafanikio unayoyataka.

Chagua nini unataka, kisha peleka rasilimali zako zote kwenye kutimiza hicho unachotaka. Hivyo ndivyo unavyoweza kuyabadili maisha yako kadiri unavyotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.