Sikiliza hapa;

Rafiki yangu mpendwa,

Najua meza ninayokwenda kuitikisa hapa ina vinywaji vya bei ghali sana, lakini sina budi, ninaitikisa na liwalo na liwe.

Kwa nini mpaka sasa bado hujaanza biashara ambayo kila mwaka unapanga kuanza?

Kwa nini umekuwa unafanya biashara yako kwa ngazi hiyo hiyo hiyo duni kwa miaka na miaka bila kukua?

Najua jibu unalo la haraka sana; MTAJI.

Na hapo ndipo ninataka kukuvuruga kwa siku ya leo, kwa sababu hilo siyo jibu sahihi.

Lingekuwa jibu sahihi, ungeshatatua hilo tatizo na ukapiga hatua unazotaka.

Na ukitaka kujua siyo jibu sahihi, kaongee na ndugu wanaowasaidia watu wao wa karibu mitaji ya biashara. Utasikia milio wanayotoa, ya jinsi wamewasaidia watu mitaji lakini wameishia kupoteza.

Kaongee na mabenki na taasisi za kifedha, zinazotoa mitaji kwa watu na sikia kilio wanachotoa, kwa wengi wanaoshindwa kurejesha mikopo wanayopewa.

Sitaki hata tuende kwenye programu mbalimbali za kiserikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, yanayokuwa na nia ya kuwainua watu kwa kuwapa mitaji. Programu nyingi zimekuwa za upotevu na hasara kubwa.

Hayo yote ni kiashiria kwamba kushindwa kuanzisha na kukuza biashara haitokani na kukosa mtaji pekee. Japokuwa mtaji ni moja ya mahitaji muhimu, lakini kuna mengine makubwa zaidi kuliko mtaji.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeshirikisha mambo matano muhimu ya kujijengea ili ujenge biashara yenye mafanikio makubwa, hata kama unaanza bila mtaji kabisa.

Hapa nitakushirikisha kwa ufupi mambo matatu, kisha utaenda kuyasoma yote kwa kina zaidi kwenye barua, kwa kiungo nitakachokuwekea hapo chini.

Unahitaji maono makubwa.

Kocha; Kwa nini mpaka sasa hujaanza/hujakuza biashara yako?

Mwanamafanikio; Ni mtaji Kocha, sijapata mtaji.

Kocha; Ni mtaji kiasi gani unachohitaji?

Mwanamafanikio; Nikipata kama milioni 10 hivi, nitapiga hatua kubwa.

Kocha; Nikikupa milioni 10 sasa hivi, utazitumiaje.

Mwanamafanikio; Hapo ni mpaka nipangilie vizuri.

Huo ni mfano wa mazungumzo halisi ambayo nimekuwa nakutana nayo kwa wengi. Na kama utakuwa mkweli kwako mwenyewe, hapo ulipo huna mpango kamili wa kiasi gani cha mtaji unahitaji na ukikipata utakitumiaje.

Unadhani ukishapata pesa ndiyo utaweka mpango. Na hilo ndiyo linakuzuia usipate pesa. Jaribu kwenda benki, hata kama una dhamana kubwa na waambie wakupe pesa. Cha kwanza watakuambia leta mpango.

Sasa wewe unadhani una akili kuliko benki, kwa kutaka upate pesa kwanza kabla ya mpango?

Biashara haifanikiwi kwa mtaji pekee, inahitaji kuwa na mpango thabiti na mpango huo unatokana na maono makubwa ambayo mwanzilishi wa biashara anayo.

Biashara za kuanza kwa kuiga wengine, hazina maisha marefu, hata kama zitapata mtaji mkubwa kadiri vinavyotaka.

Anza na maono na mipango, hivyo vikiwa sahihi, mtaji hauwezi kuwa tatizo. Angalia makampuni machanga (startup) yanayowavutia wawekezaji kuweka fedha hata kabla hayajawa na wateja. Ni kwa sababu ya maono makubwa ambayo mwanzilishi anakuwa nayo.

Unahitaji kujenga timu ya ushindi.

Kitu kingine ambacho watoa mitaji huwa wanakiangalia ni timu iliyopo kwenye biashara. Kuwa wewe mwenyewe ni hatari kubwa kwa biashara, maana wewe unakuwa ndiyo biashara yenyewe.

Kwa na watu wa kuokoteza, yaani wale unaowapata kwa sababu hawana kingine cha kufanya ni kikwazo kuaminika kwenye mtaji. Kwa sababu licha ya kuwa na watu, bado maamuzi yote unafanya mwenyewe.

Kuwa na timu ya watu wenye uwezo mkubwa na unaowapa majukumu makubwa na kufanya maamuzi, kunaifanya biashara iweze kujiendesha bila kukutegemea. Hilo linawapa imani kubwa wale wenye mitaji na kuwa tayari kuiweka kwenye biashara yako.

Kabla hujasema mtaji ni kikwazo, jiulize kama una biashara au wewe ndiyo biashara yenyewe. Ukigundua wewe ndiyo biashara, basi jua hakuna anayekuwa tayari kuibeba hiyo hatari kubwa.

Unahitaji kuepuka ushindani.

Wengi wanaingia kwenye biashara kwa sababu wanaona wengine wanafanya na kupata faida. Hivyo wanadhani wakiingia na mtaji mkubwa, wataweza kuwashinda wale wanaowakuta.

Tena wanaweza kuingia kwa kupunguza sana bei, kwa kuamini wateja watakuja kwao na watapata ukuaji mkubwa na wa haraka. Lakini huo huishia kuwa ushindani mbaya sana na unaopoteza mtaji.

Unapoingia kwenye biashara yoyote ile, kuna vitu vingi unavyokuwa huvijui. Kukimbilia kushindana moja kwa moja, kunakuingiza kwenye matatizo.

Unatakiwa kuingia kwenye biashara ambayo kuna fursa unayoweza kuitatua wewe tu. Unakuwa na kitu ambacho watu wengine hawawezi kukiiga. Hicho ndicho kinakupa faida ya upendeleo na kukuwezesha kufanikiwa.

Haya nimekueleza kwa ufupi hapa, kwenye barua ya Kocha nimeenda kwa kina zaidi. Isome ili utoke ukiwa imara na kuweza kujenga biashara yenye mafanikio hata kama huna mtaji kabisa.

Isome barua hiyo hapa; #BZK013; Zaidi Ya Mtaji – Mambo Unayopaswa Kuzingatia Ili Kujenga Biashara Yenye Mafanikio Makubwa, Hata Kama Huna Mtaji.

Rafiki, ingekuwa kuwa na mtaji ndiyo suluhisho pekee la kuanzisha na kujenga biashara, watu wengi sana wangekuwa na biashara zilizofanikiwa. Lakini kuna mengi ya msingi ya kujenga, ambayo yanahitaji kazi kubwa kuliko mtaji pekee.

Je wewe upo tayari kuweka kazi inayohitajika ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio? Kama ndiyo, basi weka hiyo kazi. Kama siyo, endelea kujifariji na kukosa mtaji, lakini ndani yako jua dhahiri unajidanganya.

Kocha