Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Ni tabia yetu binadamu, kutafuta sababu za kujifariji pale mambo yetu yanapokwenda tofauti na matarajio tunayokuwa nayo.
Kwa mfano, pale tunapokutana na watu waliofanikiwa kuliko sisi, huwa tunajifariji kwamba sisi tumeanzia chini kuliko wao. Tunatafuta kitu cha kutuaminisha kwamba wao wameanzia sehemu bora kuliko sisi.
Lakini huo siyo ukweli na haujawahi kumsaidia mtu yeyote kufanikiwa. Kwa kifupi, huwezi kujisikia vizuri na wakati huo huo ukapata mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa yanaanza na dhamira ya dhati ya ndani ya mtu kuhusu kufanikiwa. Dhamira inapokuwa ya ndani, sababu za kujifariji hazipatti nafasi kabisa.
Ndiyo maana nakuambia, kuanzia chini hakujawahi kumzuia yeyote aliyedhamiria kufanikiwa. Hiyo ni kwa sababu dhamira ya kweli inakusukuma kufanya mambo makubwa kuliko ulivyozoea.

Kwenye #BaruaYaKocha, nimekushirikisha mambo ya kuzingatia pale unapoanzia chini kabiasa ili uweze kufanikiwa kwa uhakika. Moja ya mambo hayo ni kuwa na subira kama nilivyoshirikisha hapo chini.
Kuwa Na Subira.
Haraka haraka, haina baraka.
Pole pole ndiyo mwendo.
Kawia ufike.
Mwenda pole hajikwai.
Mvumilivu hula mbivu.
Zote hizo ni mithali na semi zinazoonyesha nguvu ya subira na uvumilivu kwenye safari ya mafanikio.
Lakini tunapokuja kwenye maisha halisi, tunafikiri kwa tofauti kabisa. Tunataka mambo yatokee kwa haraka, la sivyo tunaachana nayo na kwenda kwenye mambo mengine.
Mahangaiko ya watu kwenye kutafuta njia za haraka na za mkato za kufanikiwa imekuwa kikwazo kwao kufanikiwa. Wengi wamejikuta wakipoteza muda na hata kutapeliwa kwa kuhangaika na njia za mkato za kufanikiwa.
Kama unaanzia chini kabisa na unataka kufanikiwa, jipe muda. Hiyo ndiyo silaha pekee iliyo upande wako, ambayo ukiweza kuitumia vizuri, utafanikiwa kwa uhakika.
Kila jambo kubwa linahitaji muda kujengeka. Na hakuna namna unaweza kuharakisha muda huo. Kwa sababu muda siyo tu kipindi unasubiri, bali muda ni kipindi mafanikio yanajengeka.
Warren Buffet amewahi kusema; ‘Huwezi kupata mtoto kwa mwezi mmoja kwa kugawa ujauzito mmoja kwa wanawake tisa.’ Hilo ni kosa ambalo wengi wamekuwa wanalifanya kwenye safari ya mafanikio. Wanatafuta njia za kufupisha muda, na njia hizo ndiyo zinakuwa kikwazo kwao kupata wanachotaka.
Mafanikio makubwa yanahitaji muda, ambao hakuna namna unaweza kuukwepa. Kuwa na subira, kuwa mvumilivu. Hakuna juhudi unazoweka zinapotea. Kila unachofanya kinajikusanya na kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
Rafiki, hili ni jambo moja la kufanya, kati ya mambo matano niliyoyashirikisha kwenye #BaruaYaKocha. Karibu uisome barua kamili na uchukue hatua ili popote unakoanzia kusiwe kikwazo kwako kufanikiwa.
Isome barua hapa; #BZK015; Hili Ndiyo Tegemeo Pekee Kwako Kufanikiwa Kama Unaanzia Chini, Huna Koneksheni Na Huna Akili Nyingi.
Rafiki, unakoanzia hakuna athari sana kwenye mafanikio unayoweza kupata, bali yale unayofanya ndiyo yatakayoathiri hali yako. Epuka kujikwamisha wewe mwenyewe kutoka hapo ulipo, kwa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija.
Jijengee sifa sahihi kwako na kwa wengine, kuwa mtu unayeaminika na kutegemewa, kupitia misingi unayoiishi na matokeo unayozalisha. Na kuwa mtu mwenye subira, ukijua kila kitu kinakuja kwako kwa wakati sahihi.
Kuyaishi hayo kunakupa uhakika wa kujenga mafanikio makubwa, hata kama unaanzia chini kabisa. Hakuna kinachokuzuia wewe kufanikiwa isipokuwa wewe mwenyewe. Anza sasa kuchukua hatua sahihi ili uweze kupata mafanikio unayoyataka.
Kocha