Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha YOU CAN WIN (UNAWEZA KUSHINDA)

Habari msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu, karibu tena katika wiki nyingine ya Kujifunza kutoka kwenye kitabu cha wiki. Wiki hii tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinachoitwa YOU CAN WIN (UNAWEZA KUSHINDA) kilichoandikwa na SHIV KHERA. Kitabu hiki kinazungumzia jinsi gani unavyoweza kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako bila kujalisha umetokea wapi au una umri gani. Ukifuata hatua zilizopo kwenye kitabu hiki kwa vitendo ni lazima utakua mshindi tu. Mwandishi anasema kwamba washindi hawafanyi vitu tofauti bali wanafanya vitu kwa utofauti. Yaani kilekile anachofanya mtu wa kawaida, mshindi anakifanya kwa njia ya tofauti. Mwandishi anaanza kwa kuzungumzia mtazamo (attitude) na umuhimu wake, lakini pia anaonyesha vitu vinavyowashikilia watu chini washindwe kupata mafanikio makubwa, na pia anatoa suluhisho ya vitu vya kufanya kuweza kutoka hapo ulipo na kufika juu. Kitabu hiki kina mambo mengi sana ya kujifunza, hapa nimechukua mambo 20 tu ambayo muhimu ambayo na wewe pia unaweza kujifunza.

 
Karibu tujifunze.
1. Asili ya mwanadamu ni kukataa au kupinga mabadiliko bila kujali madhara yake yatakuwa chanya au hasi. Hua tunajihisi kua na faraja kubakia katika hali zetu za sasa ambazo ni hasi, hata kama mabadiliko yataleta matokeo mazuri hatuko tayari kuyakubali.
SOMA; KITABU; Kurasa Za Maisha Ya Mafanikio, Toleo La Kwanza 2016.
2. Kama mtazamo wako ni hasi maisha yako yanakua kwenye kizuizi. Huwezi kufanikiwa huku ukiwa na mtazamo hasi, kwanza utakua na marafiki wachache na hata maisha huwezi kuyafurahia, Mtazamo wako ni kama dirisha la kioo unalotumia kuiona dunia, kama kioo cha dirisha lako ni kichafu, basi kila utakachokua unakiona nje utaona ni kichafu. Mtazamo unapokua hasi, ni kama kioo cha dirisha chako ni kichafu. Lazima uanze kusafisha kioo chako. Tengeneza mtazamo chanya na utaona mambo chanya yakikujia.
3. Watu wenye mtazamo hasi hua ni watu wa kukosoa siku zote, hata kama kitu kimefanyika vizuri namna gani. Ni wakosoaji hadi wanakua wataalamu wa kukosoa, Yaani wao ni kutafuta makosa tu, ni kama vile watapatiwa tuzo ya kukosoa. Utakutana na watu hawa maofisini hata majumbani mwetu. Unachopaswa kufanya ni kuacha kuambatana na watu wa namna hii maana hupenda kuwaambukiza wengine ili wawe kama wao.
Zipo hatua 8 za kuutengeneza mtazamo chanya.
4. Hatua ya Kwanza: Badilii Focus yako, badala ya kutazama upande hasi, basi anza kuangalia upande chanya kwenye kila jambo au watu. Unapaswa kua mtafuta mazuri. Tazama mazuri ya mtu na sio yale mabaya. Change Focus, Look for Positive
5. Hatua ya Pili: Acha kuahirisha mambo (procrastination). Kuahirisha mambo hupelekea mtu kutengeneza mtazamo hasi. Tabia ya kuahirisha hukupunguzia nguvu zaidi, kuliko juhudi ambayo ungeweka kumaliza hiyo shughuli. Kazi ukiimaliza unahisi mwenye nguvu zaidi, ila kazi isipokamilika hukuondolea nguvu na kujihisi mchovu. Watu wengi wanaotoka makazini mwao wakiwa wamechoka wanakua hawajamaliza kazi zao.
6. Hatua ya Tatu: Tengeneza mtazamo wa Shukrani. Hesabu baraka zako badala ya kuhesabu matatizo uliyonayo. Kuwa mwenye shukrani hata kama ni kidogo ulichonacho. Hata kama uko kwenye matatizo kiasi gani, ukijichunguza kwa makini utagundua unayo mambo mengi sana ya kumshukuru Mungu na hata wengine. Ukiwa kwenye tatizo, ukawa mtu wa kulalamika, haikusaidii kutoka hapo ulipo, badala yake utaendelea kujiumiza kwa mtazamo wako maana utaendelea kuona matatizo tu kila sehemu. Kulingana na Imani yako, ukiwa mwenye shukrani ina maana una imani kwamba pamoja na matatizo uliyonayo, kuna mengine mazuri ambayo Mungu amekujalia hata kama ni madogo lakini una imani pia kwamba anaweza kukutendea mazuri zaidi na kukusaidia kutoka hapo ulipo. Many of our blessings are hidden treasures; count your blessings and not your troubles.
7. Hatua ya nne. Kuwa mtu wa kujielimisha bila kukoma. Wengi huamini kwamba elimu rasmi (vyuo na vyuo vikuu) inatosha. Bahati mbaya kwenye shule zetu tunapata taarifa nyingi na kuiita elimu, kitu ambacho sio kweli. Elimu ya kweli ni ile inayokufunza akili yako na moyo wako. Kama utapata elimu ila tabia yako ikabakia vile vile basi ujue ulichopata ni taarifa tu na sio elimu. Watu huchanganya elimu na uwezo wa kukariri ukweli (facts). Ili kutengeneza mtazamo chanya tafuta maarifa yenye kukubadili akili yako na tabia zako. Jielimishe mwenyewe bila kukoma, tafuta vitabu vizuri au hudhuria semina mbalimbali. We need to compete for knowledge and wisdom and not for grades.
SOMA; Misemo Hii Mitano (5) Inaua Kabisa Ndoto Zako Za Mafanikio, Iepuke.
8. Lisha akili yako Kila siku. Kama ilivyo miili yetu inahitaji chakula kila siku, akili zetu pia zinahitaji mawazo mzuri (good thoughts) kila siku. Kama miili yetu tukiilisha vyakula visivyofaa ni ukweli usiopinga kwamba miili yetu itaugua. Hivyo hivyo akili zetu huugua zinapolishwa mawazo mabaya. Usipofanya juhudi kuilisha akili yako mambo mazuri, automatic akili yako itajilisha yenyewe vitu vibaya. Akili yako inakula kutokana na vitu unavyosikiliza, kuona na hata kusoma. Je unairuhusu akili yako kusikiliza nini muda mwingi kwenye redio au simu au hata marafiki. Ni marafiki gani unaokua nao na hua wanaongea nini? Je unaangalia nini kwenye TV au Computer au simu? We need to feed our mind with the pure and positive thoughts to stay on track.
9. Hatua ya Tano: Tengeneza heshima binafsi (self-esteem). Heshima binafsi ni jinsi unavyojihisi mwenyewe au jinsi unavyojiona ndani yako. Kama ukijihisi vizuri ndani mwako hata utendaji wako unakwenda juu, mahusiano yako yanakua bora kuanzia nyumbani hadi kazini, hata dunia unaiona nzuri zaidi. Sababu ni kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya jinsi tunavyojihisi wenyewe na tabia au mwenendo wetu. Kama unataka kutengeneza heshima binafsi chanya, njia ya haraka ni kufanya kitu kizuri kwa wale wasiokua na uwezo wa kukulipa. Unaweza kutoa msaada wa fedha au wa kujitolea kwa wengine ambao ni wahitaji. Unapowasaidia wengine bila kulipwa unajihisi vizuri, heshima binafsi inaongezeka. Givers have high self-esteem, positive attitude and they serve society.
10. Hatua ya Sita: Epukana au kaa mbali na Vishawishi hasi (negative influences). Vishawishi hasi vinaweza kua watu au marafiki wenye mtazamo hasi, ama vyombo vya habari vyenye habari hasi. Mfano unakuta watu wanaokuzunguka kila siku ni kuongea umbea tu kuhusu wengine, au kukuelezea habari mbaya mbaya tu mara za uchawi, kufumaniwa, ajali au habari za mapenzi tu. Yaani hakuna siku mnajadili mawazo (ideas) zenye kuwapeleka mbele. Kwenye vyombo vya habari, unakuta kila mara unasikiliza ajali, mara siasa chafu, mara vita, tena habari hizi unazisikia au kuziona asubuhi mchana na hata jioni. Hivi akilini mwako unadhani ni nini kinajengeka? Ni mtazamo hasi kuhusu dunia, watu au hali fulani. Stay Away from negative influences.
11. Hatua ya Saba: Jifunze kupenda vitu ambavyo vinahitajika kufanywa. Baadhi ya vitu vinahitaji kufanywa bila kujali tunavipenda au hatuvipendi. Mfano mama kulea mtoto wake haijalishi anapenda au hapendi anahitajika kumlea. Vipo vitu ambavyo kila mmoja wetu anapaswa kuvifanya bila kujali anavipenda au hapendi, lakini ni muhimu kuvifanya. Kutokuvipenda ndio hupelekea kuviahirisha au kuacha kabisa kuvifanya. Sasa chakufanya, angalia vile vitu vyote unavyodhani vimekua ni vya muhimu sana kwako lakini kila ukitaka kuvifanya unavipiga kalenda. Orodhesha vitu hivyo anza na kimoja kimoja, jifunze kukipenda, angalia uzuri wa shughuli hiyo, pata picha jinsi utakavyonufaika pale utakapokua umekifanya tayari. This may not always be fun, and may even be painful. But learn to like the task, the impossible becomes possible.
12. Hatua ya Nane: Ianze siku yako na kitu chanya. Soma au sikiliza kitu chanya wakati wa asubuhi. Baada ya kulala akili inakua imepumzika na kutulia vizuri. Tunapoamka akili yetu ya ndani (subconscious mind) inakua ipo tayari kupokea kitu cha kwanza asubuhi, kitu hicho ndicho kitakachoitawala siku yako nzima. Kwa bahati mbaya akili yetu hii (subconscious mind) hua haichagui, inaingiza kinachokuja. Unapoanza asubuhi yako na habari hasi, uwezekano ni mkubwa wa kukutana na mambo hasi siku nzima. Hivyo ni muhimu sana unapoamka kabla ya kukutana na watu anza kuipatia akili yako kifungua kinywa kizuri. Unaweza kusoma, kusikiliza au kuangalia vitu chanya vyenye kukuhamasisha. Start your day with something positive.
SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha Critical Thinking.
13. Mwanadamu amepewa Zawadi Kuu. Ukiangalia mwanadamu hawezi kupeperuka kama ndege, hawezi kukimbia kumzidi chui au duma, hawezi kupanda miti kwa haraka kama tumbili au ngedere. Mwanadamu hana jicho lenye uwezo mkubwa kama tai, wala hana meno na makucha makali kama Simba. Ukicheki mwili wa mwanadamu ulivyo hauna kinga au vitu vya kujilinda kama walivyo viumbe wengine. Hata mdudu mdogo tu anaweza kumuua mwanadamu. Lakini Mungu ni wa ajabu sana, akampatia mwanadamu zawadi kubwa sana. Zawadi kuu hiyo tuliyonayo wanadamu inayotutenganisha na viumbe vingine ni UWEZO WA KUFIKIRI. Kwa kutumia uwezo huo, mwanadamu anaweza kutengeneza mazingira yake ya kuishi wakati wanyama wao huchukuliana na mazingira (adapt) kama yalivyo. Uwezo wa kufikiri ndio unamsaidia mwanadamu kuumba au kutengeneza vitu ambavyo vinaweza kurahisi shughuli na kuboresha maisha yake. Cha kuhuzunisha ni kwamba wachache sana ndio wanaoweza kutumia zawadi hii hadimu kwa kiwango chake cha mwisho.
14. Maisha yamejaa machaguo (choices). Kila chaguo lina madhara yake chanya au hasi. Mfano unapochagua kula kupita kiasi ni kwamba unachagua kua na kiriba tumbo (obesity) au uzito uliozidi ambao hupelekea kupatwa na magonjwa mengi kama kisukari, shinikizo la damu, matatizo ya moyo n.k. Tuna uhuru wa kufanya uchaguzi, ila tukishachagua, uchaguzi tuliofanya ndio unaotudhibiti. Fanya uchaguzi sahihi.
15. Mafanikio hayapimwi kwa nafasi uliyofikia katika maisha, wala hayapimwi kwa vitu ulivyonavyo kama fedha, magari, nyumba n.k. Mafanikio ya kweli yanapimwa kwa vikwazo ulivyoweza kuvishinda. Nelson Mandela aliwahi kusema kwamba watu wasiyapime mafanikio yake kwa kutizama alikofika, bali kwa kutizama ni mara ngapi alijaribu akashindwa na kuinuka tena. Vile vile mafanikio hayapimwi kwa kujilinganisha na wengine bali unapaswa kujipima kwa kuangalia jinsi unavyofanya ukilinganisha na uwezo wako (potential) ulionao wa kufanya mambo. Kila mtu ana uwezo wake binafsi ambao ni mkubwa sana kutegemeana na kusudi mtu alilopewa, hivyo ukitumia wengine kama kipimo utakua hujitendei haki, maana yawezekana uwezo ulionao (Potential) ni mkubwa kuliko hao unaojilinganisha nao. Watu waliofanikiwa wengi wao walishindwa mara kadhaa, walianguka mara nyingi lakini wakapanda juu tena.
16. Mafanikio sio kitu kinachotokea kama ajali au kama bahati. Kunahitajikia maandalizi ya kutosha pamoja na tabia. Maandalizi ni kwa ajili ya kupata hayo mafanikio, tabia ndiyo itakayokufanya uendelee kuwepo kwenye mafanikio. Kila mtu anapenda kushinda, lakini watu wengi hawako tayari kutia juhudi na muda wa kujiandaa kushinda. Kwenye mafanikio bahati hutokea pale maandalizi yanapokutana na fursa, yaani fursa ikitokea unakua ulishajiandaa tayari, wewe ni kuitumia vizuri. Mafanikio yanahitaji kujidhabihu/kujitoa sana pamoja na kuweka nidhamu binafsi. Everything that we enjoy today is a result of someone’s hard work. There is no substitute for hard work.
17. Katika biashara matatizo mengi ni matatizo yanayohusu watu. Tukiweza kutatua matatizo ya watu wetu (wafanya kazi) basi matatizo ya biashara nayo yanatatulika. Mfano kuna hoteli moja hapa Mwanza hua ninapenda kwenda hasa mwisho wa wiki, hua napenda kwenda hapo Kujisomea kwa sababu pametulia na ni jirani kabisa na ziwa Victoria. Ila sasa wahudumu hua wanagombana na wateja mara kwa mara, wengine wanawajibu wateja jinsi wanavyotaka, yaani huduma kwa wateja ni mbovu. Kuna wakati wahudumu wao kwa wao wanajibizana hata mbele ya wateja. Sasa wateja wakipungua na mauzo yakishuka hapa unaweza kusema biashara ndio tatizo? Kwa bahati nzuri wiki hii nilifanikiwa kwenda tena hotelini hapo, na kulikua na kikao cha wafanyakazi wa hoteli hiyo. Walipata ugeni wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahotelini, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU). Viongozi hao walikua wamekuja kuwaelimisha wafanyakazi hao kuhusiana na wajibu wa chama hicho lakini pia kusikiliza kero zao. Kwa vile nilikua siko mbali sana nilisikia kila kilichokua kinaongelewa. Mfanyakazi mmoja akasema, kwamba mwajiri wao hawajali, akatolea mfano hata chakula kila siku wanapewa ugali kabichi, kitu kinachowafanya hata wakati mwingine kushinda bila kula kuliko kufululiza tu kula kabichi. Mwingine akadakia kabla mwenzake hajamaliza, akasema “yaani wakati mwingine unamhudumia mteja huku wewe hujala, unatamani hata chakula cha mteja”, Hapo unaweza kuona uhusiano kati ya huduma wanayotoa na jinsi wanavyojaliwa na mwajiri. Hii ni wazi kwamba wafanyakazi hawafurahii kazi yao na ndio maana hawawajali wateja. Jali wafanyakazi wako, na wao watawajali wateja wako.
18. Katika kuweka malengo, ni muhimu sana kuzingatia uwiano (balance). Watu wengi wanapoweka malengo hutizama fedha na vitu kama magari nyumba viwanja n.k Hebu jiulize ukipata fedha nyingi halafu afya yako ikawa ya mgogoro kisha ukatumia fedha hizo kwenda kujitibu utakua umefanya nini? Au ikitokea umefanikiwa kupata fedha nyingi lakini ndoa yako au familia imesambaratika kwa sababu ya kukosa muda wa kuilea kwa kuwa uko bize kutafuta fedha, hapo utafurahia maisha? Katika kuweka malengo hebu tanua mawazo yako yasitazame fedha peke yake. Weka uwiano, angalia swala la afya yako, weka malengo ya kuhakikisha unakua na afya njema. Weka malengo yanayohusu mahusiano yako na Mungu wako, mahusiano yako ya kifamilia (ndoa na watoto) na mahusiano yako na watu wengine. Weka malengo yanahusu kazi au biashara yako, Weka malengo yanahusu fedha. Pia waweza kuweka malengo binafsi. Hayo ni baadhi ya makundi muhimu katika kuweka malenga. Goals must be balanced.
SOMA; USHAURI; Mambo Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuacha Ajira Na Kuingia Kwenye Ujasiriamali.
19. Ukarimu ni lugha ambayo kiziwi anaweza kuisikia, na kipofu anaweza kuiona. Bora zaidi kumjali rafiki yako kwa ukarimu wakati yuko hai, kuliko kupeleka maua mazuri kwenye kaburi lake wakati ameshafariki. Kind words never hurt the tongue
20. Washindi wanaacha kumbukumbu zinazoishi (legacy) hata baada ya wao kuondoka. Hebu pata picha watu kama kina Abraham Lincoln, Mother Theresa, Patrice Lumumba, Bob Marley, Martin Luther King Jr., Alfred Nobel, Nelson Mandela, J.K Nyerere. Mahatma Gandhi, Isaac Newton n.k hadi leo watu hawa wanaishi japo hawapo nasi kimwili, dunia bado inawakumbuka na inatumia falsafa zao kwenye mambo mbalimbali. Je wewe baada ya kuondoka hapa duniani, utaiachia dunia kitu gani ambacho kitabakia kama historia yako? Kama tu watu wengi wanakufa wakati bado wanaishi, sasa wakishakufa kimwili si ndio wanasahaulika baada tu ya matanga? Bila kujali umri wako unaweza kuamua leo, kutengeneza historia yako unayotaka ikumbukwe baada ya wewe kuondoka hapa duniani. Ukishajua unataka dunia ikukumbuke kwa lipi, nenda mbele zaidi kwa kujua ni vitu gani unapaswa kufanya ili uweze kufikia hiyo hatua ya kukumbukwa kisha anza kuvifanyia kazi. Our greatest responsibility is to pass on a legacy that the coming generation can be proud of.
Asante sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: