Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu aliyeweza kujenga mafanikio makubwa, ana watu wengi wanaomchukia kuliko wale wanaompenda.

Hilo halipo hivyo kwa bahati mbaya, ni sehemu ya mafanikio makubwa.

Wanaofanikiwa sana huwa wanachukiwa na watu wengi, kwa sababu kinachowafanya wafanikiwe ni ambacho hakieleweki na hao wengi.

Kila mtu aliyeshindwa ana maoni na ushauri mzuri sana kwa wale waliofanikiwa. Walioshindwa huwa wanawaona waliofanikiwa hawapo sahihi kwenye mengi wanayofanya.

Lakini kinachoshangaza ni jinsi hao wanaojiona wako sahihi hawafanikiwi, huku wale wanaoonekana hawapo sahihi wakiwa wanapata mafanikio makubwa.

Ukweli ni kwamba, mafanikio makubwa yanataka mtu kuwa na mtazamo wa tofauti kabisa na walionao watu wa kawaida. Yanataka namna ya tofauti ya kufikiri na kufanya mambo.

Na moja ya kitu ambacho kinahitajika sana kwenye safari ya mafanikio ni kujiamini kupitiliza. Siyo tu kujiamini kama ambavyo wengi wamekuwa wanaambiwa, bali ni kujiamini kupitiliza.

Kujiamini kupitiliza ni kuwa na uhakika kwamba utapata kila unachotaka na hakuna namna yoyote unaweza kushindwa. Unashikilia imani hiyo bila kuyumbishwa, hata pale unapokuwa huoni kabisa njia ya kupata unachotaka.

Ni vigumu sana kuwa na imani ya aina hiyo kama utatumia akili zako za kawaida. Kwa sababu akili za kawaida huwa zinatumia mantiki, zinaamini kitu baada ya kukiona.

Akili zisizo za kawaida hazitumii mantiki, bali zinatumia imani na hisia. Akili zisizo za kawaida zinaamini kitu kabla hata hakijaonekana. Ni akili hizo zisizo za kawaida ndiyo zimeweza kuleta uvumbuzi wa vitu vingi vipya.

Fikiria vitu vyote tunavyovitumia leo, ambavyo miaka ya nyuma havikuwepo kabisa. Simu, kompyuta, magari na vifaa vingine. Hivi vyote vilianzia kwenye fikra za watu na wakaamini kabisa vinaweza kuwepo. Walipingwa na kukataliwa, lakini hawakukubali kurudi nyuma. Na leo hii, tunafurahia na kunufaika na vitu hivyo.

Swali nililo nalo kwako rafiki yangu ni maeneo gani ambayo una imani kali ya kupata unachotaka licha ya kutokuona njia ya kupata? Ni maeneo gani ambayo watu wanakuchukulia kama umechanganyikiwa au akili zako hazipo sawa?

Hayo ndiyo maeneo ambayo una uwezekano mkubwa wa kujenga mafanikio makubwa. Kwa sababu kuna vitu vya tofauti unavyoviona, ambavyo wengine hawajabahatika kuviona.

Usijione una mapungufu yoyote pale unapoona na kuamini vitu ambavyo kwa wengine vinaonekana ni vya ajabu. Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa, kwa akili zisizo za kawaida.

Wito wangu kwako rafiki yangu, chochote unachokiamini ndani yako, kisimamie na kukifanya, hata kama watu wote wanakuona umechanganyikiwa. Kuonekana umechanganyikiwa ni kiashiria kwamba upo kwenye njia sahihi. Usiiache njia hiyo na kwenda kwenye mazoea ambayo wengi wanayo.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekupa mbinu za kuweza kujijengea hali ya kujiamini kupitiliza kiasi kwamba huwezi kuyumbishwa na mtu yeyote. Nimekuandikia barua hiyo kama zana za mapambano kwenye safari yako ya mafanikio makubwa.

Isome barua hiyo hapa; #BZK016; Jiamini Kupitiliza. Kwa Nini Akili Za Kawaida Kamwe Haziwezi Kukupa Mafanikio Makubwa.

Rafiki, hakuna mtu yeyote ambaye anaona na kuamini kama wewe. Hiyo ni kwa sababu wewe ndiyo toleo pekee hapa duniani. Usijipime kwa kutumia wengine, usiache unachotaka kwa sababu wengine hawakielewi.

Unapochagua kupata mafanikio makubwa, chagua kutokueleweka na walio wengi. Kwa sababu wajibu wako siyo kuwafurahisha watu, bali kupata ushindi ambao upo ndani ya uwezo wako kuupata.

Jiamini kupitiliza ili uweze kupata ushindi mkubwa unaoutaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.