Sikiliza hapa;

Rafiki,

Hivi umewahi kugundua kwamba watu huwa wanapenda kushindana ni nani anateseka zaidi? Mwambie mtu changamoto unazopitia kwenye maisha na ataanza kukuonyesha kwa nini changamoto zako ni ndogo kuliko nyingi alizonazo yeye.

Ni kama vile kuna tuzo za nani anayeteseka zaidi, nani mwenye matatizo na msongo zaidi. Jambo hilo linaloweza kuonekana dogo sana, limekuwa chanzo cha wengi kukosa furaha na mafanikio kwenye maisha yao.

Huwa kuna kauli inasema; ‘Ukicheza michezo ya kijinga, utashinda zawadi za kijinga’. Moja ya michezo ya kijinga ambayo wengi wanaicheza kwenye mafanikio ni huo wa kuonyesha una matatizo na changamoto zaidi ya wengine.

Hata kama kweli umewashinda wengine, kwa kuwa mwenye matatizo na changamoto zaidi, huo ushindi unakuwa umekupa nini? Hakuna unachokuwa umepata zaidi ya matatizo zaidi na changamoto zaidi.

Tumejadiliana mara nyingi hapa jinsi ambavyo furaha ni hitaji muhimu kwenye safari ya mafanikio. Tumeona jinsi ambavyo furaha inayatangulia mafanikio, yaani unaanza kuwa na furaha kwanza ndiyo unafanikiwa, na siyo kinyume chake.

Sasa kama tena unakuja kuingia kwenye mashindano ya nani hana furaha zaidi, unadhani utaweza kweli kuyakaribisha mafanikio makubwa unayoyataka?

Ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka, furaha inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza. Na siyo tu furaha, bali furaha yako binafsi. Kama huwezi kujihakikishia furaha yako, huwezi kujihakikishia mafanikio makubwa.

Huenda unawaonyesha wengine wewe una matatizo na changamoto zaidi ili kuwafanya wajisikie vizuri, lakini hilo halina afya kwa mafanikio yako.

Una jukumu moja kubwa hapa duniani, ambalo ni kujifurahisha wewe mwenyewe kwanza. Una wajibu wa kuhakikisha una furaha ya uhakika na ya kudumu, ili uweze kuvuta mengine unayoyataka kwenye maisha yako.

Na furaha siyo kitu kinachotokea tu, bali ni kitu kinachotengenezwa. Wengi hawna furaha siyo kwa sababu za nje, bali kwa sababu za ndani yao wenyewe.

Ili kuhakikisha wewe una furaha wakati wote, hata kama bado una changamoto na vikwazo mbalimbali, zingatia mambo haya ya msingi.

Moja ni kujitambua wewe mwenyewe.

Huwezi kuwa na furaha kama hujijui wewe mwenyewe. Kama unaendesha maisha yako kwa kuiga wengine, utapata matokeo ambayo hayaendani na wewe. Hilo litakunyima furaha, hata kama matokeo unayoyapata kwa nje yanaonekana makubwa.

Furaha haitokani na kile unachopata, bali jinsi unavyoishi kikamilifu kama wewe. Jinsi unavyotumia rasilimali zilizo ndani yako ndiyo inakupa kuridhika na furaha.

Jitambue na kuwa wewe, ufanye yale yenye tija kwako na utayafurahia maisha yako hata kama unapitia matatizo na changamoto kubwa kiasi gani.

Mbili ni usihangaike kuwafurahisha wengine.

Unaweza kujiona una wajibu wa kuwafurahisha watu wengine. Lakini unapojaribu kufanya hivyo, unashindwa kwenye maeneo mawili.

Kwanza unashindwa kuwafurahisha wengine, kwa sababu wao wenyewe wanashindwa kujifurahisha.

Mbili ni wewe mwenyewe unashindwa kujifurahisha, kwa sababu ulichopanga kimeshindwa.

Kuliko ujisumbue na kitu kilicho nje ya uwezo wako, kitakachopelekea wewe kukosa furaha, ni bora kuhangaika na kile unachoweza kukidhibiti.

Na inapokuja kwenye furaha, kitu pekee unachoweza kudhibiti ni furaha yako mwenyewe. Furaha za wengine zipo ndani ya uwezo wao.

Kama unaona furaha ya wengine ni wajibu wako, njia pekee ya kutekeleza wajibu huo ni kuhakikisha wewe una furaha na kutokuwalazimisha wengine kuwa na furaha.

Tatu ni kuona uzuri kwenye kila jambo.

Utapanga mambo mengi mazuri, utatekeleza mipango unayoweka, lakini matokeo yatakuja tofauti kabisa na matarajio uliyokuwa nayo.

Wengi wanaruhusu matokeo wanayopata yawakwamishe kwenye kuwa na furaha kwenye maisha yao.

Kwa sababu huwezi kudhibiti matokeo, unapaswa kudhibiti jinsi unavyoyapokea matokeo hayo. Na unachoweza kufanya ni kuona uzuri kwenye kila jambo.

Kwa kila matokeo unayopata, jiulize ni kitu gani kizuri kipo ndani yake. Hata kama ni tofauti kabisa na matarajio yako, wewe angalia fursa iliyo ndani yake.

Kwa njia hiyo utaona fursa nzuri za kutumia kila unachokutana nacho kupata furaha na mafanikio makubwa.

Kwenye #BaruaYaKocha nimeeleza kwa kina dhana ya furaha kuwa wajibu wako namba moja. Nimekuonyesha jinsi ambavyo ubinafsi ni muhimu kwenye kujihakikishia furaha. Ni barua itakayokuondoa kwenye vifungo vinavyokuzuia kuwa na furaha.

Isome barua hiyo hapa; #BZK012; Una Jukumu La Kumfurahisha Mtu Mmoja Pekee, Na Umeshindwa Kulitimiza

Rafiki, ukijipa wajibu wa kuwafurahisha watu wengine, unakuwa umeshindwa kabla hata hujaianza safari. Lakini ukijipa wajibu wa kujifurahisha wewe mwenyewe, ushindi unakuwa wa uhakika kwako.

Kizuri ni kwamba, kama utajifurahisha mwenyewe, unawapa wengine sababu ya wao kujifurahisha wenyewe pia. Na hilo linakupa nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa.

Kocha