Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kila mtu anayataka mafanikio, kwa namna anavyoeleza mafanikio kwake yeye mwenyewe. Pamoja na kuhangaika na siri na mbinu nyingi za mafanikio, bado wanaofanikiwa kweli ni wachache sana.

Hiyo siyo kwa sababu wachache hao ndiyo wenye bahati ya kufanikiwa, au kwamba wengi hawana uwezo wa kufanikiwa. Bali ni kwa sababu wengi wanahangaika na mafanikio ka namna isiyokuwa sahihi. Vile ambavyo wengi wanayachukulia mafanikio siyo yanavyopaswa kuchukuliwa.

Wengi wamekuwa wanachukulia mafanikio kama mwisho wa safari, ambapo wakifika hapo ndiyo wamefanikiwa. Wanaona kila wanachofanya ni kujiandaa kwenda kuyapata hayo mafanikio. Na matokeo yake wamekuwa wana ahirisha kufanya mambo ya msingi ambayo ndiyo yangewapa mafanikio wanayotaka.

Hakuna Siku Moja Utakayoyafikia Mafanikio, Mafanikio Ni Kila Siku.

Dhana ya kwamba upo kwenye safari ya mafanikio na hayo mafanikio yako kwenye mwisho wa safari imewakwamisha wengi sana kufanikiwa. Ukweli ni kwamba, hakuna siku moja ambayo utayafikia mafanikio, bali mafanikio ni jinsi unavyoiishi kila siku.

Hakuna siku moja ambayo ndiyo utapata mafanikio, mafanikio ni mkusanyiko wa siku ambazo umeziishi kimafanikio. Kwa maana hiyo basi, mafanikio ni siku moja tu, siku ambayo umeiishi kimafanikio kwa asilimia 100.

Unaona sasa jinsi ambavyo mafanikio ni rahisi na yanawezekana kwa kila mtu. Kwa sababu kinachohitajika ni kuiishi kila siku yako kimafanikio. Halafu kurudia kuishi hivyo kila siku kwa maisha yako yote. Kwa njia hiyo, husubiri siku moja ndiyo uyapate mafanikio, bali unafanikiwa kila siku.

Mafanikio Ni Leo, Kila Siku.

Kama ni rahisi hivyo, kwamba mafanikio ni mkusanyiko wa siku ambazo mtu ameziishi kimafanikio, kwa nini wengi wanashindwa kufanya hivyo? Unaweza kushangaa, kwamba kitu rahisi hivyo watu hawakijui na kukifanya?

Jibu ni kesho. Kesho imekuwa kikwazo kwa watu wengi kufanikiwa kwa namna wanavyotaka. Wanajua kabisa nini wanapaswa kufanya ili wafanikiwe, lakini inapofika wakati wa kufanya, wanajiambia watafanya kesho.

Kwa kifupi kuahirisha mafanikio kwa kuona bado hujawa tayari kuanza, au kuanza na kutokuendelea kwa msimamo imekuwa kikwazo kwa wengi kupata mafanikio ambayo yako ndani ya uwezo wao.

Tunaposema mafanikio ni kila siku, maana yake ni mtu kuishi kimafanikio kwenye kila siku ya maisha yake, bila kuacha au kufanya kwa upungufu. Kila siku unayoacha kuishi kimafanikio, unakuwa umerudi nyuma sana, kiasi kwamba unapokuja kuishi kimafanikio huendelezi ulikokuwa umefikia, bali unalipa deni unalokuwa umetengeneza.

Ni sawa na kupiga hatua mbili mbele na kurudi hatua tano nyuma, ukipiga hatua nyingine mbili hujasogea mbele, bali bado upo nyuma zaidi.

Na siyo tu kuacha kabisa, hata kuweka juhudi kwa kiwango cha chini ni kuharibu siku na kujirudisha nyuma. Siku za mafanikio hazikopwi. Huwezi kuweka juhudi kwa asilimia 80 leo na kusema kesho utalipa kwa kuweka asilimia 120. Mafanikio ni siku moja, unaposhindwa kuitumia kikamilifu unaipoteza kabisa na huwezi kuipata tena.

Unaona sasa kwa nini pamoja na urahisi wa mafanikio, bado wengi sana wanakwama. Kwa sababu imekuwa mazoea kwa watu wengi kuahirisha mambo ambayo wangeweza kuyatekeleza, kwa sababu tu wanaona kesho watafanya. Hivi kama umeshindwa kufanya kitu leo, nini kinakuaminisha kesho unaweza kukifanya?

Ni kupeleka mambo kesho ndiyo kumewakwamisha wengi sana kupata mafanikio makubwa ambayo yapo ndani ya uwezo wao. Ni kushindwa kuishi kila siku kimafanikio na kwa kuweka juhudi kwa asilimia 100 ndiyo kumewafanya wengi kujikuta wanahangaika sana ila hawapigi hatua.

Watu wamekuwa wanateseka na madeni ya fedha, ila kuna mateso ya madeni ya muda ambayo wanayatumikia ila hawajajua. Kadiri unavyochelewa kuanza kufanya, au kufanya na kuahirisha au kufanya kwa viwango vya chini, ndivyo unavyotengeneza deni la muda. Ubaya wa deni la muda ni huwezi kulilipa ukamaliza, kwa sababu muda ukishapotea huwezi kuupata tena.

Ni changamoto hiyo kubwa iliyopo kwenye kuiishi kila siku kimafanikio ndiyo imefanya barua hii ije kwako siku ya leo. Siyo kwa lengo la kukufundisha, bali kukukumbusha dhana hii ambayo ni muhimu sana. Na kukuonyesha kwa kona nyingine hilo deni la muda ambalo unapaswa kuacha kulitengeneza kama unataka mafanikio makubwa.

#BaruaYaKocha ina mambo matano unayopaswa kuyafanyia kazi ili kuifanya kila siku kuwa siku ya mafanikio na kupata mafanikio makubwa kwa uhakika kwenye maisha yako.

Soma barua hiyo hapa; #BZK068; Mafanikio Ni Siku Moja Tu, Leo