Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Unasoma hapa kwa sababu unataka kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako. Hutaki kuendelea kubaki hapo ulipo sasa, unaamini unaweza kwenda mbali zaidi ya hapo.

Lakini kuna kitu kimoja lazima nikuambie kama rafiki yako. Kuna namna umeng’ang’ania kubaki hapo ulipo sasa. Najua unaweza kubisha hilo, kwa kudhani umedhamiria kutoka hapo na ndiyo maana uko hapa.

Rafiki, kutaka kitu ni hatua moja. Kuhakikisha unapata kile unachotaka ni hatua nyingine muhimu zaidi. Na kwa bahati mbaya sana, wengi huwa wanaishia kwenye kutaka, kamwe hawaendi kwenye kupata.

Inapokuja kwenye fedha, watu wengi sana wameshindwa kujenga utajiri, siyo kwa sababu haiwezekani kwao, bali kwa sababu wamekuwa wanajizuia wenyewe. Ndiyo, wewe mwenyewe, kwa muda mrefu umekuwa unajizuia kujenga utajiri mkubwa.

Na kwa hili sitanii rafiki, uko hapo ulipo sasa, kwa sababu ndiyo umechagua kuwa hapo. Ukitaka kwenda tofauti na hapo ulipo sasa, lazima uchukue hatua za tofauti.

Kama bado hujafikia utajiri ambao unautaka, siyo kwa sababu utajiri huo hauwezekani, bali ni kwa sababu umechagua hapo ulipo panakutosha. Hata kama kwa maneno unasema tofauti, matendo yako ndiyo yanayodhihirisha ukweli ni upo.

Kuna mambo ambayo umekuwa unayafanya, kama sehemu ya mazoea yako, lakini yamekuwa ni kikwazo kwako kupata pesa nyingi na kujenga utajiri. Mambo hayo ambayo wewe unaona ni ya kawaida, ni kikwazo kikubwa sana kwako.

Kwenye moja ya #BaruaZaKocha nimekuonyesha mambo matano yanayodhihirisha jinsi unavyojizuia wewe mwenyewe kufanikiwa. Hapa nakupa jambo moja, ambalo ni kubwa sana na ukianza kulifanyia kazi, utabadili hali yako mara moja.

Huna Ujuzi Sahihi.

Huwa kuna kanuni moja ya kifedha ambayo ina nguvu sana kama mtu akiielewa na kuifanyia kazi. Kanuni hiyo huwa inatokana na ukweli huu;

‘Huna fedha kwa sababu hutoi thamani,

Hutoi thamani kwa sababu hutatui tatizo,

Hutatui tatizo kwa sababu huwezi kutoa suluhisho,

Huwezi kutoa suluhisho kwa sababu huna ujuzi.’

Hivyo basi, ili kupata fedha nyingi, unapaswa kugeuza huo mtiririko, unajenga ujuzi, ambao unatoa suluhisho kwenye matatizo ambayo watu wanayo na hiyo inakuwa thamani inayofanya ulipwe zaidi.

Fedha ni zao la thamani, na thamani ni matatizo ya watu unayotatua kwa kutumia ujuzi ulionao. Kadiri unavyotatua matatizo makubwa zaidi na yanayowagusa watu wengi zaidi, ndivyo unavyoingiza fedha nyingi zaidi.

Hapo una mahali pa kuanzia, kipato unachoingiza sasa ndiyo kiwango cha thamani unayotoa ambapo ndiyo ujuzi uliojenga. Hujafungiwa kwenye kipato na maisha uliyonayo sasa.

Iko ndani ya uwezo wako kuingiza kipato kikubwa kuliko unachoingiza sasa, kama utatoa thamani kubwa zaidi, kwa kutatua matatizo makubwa kupitia ujuzi mkubwa unaoweza kujijengea.

Huwa kuna kauli maarufu kwamba; ‘Chini ya miaka 30, umasikini ni tatizo la kuzaliwa nalo na zaidi ya miaka 30 umasikini ni tatizo la kujitakia’. Hiyo ni kwa sababu inamchukua mtu miaka 10 kujenga ujuzi kwa viwango vya juu sana kumwezesha kulipwa kiasi kikubwa pia.

Kama mtu ataanza kujenga ujuzi akiwa na miaka 20, mpaka anafika miaka 30 lazima atakuwa na ujuzi wenye thamani kubwa. Kama umri huo umefika na bado anasumbuka na kipato, tatizo siyo alikotoka, bali tatizo ni yeye.

Jitafakari wewe mwenyewe, kama umekuwa kwenye kazi au biashara kwa zaidi ya miaka 5 na bado hali yako ya kifedha ni duni, hilo ni tatizo la ujuzi. Bado hujaweza kujenga ujuzi mahususi, unaotatua matatizo makubwa na ambayo wengi wanayo ili uweze kulipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Na, hakuna njia ya mkato ya kutoka hapo, hata kama umri wako umeenda kiasi gani. Ni lazima urudi kwenye msingi wa kujenga ujuzi unaotatua matatizo ndiyo ulipwe kwa kiasi kikubwa.

Anza na hilo mapema ili uweze kubadili hali yako ya kimaisha.

Rafiki, unaona sasa kwa nini nakuambia umekuwa unajizuia wewe mwenyewe kujenga utajiri? Kama utakuwa mkweli kwako, ingekuwa wewe ndiye umepewa wajibu wa kumlipa mtu mwenye ujuzi ulionao wewe, kwa kupima thamani anayokupa, ungempa hicho unachodhani unastahili kupata?

Kama utakuwa mkweli kwako, unahitaji kujenga ujuzi mkubwa zaidi, unaotoa thamani kubwa kwa walio wengi. Kisha utalipwa kulingana na huo ujuzi na thamani unayopeleka sokoni.

Kamwe usifikiri unapaswa kulipa kulingana na muda, elimu, umri, uzoefu au kingine chochote. Hivyo vipimo vya malipo ndiyo vimekufikisha hapo ulipo sasa. Kutoka hapo, chagua kulipwa kulingana na thamani unayopeleka sokoni. Na hapo sasa, hakikisha unapeleka thamani kubwa zaidi, ambayo inawafanya watu kuwa tayari kukulipa kile unachotaka kulipwa.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza mambo mengine manne, makali kama hili moja ulilojifunza hapa, ambayo yanakuzuia kujenga utajiri. Unapaswa kuyajua mambo hayo ili ujiweke huru na kupata utajiri unaoutaka.

Isome barua hiyo hapa; #BZK014; Mambo Haya Unayokosa Ndiyo Yanakuzuia Kuwa Na Pesa Nyingi Kama Unavyotaka Na Hata Unapozipata Hazikai.

Usichagua ujinga, kwa kuendelea kufanya hayo ambayo umekuwa unafanya halafu utegemee matokeo ya tofauti. Anza sasa kubadili namna unaendea mambo yako ya kifedha na utabadili matokeo yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.