Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Ubongo wetu sisi binadamu umeumbwa kwa kazi kubwa mbili.

Moja ni kuhakikisha tuko salama, ndiyo maana huwa unatuonyesha hatari za kila aina.

Mbili ni kuhakikisha tunapata raha, ndiyo maana huwa tunajisikia vizuri pale tunapofanya baadhi ya vitu.

Ubongo umeumbwa hivyo kuhakikisha tunaendelea kuwa hai, kwa kuepuka hatari zinazoweza kukatisha uhai wetu na kuzingatia mambo yanayotufanya tuendelee kuwa hai.

Chakula ni kitamu, kwa sababu tunahitaji kula ndiyo tuendelee kuwa hai. Kufanya mapenzi kuna raha kwa sababu ni kupitia hilo ndiyo tunazaliana.

Pamoja na nia hiyo njema ya ubongo, siyo mara zote unafanya mambo yenye tija kwetu, hasa inapokuja kwenye mafanikio makubwa.

Tunaweza kusema kwamba ubongo hauna kazi sana na mafanikio makubwa, wenyewe una kazi na kuhakikisha tunakuwa hai. Ndiyo maana hata viumbe ambao hawana akili kama zetu binadamu, wanaweza kuendelea kuwa hai.

Unapotaka mafanikio makubwa, hapo jua kabisa kwamba unatoka nje ya mfumo wa kawaida wa ubongo. Kama hutachukua hatua zisizo za kawaida, utakwama kupata mafanikio unayoyataka.

Moja ya vitu unavyopaswa kuachana navyo ili uweze kujenga mafanikio makubwa unayoyataka, ni raha rahisi kupatikana.

Raha rahisi kupatikana ni vitu unavyofanya na kujisikia raha kuvifanya, lakini havina mchango wowote kwenye hatua kubwa unazotaka kupiga.

Unapofanya vitu hivyo, unajisikia vizuri, lakini vinakuwa havina mchango kabisa kwenye mafanikio makubwa unayotaka kujenga.

Wengi sana wamekwama kufanikiwa kwa sababu wamepotezwa na raha hizo rahisi. Kama unataka kujenga mafanikio makubwa, ni lazima uhakikishe huhadaiwi na raha ambazo unapata kirahisi.

Kwenye #BaruaYaKocha, nimekuonyesha kwa kina jinsi mtego huu wa kupata raha rahisi umekukwamisha hapo ulipo sasa. Na moja ya vitu nilivyoeleza vizuri ni kuhusu raha ya kujifunza inavyokukwamisha kufanikiwa.

Unaweza ukaona kujifunza kuna manufaa kwako, lakini kama huchukui hatua, unajipa raha bila manufaa. Hivi ndivyo nilivyoandika kwenye #BaruaYaKocha;

Raha Ya Kujifunza Inavyokukwamisha.

Ni rahisi kuona mitandao na michezo ya kielektroniki kama raha za haraka zinazotukwamisha. Na baadhi ya watu wanachukua hatua ya kuepuka raha hizo. Wapo wanaotoa kabisa mitandao ya kijamii kwenye simu zao. Wengine wanaenda mbali na kujitoa kabisa kwenye mitandao hiyo.

Pamoja na kuondokana na hizo raha rahisi zinazowakwamisha, bado watu hawapigi hatua kubwa kama walivyokuwa wanategemea. Na sababu kubwa inarudi kwenye raha rahisi, lakini inayokuwa imejificha zaidi.

Moja ya raha ambayo inawahadaa wengi kwenye mafanikio ni kujifunza. Inapokuja kwenye kufanya mambo mapya na makubwa, mtu anaona kuna vitu hajui. Hivyo anachukua hatua ya kujifunza. Anapojifunza vitu vipya, anapata raha.

Akianza kufanya, anakutana na ugumu na changamoto. Hilo linamrudisha tena kujifunza, kwa sababu anaona kuna vitu bado hajajua. Anapojifunza, anasikia raha. Sasa niambie hapo, kipi ambacho mtu atafanya zaidi? Uko sahihi, kila wakati atakuwa anajifunza. Kila anapokutana na ugumu, anarudi tena kujifunza. Kwa sababu kujifunza kuna raha ya haraka.

Na hiyo ya kujifunza imeenda mbali zaidi, kiasi cha watu kuhesabu mafanikio kwa waliyojifunza. Kumekuwa na utaratibu wa watu kushirikisha vitabu ambavyo wamesoma. Hilo linakuwa kwa nia njema ya kuhamasisha wengine kujifunza pia. Lakini wengi wamegeuza hilo kuwa kipimo cha mafanikio. Kwamba ukisoma vitabu vingi, basi umefanikiwa.

Kuna njia nyingine za kujifunza ambazo zimetawala akili za wengi kwa sasa na zimekuwa ni hasara kuliko hata kutokujifunza kabisa. Kumekuwa na wimbi la video fupi za sekunde 30 mpaka 60, ambazo zinanasa sana umakini na kufanya watu wajisikie vizuri. Hata kama utaangalia video 100 za sekunde 30 kila moja, bado hutakuwa umejifunza kama aliyeangalia video moja ya dakika 30 au kusoma kitabu kimoja.

Raha ya kujifunza ni mtego mkali sana, ambao siyo rahisi kuujua na kujinasua. Kwa sababu kila unapojifunza unaona kabisa kwamba unapiga hatua. Lakini ukweli ni kujifunza kwingi ni sawa na punyeto ya akili (mental masturbation), unasikia raha, lakini hakuna kikubwa unachokuwa umekamilisha.

Kama unapata raha zaidi kwenye kujifunza na kila wakati unajifunza bila kuchukua hatua, kujifunza kunakuwa kikwazo kwako kufanikiwa.

Kuna raha nyingine ambazo zinakukwamisha, kwenye barua nimeeleza kwa kina zaidi. Pia nimekupa hatua za kuchukua ili raha zisiendelee kuwa kikwazo kwako. Isome barua kamili ili usikwamishwe na hizo raha rahisi.

Isome barua hapa; #BZK017; Raha Unazopata Kwa Urahisi Ndiyo Zinazokukwamisha Kupata Mafanikio Makubwa.

Rafiki, kama ambavyo umeona hapa, wakati mwingine unajizuia kufanikiwa bila hata ya wewe mwenyewe kujua. Unaona unafurahia tu maisha, kumbe huko kufurahia ndiyo kunakukwamisha.

Naamini somo hili limefungua kitu cha tofauti kwako, wajibu wako ni kuchukua hatua ili ubadili maisha yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.