Habari za leo ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio.

Leo tutajadili changamoto ya kusafisha nyota ya biashara. Kabla hatujajadili changamoto hii tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu.

kila ninapo anzisha biashara mwanzoni inachanya sana na napata wateja sana lakini ninavyozidi kukazana napata hasara kubwa ghafla hadi napoteza hamu ya kuendelea, ndugu zangu wa karibu wanasema sina nyota ya biashara na wengine wanasema nyota yangu imechafuliwa sasa nashindwa nifanyeje na wengine wana sema niende kwa mganga daaah yaaan mpaka kichwa kinafreeze kabisa nisaidie ndugu na kama kunadala inatakiwa nilipate niko tayari mimi ni mwanafunzi wa mwaka wapili kutoka chuo cha kumbukumbu ya mwl.nyerere kigamboni nasomea ualimu.

Kama tulivyoona kwenye maoni ya msomaji mwenzetu kuna watu wengi sana wanaopitia changamoto kama hiyo na wengi zaidi wanaoamini hawana nyota ya biashara au nyota yao imechafuliwa.

Je una nyota ya biashara?

Unapoanza kujiuliza kama una nyota ya biashara au huna hapa unaingia kwenye maswala ya imani. Na kama utaamini una nyota ya biashara ni kweli utakuwa nayo na pia kama utaamini huna nyota ya biashara ni kweli hutakuwa nayo. Hakuna kitu kwamba watu fulani ndio wamepewa nyota ya biashara, kila mtu anaweza kufanya biashara kama atakuwa anaipenda kweli na kama atajituma na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kutokukata tamaa.

Hivyo amini kwamba unayo nyota ya biashara na utaweza kufanya biashara.

Je nyota yako ya biashara inaweza kuchafuliwa?

Habari ya kuchafuliwa nyota ya biashara nayo ni imani, kama utaamini nyota yako imechafuliwa itakuwa imechafuliwa kweli. Lakini kitu kimoja nachoweza kukuambia ni kwamba kama nyota yako imechafuliwa basi umeichafua mwenyewe. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuchafua nyota yako ya biashara isipokuwa imani yako. Kumbuka imani inaumba, chochote unachoamini bila ya kuyumbishwa kinakuwa kweli.

Kama nilivyosema kwenye makala hivi ndivyo unavyoweza kuepuka chuma ulete kwenye biashara yako wewe mwenyewe ndio chuma ulete wa biashara yako.(fungua hapo kusoma)

Kitu ambacho kinatokea kwa msomaji mwenzetu ni hali ya kawaida kwenye biashara, mafanikio kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla sio njia iliyonyooka, bali ni njia ambayo ina kona nyingi na inaweza kukukatisha tamaa.

Unapoanza biashara unaweza kuwa na matumaini makubwa na shauku kubwa ya kufanya biashara hiyo. Baada ya muda kidogo unaanza kukutana na changamoto ambazo kama hujajipanga zinaweza kukukatisha tamaa na ukaondoka kwenye biashara kabisa. Kila biashara inapitia kipindi kigumu na wale wanaoweza kuvumilia ndio wanapata mafanikio, wanaoshindwa kuvumilia ndio wanakata tamaa na kuanza kutafuta sababu kwa nini wameshindwa.

Ufanye nini ili uweze kuvuka vipindi hivi vigumu kwenye biashara?

Kwa kuwa kufanikiwa au kushindwa kwenye biashara inategemea na wewe mwenyewe, hapa nakushirikisha mambo machache yanayoweza kukupitisha katika kipindi hiki kigumu.

1. Kuwa na mpango wa biashara ambao utaainisha hatua zote za biashara.

Kama unafanya biashara kwa njia za kienyeji ni vigumu sana kujua kama biashara iko vizuri au imeshaanza kuporomoka. Jinsi unavyochelewa kujua maendeleo ya biashara yako ndio inavyokuwa rahisi kwa wewe kupata hasara.

2. Kuwa na mpango mbadala wa kukuinua mambo yanapokuwa magumu.

Mara nyingi inashauriwa kutokuweka mtaji wako wote kwenye biashara pale unapoanza. Hii ni kwa sababu ikitokea changamoto na ukawa huna fedha za kukunyanyua utapotea kabisa. Hivyo mwanzoni mwa biashara weka sehemu ya mtaji pembeni kama fedha ya kukuinua pale mambo yanapokwenda vibaya.

3. Kuwa na usimamizi mzuri wa fedha katika biashara yako.

Fedha ndio damu ya biashara, ukiwa na usimamizi mbovu na ukaanza kupoteza fedha ndio kifo cha biashara kinaanza na baadae unasingizia chuma ulete. Asilimia kubwa ya biashara zinazokufa matatizo yanaanzia kwenye usimamizi wa fedha.

Soma; Njia sita za kudhibiti matumizi ya fedha kwenye biashara.

4. Amini kwamba unaweza.

Ndio una nyota ya biashara na hapana hakuna aliyechafua nyota yako ya biashara. Usihangaike kwenda kwa mganga kusafishiwa nyota. Mganga anaenda kubadili saikolojia yako tu, kitu ambacho hata wewe unaweza kukifanya. Amini kwamba unaweza kufanikiwa kwenye biashara na weka juhudi na maarifa ili uweze kufikia mafaniko makubwa.

Soma; Kwa nini waganga wanaweza kuwasaidia wengine wakati wao wana maisha magumu.

5. Uvumilivu, uvumilivu, uvumilivu.

Hili ndio jamno la msingi sana kwenye biashara na hata kwenye maisha. Mambo yanapokuwa magumu(na lazima itakuwa hivyo) sio wakati wa wewe kukata tamaa na kuachana nayo bali huo ndio wakati wa wewe kujifunza na kufanya marekebisho madogo madogo ili uweze kufikia malengo yako. Kuwa na uvumilivu huku ukijaribu njia mbalimbali zinatakozoweza kukutoa kwenye hali hiyo ngumu.

Kufanikiwa au kushindwa kwa biashara yako kupo mikononi mwako. Amua kwamba utakwenda kufanikiwa kwenye biashara unayofanya na tumia njia zote ulizojifunza na utakazoendelea kujifunza ili kufikia mafanikio hayo. Kushindwa sio mwisho wa safari bali ni sehemu ya kujifunza. Usiwasikilize wanaokukatisha tamaa na kukuambia huwezi.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo432