Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Tasnia ya mafunzo ya mafanikio ina semi za aina nyingi, ambazo zimekuwa zinaaminika kama njia ya kuwapa watu hamasa ya kufanikiwa.
Moja ya semi hizo ni; ‘Ukifanya kile unachopenda, hutajiona unafanya kazi na mafanikio yanakuwa ya uhakika’.
Usemi huu kuna sehemu una ukweli, lakini kwa sehemu kubwa siyo kweli. Kwa watu kutokujua upande wa usemi huo ambao siyo kweli, wamejikuta wakijipotosha wao wenyewe na kujizuia kupata mafanikio makubwa yanayokuwa ndani ya uwezo wao.
Upande sahihi wa usemi huo ni unapofanya kile unachopenda, haiwi kazi ngumu kwako. Hilo halina ubishi kabisa, unachopenda kinakuwa mchezo kwako, wakati kwa wengine inakuwa ni kazi ngumu.
Na moja ya vitu vinavyoweza kukutofautisha sana kwenye safari ya mafanikio ni uwezo wa kufanya kitu kwa muda mrefu bila kuchoka. Wakati wengine wanakata tamaa na kuacha, anayeendelea kwa muda mrefu ndiye anayepata ushindi.
Upande usio sahihi wa usemi huo ni unapofanya kile unachopenda mafanikio yanakuwa ya uhakika. Huu upande unahitaji tahadhari kubwa, kwa sababu umepelekea wengi kupoteza muda mwingi wa maisha yao kwenye vitu visivyokuwa na tija.
Kabla hatujaendelea na huo upande wa kufanya unachopenda, turudi kwenye msingi kamili wa mafanikio. Hufanikiwi kwa sababu unastahili kupewa mafanikio, unafanikiwa kwa sababu umeishawishi dunia ikupe unachotaka.
Na njia ya kuifanya dunia ikupe unachotaka, ni wewe kuipa dunia kile inachotaka. Ni lazima utoe thamani kwanza, ndiyo dunia ikulipe sawasawa na thamani hiyo. Hivyo ndivyo unavyopata mafanikio makubwa.

Sasa turudi kwenye usemi wa kupenda unachofanya. Je kile unachopenda kufanya ndiyo chenye thamani kwenye dunia?
Kwa mfano kama unachopenda kufanya ni kulala, ni thamani gani unaipa dunia kupitia kupenda kwako kulala? Sisemi kwamba kupenda kulala hakuwezi kukupa mafanikio, bali ni lazima ujiulize ni thamani gani unatoa kwenye dunia kupitia hicho unachopenda kufanya.
Watu wengi wanakazana kuangalia upande wa mapenzi na kusahau kuangalia upande wa thamani wanayotoa. Hilo ndiyo limewapotosha wengi, wakajikuta wanapoteza muda na kushindwa kujenga mafanikio makubwa waliyoyataka.
Kabla hujapoteza muda mwingina kitu unachochagua kufanya, jibu kwanza swali la thamani unayotoa kupitia kitu hicho. Ni matatizo gani ya wengine unayoyatatua kupitia hicho unachofanya?
Kadiri matatizo unayotatua yanavyokuwa makubwa na yanayowaathiri watu wengi, ndivyo mafanikio unayopata yanavyokuwa makubwa.
Ikitokea kile unachopenda kufanya kinatatua matatizo makubwa na yanayowaathiri wengi, badi upo kwenye njia sahihi ya kujenga mafanikio makubwa.
Je, vipi upande wa pili? Vipi kama umegundua unachopenda kufanya hakitoi thamani na hivyo hakiwezi kukupa mafanikio makubwa? Je ndiyo huna kabisa tumaini la kufanikiwa?
La hasha, bado unaweza kufanikiwa kwa ukubwa tu, lakini siyo kwa kwenda na kauli hiyo kwa mazoea. Badala yake unapaswa kuigeuza ili upate matokeo sahihi.
Kama unachopenda kufanya hakiwezi kukupa mafanikio, penda kile kinachoweza kukupa mafanikio. Yaani kama hicho unachopenda kufanya hakitoi thamani kubwa, angalia nini kinatoa thamani kubwa na ukipende hicho.
Kwa kujua kile ambacho kinatatua matatizo makubwa na yanayowaathiri wengi na ukapenda kukifanya, inakuweka kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa. Ni mapenzi unayoyatengeneza ndiyo yanayokutofautisha na wale wanaofanya kwa mazoea tu.
Kama unaona hilo ni gumu, kwamba huwezi kupenda kile kinachotoa thamani kwa wengine, umechagua kujikwamisha wewe mwenyewe kufanikiwa. Wewe siyo mti, wewe ni binadamu. Na moja ya sifa za binadamu, ambayo inatutofautisha kabisa na viumbe wengine wote ni uwezo wetu wa kubadilika na kuendana na mazingira.
Uwezo huo wa kubadilika na kuendana na mazingira ndiyo umefanya kizazi chetu binadamu kuvuka nyakati ngumu na kuendelea kubaki hapa duniani. Hivyo hata wewe unaweza kubadilika, kutoka kwenye hicho unachopenda sasa ambacho hakikupi mafanikio na kwenda kwenye kupenda kinachoweza kukupa mafanikio.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha njia za kukuwezesha kubadilika kutoka kwenye hicho unachopenda sasa na kupenda kile kinachoweza kukupa mafanikio unayoyataka.
Moja ya njia ambayo utaipenda sana ni inayohusu kuisha kwa kipindi cha fungate (honey moon). Kutokujua dhana hiyo kumekuwa kunakukwamisha sana kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Isome barua hiyo hapa ili usijikwamishe tena kufanikiwa; #BZK011; Usivurugwe Na Mapenzi Kwenye Safari Ya Mafanikio.
Rafiki, kutaka mafanikio na kupata mafanikio ni vitu viwili tofauti. Usiishie tu kuyataka mafanikio, nenda kwenye kuweka mkakati sahihi utakaokuhakikishia mafanikio.
Kuachana na kile unachopenda kufanya na kisichokupa mafanikio na kwenda kwenye kupenda kufanya kitakachokupa mafanikio ni mabadiliko muhimu unayopaswa kufanya ili ufanikiwe kwa uhakika.
Kocha
