Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kupiga hatua na kufanikiwa kwenye maisha.

Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza jinsi ya kuondoka kwenye uraibu wa kucheza kamari au kama ilivyo maarufu kwa jina la betting.

Hii ni changamoto ambayo imekuwa inawasumbua wengi na baadhi ya wasomaji wameomba ushauri kwenye hili kama inavyosomeka hapo chini;

Mimi nipo kazini na kamari imekua kikwazo kwangu najikuta nafanya kazi na Kila siku nabeti naomba ushauri. – Leonce L.

Kamari imeniumiza sana tangu 2000 adi 2020 nimejaribu kuacha lakini nimeshindwa kwa kweli. – Robert M.

Betting, nimekuwa nikitumia 20k – 50k kwa siku. Naomba ushauri nawezaje kuacha. – Lucas J.

Uraibu wa kucheza kamari ni tatizo ambalo kwa sasa linawasumbua watu wengi, ila wengi hawajui njia sahihi ya kuondokana na hilo.

Hilo linapelekea waendelee kuumia na tabia hiyo ambayo inakuwa imejenga mizizi ndani yao na kuwa kikwazo kwa mafanikio yao.

Nimewahi kuandika na kutoa maneno makali kwa wote wanaocheza michezo hii (unaweza kusoma hapa; Kama Umewahi Kucheza Kamari Au Bahati Nasibu Nina Maneno Makali Kwako, Yasome Na Yatakusaidia.).

Lakini leo sitakuwa upande wa ukali au kumlaumu mchezaji, uraibu wa kamari ni kama ugonjwa mwingine, hivyo nitakuwa upande wa daktari kukusaidia wewe ambaye umeshaingia kwenye uraibu wa kamari au kitu kingine chochote.

Uraibu ni pale ambapo unafanya kitu nje ya udhibiti wako, yaani unajikuta umefanya hata kama hutaki kufanya.

Uraibu huwa unajengwa kama tabia, kwa kurudia kufanya kitu kwa muda mrefu, mazoea yanajengeka ndani yako na hivyo unajikuta unafanya bila ya kufikiria.

Kwenye uraibu, kunakuwa na zaidi ya mazoea, akili na mwili vinakuwa vimeshategemea sana mtu ufanye kitu hicho, kiasi kwamba ukiacha unakuwa haupo sawa kiakili na kimwili.

Uraibu wa kamari ni moja wapo ya magonjwa ya akili, kwa sababu akili ya mtu mwenye uraibu huo haiwezi kutulia mpaka atakapocheza kamari. Hata kama anapoteza kiasi kikubwa, bado atacheza ili kuiridhisha akili yake.

Unaweza kushangaa kwa nini watu wapo radhi kuuza hata vitu vya thamani au kuviweka rehani ili tu wapate fedha za kucheza kamari. Ni kwa sababu kamari ikishakuwa uraibu, inakuwa ugonjwa wa akili.

Hivyo ili kuvunja uraibu huu, tunapaswa kuanzia kwenye akili.

Hatua ya kwanza ya kuvunja uraibu wa kamari ni kujua imani ulizojijengea kuhusu fedha na utajiri.

Iko wazi kwamba mtu anaanza kucheza kamari kwa kuvutiwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho anaweza kukipata. Mtu anakuwa anaamini kupitia kamari anaweza kupata fedha nyingi na kufika kwenye utajiri.

Hiyo ndiyo imani unayopaswa kuivunja ili kuondoka kwenye uraibu huo.

Tambua kwamba kamari siyo njia ya kuingiza fedha wala kufika kwenye utajiri, bali ni njia ya kupoteza fedha.

Ukiwa kwenye uraibu utasema, mbona kuna wengine wanapata, mbona huko nyuma nimewahi kupata fedha nyingi. Lakini hizo zote ni dalili za ugonjwa.

Kamari ya aina yoyote ile, imetengenezwa kwa namna ambayo mtu mmoja akishinda, watu wanne wamekuwa wameshindwa. Huwezi kuzidi hesabu hizo hata uwe na akili kiasi gani.

Kamari ni biashara ya wale wanaoziendesha na ili biashara iendelee lazima iwe na faida. Hivyo unapoona kamari zinawalipa watu mamilioni ya fedha, jua hao waendesha kamari wamebaki na mamilioni mengi zaidi kama faida.

Kwa kifupi tunaweza kusema kamari ni mchezo wa kukusanya fedha kwa watu wengi, halafu kuchagua mmoja au wachache kwa kubahatisha na kuwapa kiasi kidogo cha fedha, ili wengine waendelee kupata matumaini na kuendelea kucheza.

Vunja imani kwamba unaweza kupata fedha na utajiri kupitia kamari. Jua njia ya uhakika ya kupata fedha na utajiri ni kwa kutoa thamani kwa wengine. Kwenye kamari hakuna thamani yoyote unayotoa.

Imani huwa zina nguvu sana kwetu, ukivunja imani, utabadili fikra, maamuzi, matendo na matokeo unayozalisha.

Kuanzia sasa kila ukiona kamari au wengine wanacheza kamari jiambie wale wanapoteza fedha zao. Wewe mwenyewe kokotoa fedha umewahi kupoteza na linganisha na ulizowahi kupata, utaona wazi kwamba umekuwa unapoteza fedha.

Uraibu wowote huwa unaendelea kujijengea mizizi kutokana na vichocheo vya nje ambavyo mtu anakutana navyo na vinamsukuma kwenda kwenye uraibu.

Hivyo hatua ya pili ya kuondokana na uraibu wa kamari ni kujua vichocheo vya nje vinavyokusukuma kucheza kamari.

Angalia ni wakati gani unasukumwa kucheza kamari, utaona kuna hali au mazingira fulani ambayo unakuwepo.

Mfano kama wewe ni mshabiki wa michezo, siku ya michezo mikubwa utakuta unasukumwa sana kucheza kamari.

Kama una marafiki ambao ni wacheza kamari, kila ukiwa nao utashawishika kucheza kamari.

Na wakati mwingine ukiwa na hasira au unajisikia vibaya, unaweza kujikuta unacheza kamari ili tu kujisikia vizuri.

Unapaswa kujua msukumo wa nje unaokufanya ucheze kamari na kuweza kuudhibiti.

Katika kuvunja tabia au uraibu wa aina yoyote ile, mazingira ni muhimu sana. Kama unataka kuacha pombe halafu ndani kwako una kreti ya bia unajidanganya tu.

Kadhalika kwenye kamari, kama unataka kuacha kamari lakini unaambatana na wanaocheza kamari au kwenda kuangalia michezo maeneo ambayo kamari inachezeshwa unajidanganya.

Futa kabisa mazingira au hali zinazokuchochea kucheza kamari. Kama ni marafiki epuka kukaa nao, kama ni eneo epuka kulitembelea na kama ni michezo achana nayo kwa muda.

Kadhalika kwa hali zako mwenyewe kama hasira, uchovu au kutokujisikia vizuri, usikimbilie kuchukua hatua unapokuwa kwenye hali hizo. Jipe muda na hali hizo zitaisha zenyewe.

Unapotaka kuvunja uraibu ulionao saa, unapaswa kuwa na tabia nyingine inayochukua nafasi yake, la sivyo utarudi kwenye uraibu huo.

Hatua ya tatu kwenye kuvunja uraibu wa kamari ni kutafuta tabia nyingine itakayoziba pengo la kamari.

Asili huwa haipendi utupu, huwa inaujaza kwa namna yoyote ile. Ukiacha kucheza kamari halafu muda wako ukawa huna cha kufanya, utajikuta unarudi tu kwenye kamari, kwa sababu utakuwa unajisikia vibaya sana.

Hivyo unapaswa uchague kitu kingine cha kufanya kitakachokuwa mbadala wa kamari.

Unaweza kuchagua kujisomea vitabu, kujifunza kitu fulani, kushiriki michezo unayopenda na kadhalika.

Lengo ni usiwe na muda ambao unakuwa huna cha kufanya, wanasema akili isiyo na cha kufanya ni karakana ya maovu.

Msukumo huo huo unaokupeleka kwenye kamari, utumie kwenye kufanya kitu kingine unachopenda, lakini chenye manufaa kwako.

Vipo vingi mno vya kufanya, jua kipi unapenda kisha panga kukifanya kwenye muda ambao unauokoa kwenye kucheza kamari.

Kuwa na pesa za ziada inaweza kuwa kichocheo cha wewe kucheza kamari, hivyo kutokuwa na fedha inaweza kuwa njia nzuri ya kuvunja uraibu huu.

Hatua ya nne kwenye kuvunja uraibu wa kamari ni kutengana na fedha zako za ziada. Hakikisha huna fedha ambayo haina matumizi mfukoni, benki au kwenye simu yako.

Na hapa unapaswa kuchukua hatua moja, nenda benki na fungua akaunti maalumu ambayo unaweza kuweka fedha tu ila kutoa siyo rahisi. Akaunti hiyo usiwe na ATM wala kuunganisha na huduma za simu.

Hapo sasa kila fedha ya ziada unayokuwa nayo, weka kwenye akaunti hiyo. Kila fedha ambayo ulikuwa unaitumia kucheza kamari, weka kwenye akaunti yako.

Mara zote baki ukiwa umefulia na fedha zote weka kwenye akaunti yako maalumu. Kama huna fedha za ziada, huwezi kucheza kamari na hapo tabia itakosa nguvu ya kuendelea kuwa imara kwako.

Kama nilivyoeleza, uraibu ni ugonjwa, umejijenga kwa muda mrefu na hata kuuvunja itachukua muda pia, hivyo unapaswa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua sahihi.

Hatua ya tano ya kuvunja uraibu wa kamari ni kuendelea kujifunza na kuchukua hatua sahihi za kuondoka kwenye uraibu huo.

Kuna vitatu viwili muhimu sana unavyopaswa kuvisoma ili kuendelea kuelewa kwa kina kuhusu uraibu huo na hatua sahihi unazopaswa kuendelea kuchukua ili kuuvunja na kuhakikisha hurudi tena.

Kitabu cha kwanza ni UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, kitabu hiki kinaeleza jinsi akili yako ilivyo na nguvu ya kujenga tabia. Ni katika nguvu hiyo pia ndiyo unaweza kuvunja tabia mbalimbali ulizojijengea.

Kitabu cha pili ni EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI, kitabu hiki kimeeleza jinsi uraibu unavyojengeka na unavyoweza kutumia uwepo wa kiakili (mindfullness) kuvunja uraibu wowote ulionao.

Kitabu cha tatu ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kwenye kitabu hiki utajifunza jinsi ya kujijengea gereza la kifedha na kuweka akiba bila kuzigusa, hapo utaweza kutengana na fedha unazopotezea kwenye kamari.

Kupata vitabu hivyo, wasiliana na 0752 977 170.

Uraibu wa aina yoyote ile ni ugonjwa ambao unahitaji jitihada kubwa ili kuweza kuuvunja.

Kwa sasa kuna wengi wana uraibu wa matumizi ya mitandao pia, kwenye kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI kuna mengi ya kujifunza kuhusu hilo.

Fanyia kazi hatua hizi tano tulizojifunza hapa na utaweza kuvunja uraibu wa kamari unaokusumbua.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp