Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwa chochote utakachochagua kufanya kwenye maisha yako, watu watagawanyika kwenye makundi matatu.
Kundi la kwanza watakubaliana na wewe kwa hicho unachofanya. Watakuunga mkono na kukuambia uko sahihi kwa unachofanya. Hawa utawaona wana ushauri mzuri kwako.
Kundi la pili watakupinga kwa hicho unachofanya. Watakuona unakosea na kukushauri uachane nacho. Hawa utawaona wana ushauri mbaya kwako.
Kundi la tatu hawatajali kuhusu unachofanya. Hawajui hata unachofanya ni nini na hawana ushauri wowote kwako. Hawa utawaona kama watu wasiokujali na wanaojali mambo yao tu.
Swali ni je, kundi lipi lipo sahihi? Kwa haraka utaona kundi la kwanza lipo sahihi. Lakini hiyo siyo kweli, hakuna kundi hata moja ambalo lipo sahihi hapo inapokuja kwenye kile ulichochagua kufanya.
Usahihi wa chochote unachofanya, unaanzia ndani yako wewe na siyo nje. Haijalishi watu wengine wanachukuliaje na wanakushauri nini, usahihi wa kitu unaanzia ndani yako.

Kitu sahihi kwako kufanya ni kile kinachokidhi vigezo hivi viwili;
Moja ni FURAHA.
Furaha ni hitaji la msingi sana kwetu. Kila tunachofanya, huwa tunasukumwa na hitaji la kuwa na furaha zaidi, kuwa bora zaidi ya tulivyokuwa. Hakuna mtu anayechagua kufanya jambo ambalo linamfanya asiwe na furaha.
Lakini kwa bahati mbaya sana, kuna wengi wamechanganya raha na furaha. Raha ni kitu cha muda mfupi, na kinachotokana na vitu vya nje. Kutumia vilevi ni moja ya njia ambazo watu wanatumia kupata raha.
Furaha ni kitu kinachodumu kwa muda mrefu, na kinatokana na vitu vya ndani. Pale unapojua kusudi la maisha yako na kuliishi, ni rahisi kuwa na furaha. Unapofanya vitu ambavyo vinatoa thamani kubwa kwa wengine, unakuwa na furaha.
Kama unachofanya kinakupa furaha ya ndani, wapuuze wote wanaokushauri kufanya vinginevyo. Hawapo ndani yako na hawawezi kuelewa chanzo cha furaha yako. wasikilize, ila wapuuze.
Mbili ni UHURU.
Tangu tunazaliwa, tumekuwa tunapambana kuwa huru zaidi. Kitendo chenyewe cha kuzaliwa ni kutafuta uhuru. Maana tunakaa ndani ya matumbo ya mama zetu tukipata kila kirutubisho tunachotaka. Lakini tunakosa uhuru. Tangu utoto mpaka kukua, tunatafuta uhuru zaidi.
Lakini kwa bahati mbaya sana, kadiri tunavyokuwa watu wazima, ndivyo tunavyopoteza uhuru wetu. Tunajikuta kwenye kazi au biashara tusizozipenda, tukiwa na kipato kisichotosheleza na mahitaji makubwa ya maisha.
Unapaswa kutumia uhuru kama kigezo cha jambo lolote utakalofanya. Kama unachofanya kinakupa uhuru zaidi, kifanye bila kusikiliza ushauri wa wanaokupinga.
Watu wasio huru, hawawezi kukuelewa pale unapopambana kuwa huru. Kwa sababu wao wameshapoteza uhuru, hawaamini wengine wanaweza kuwa huru. Hivyo usitegemee kuungwa mkono na wasio huru, kwenye harakati zako za kuwa huru.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekueleza kwa kina zaidi vigezo hivi viwili na jinsi ya kuvitumia kujenga maisha ya mafanikio makubwa, unayoyafurahia na yanayokuweka huru.
Isome barua hiyo hapa; #BZK010; Tumia Vigezo Hivi Viwili Kuchagua Utakachofanya Bila Kuyumbishwa Na Wengine.
Kuna maeneo utahitajika kuwaomba watu ushauri au kusikiliza ushauri wao. Lakini hilo halipaswi kuwa kwenye maamuzi ya nini hasa unafanya na maisha yako. Hilo ni wewe mwenyewe unayeweza kujua, kwa kuzingatia vigezo viwili vya FURAHA na UHURU.
Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, chagua kwa utashi wako ili usije ukapeleka lawama kwa wengine pale matokeo unayopata yanapokuwa tofauti na matarajio uliyokuwa nayo.
Kocha
