Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Propaganda ni kitu kinachochukuliwa hasi, kwa sababu ya jinsi ambavyo imekuwa inatumika. Propaganda imetumika sana kwenye siasa na vita kwa lengo la kuwahadaa watu na hilo limepelekea wengi kuchukia propaganda.
Lakini unapoangalia kwa kina, unakuja kugundua propaganda ni kitu chenye nguvu, ambacho watu wamekitumia vibaya. Yaani propaganda kama yenyewe siyo mbaya, ni zana tu. Lakini jinsi watu wanavyotumia propaganda ndiyo wanaweza kuleta matokeo mabaya.
Propaganda imetumika kwenye mambo mengi mazuri, bila ya kuitwa hivyo au watu kujua kwamba kinachoendelea ni propaganda. Elimu, michezo, sanaa na mambo mengine ya kijamii, huwa yanaweza kutumika kupenyeza kitu fulani kinachopaswa kukubalika na wengi.
Propaganda ndiyo njia pekee ya watu kukubali mabadiliko kwa haraka. Kwa asili sisi binadamu huwa hatupendi mabadiliko. Ndiyo maana mambo mengi mapya huwa yanapingwa na kukataliwa. Pale mabadiliko yanapohitajika kwa haraka, tena kwa watu wengi, lazima propaganda itumike.
Na propaganda ni mawazo tu ambayo yanarudiwa rudiwa kwa muda mrefu, ambayo yanagusa na kunasa hisia. Mwanzo watu wanaweza kuyapuuza, lakini kwa namna yanavyorudiwa ndivyo yanavyozoeleka na kuonekana kitu cha kawaida.

Kwa maana hiyo, hata kampeni za masoko ni propaganda. Fikiria umekuja na bidhaa au huduma mpya na watu hawaijui kabisa. Ni lazima ufanye kampeni ya kuwafanya watu wajue ipo na watake kuipata. Mwanzo wengi watapinga na kupuuza. Lakini wanapoona kwa kurudia rudia, wanazoea na kuvutiwa kuipata.
Ni nguvu hiyo ya propaganda ndiyo nataka tuitumie kwenye safari yetu ya ushindi na mafanikio makubwa kwenye maisha. Kuna mawazo ya msingi sana tunayopaswa kuyakubali kifikra na kuyaamini kiroho ndiyo yaweze kutokea kwenye maisha yetu.
Mawazo hayo hayawezi kuingia tu kawaida, lazima tuyafanye kama propaganda binafsi kwetu. Lazima tujenge itikadi kali kwenye mawazo hayo, kwa namna ambayo tutayakubali na kuyaamini.
Na kiuhalisia, bila propaganda binafsi, ni vigumu sana kupata ushindi na mafanikio makubwa. Kwa sababu kuna propaganda nyingi za nje ambazo unasukumiwa ili uone unahitaji kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kwako.
Wanaokuzunguka, jamii, dini, taifa na taasisi nyingine ambazo zinataka kukutawala, zinataka wewe uwe na maisha ya kawaida, ili ufae kutawaliwa. Hazitaki uwe na mafanikio makubwa sana, kwa sababu hutaweza kutawaliwa. Wote hao wanataka kukuona ukiishi, lakini siyo ukiwa huru kabisa.
Japo hilo hakuna atakayekuambia wazi wazi, lakini propaganda kali sana zinaendelea kuhakikisha unabaki kwenye hali ya utegemezi na kutawaliwa. Kama unataka ushindi na mafanikio makubwa, unahitaji kuwa na propaganda binafsi ambayo ni kali kuliko za wanaotaka kukutumia.
Barua hii ni mwongozo kwako kujenga na kuimarisha propaganda binafsi, ambayo itakupa ushindi mkubwa na uhuru wa kuyaishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe mwenyewe.
1. Tayari Mimi Ni Mshindi.
Propaganda iliyopo kwenye jamii ni kwamba wewe huwezi kupata ushindi na mafanikio makubwa unayoyataka. Unapewa ushahidi wa familia uliyotokea, ambapo hakuna aliyewahi kupata mafanikio hayo. Unakumbushwa jinsi ulivyofeli shule au makosa uliyofanya kwenye maisha. Jamii inakazana kukupa ushahidi mwingi sana wa kwa nini huwezi kufanikiwa.
Unahitaji propaganda sahihi kuvuka hiyo, na propaganda hiyo ni; ‘TAYARI MIMI NI MSHINDI’. Hii ni propaganda ya kujiambia kwa kurudia rudia kila wakati mpaka iwe kitu ambacho unakiamini bila ya wasiwasi wowote. Na ushahidi wa propaganda hiyo ni kitendo cha kuwa hai mpaka leo. Ni watu wangapi wangekuwa tayari kulipa kiasi kikubwa sana cha fedha ili tu wawe hai leo, lakini hawapo hai? Kitendo cha wewe kuwa hai, ni ushindi mkubwa sana. Kinachofuata hapo ni wewe kutumia ushindi wa uhai kupata ushindi mwingine.
Haijalishi unapitia nini kwenye maisha, haijalishi unapewa ushahidi mkubwa kiasi gani kwamba huwezi kufanikiwa, usiache kuamini kwamba wewe ni mshindi. Na siyo tu kuamini, bali hilo liwe sehemu ya maisha yako. Uwe na itikadi kali mno kuhusu ushindi wako. Uwe msumbufu mno kwa wale wanaokuambia kinyume na hiyo itikadi yako.
Ushindi na mafanikio makubwa kwenye maisha ni zao la propaganda binafsi ya kuwa tayari wewe ni mshindi. Huhitaji chochote cha ziada kwenye kujenga hilo, ni kuifanya kuwa propaganda binafsi na kuiimba wakati wote.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha propaganda nyingine 4 muhimu sana unazopaswa kujijengea ili kuzima nguvu ya propaganda za kijamii zinazokukwamisha kufanikiwa.
Soma barua hiyo hapa; #BZK069; Propaganda Binafsi Zitakazokupa Mafanikio Makubwa