Kila mmoja wetu anafahamu ni jinsi gani ilivyo muhimu kuweka malengo kwenye maisha. Na kila mtu anafikiria malengo atakayojiwekea kwa mwaka unaoanza. Pamoja na kwamba kila mwaka tunajiwekea malengo mbalimbali ila wengi wetu inatuwia vigumu sana kutimiza malengo tuliyojiwekea.

  Unaweza kuwa wewe ni mmoja wa watu ambao umefikia hatua ya kukata tamaa ya kujiwekea malengo kutokana na kushindwa kutimiza malengo uliyojiwekea miaka ya nyuma. Kila mwanzo wa mwaka unaweka malengo ukiwa na ari kubwa kwamba unakwenda kuyatimiza ila kati kati ya mwezi wa kwanza unakuwa umeshayasahau malengo yako. Kufika mwezi wa kumi na mbili unajisikia vibaya sana kwa kushindwa kufikia vile ulivyopanga.

Soma; Jinsi ya kuweka malengo utakayofikia.

  Watu wengi wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na makosa mbalimbali wanayofanya wakati wanaweka malengo yao. Hapa tutazungumzia makosa makubwa matano ambayo wengi wetu huwa tunayafanya wakati tunajiwekea malengo.

1. Unaweka malengo siku ya mwaka mpya.

  Watu wengi wanajikuta wanaweka malengo yao ya maisha siku ya sikukuu ya mwaka mpya(tarehe moja januari). Kuna ushawishi mkubwa unautufanya tuone siku hiyo ndio siku nzuri ya kuweka malengo. Tatizo kubwa la kuweka malengo siku hiyo ni kwamba tunakuwa tunafanya mambo kwa hisia zaidi ya kufikiri kwa kina. Tunakuwa na furaha ya kuuona mwaka mwingine na hivyo tunajikuta tunaweka tu mipango ambayo hatujafikiria kama tunaweza kuitekeleza. Hii ndio inayosababisha mtu kuyasahau malengo yake wiki ya pili ya mwezi januari.

  Tafuta siku utulie, uyatafakari maisha yako na uweke malengo yako, hata kama utafanya siku hiyo ya mwaka mpya hakikisha huendeshwi na hisia zozote.

0101

2. Huandiki malengo yako.

  Kusema ni rahisi sana, kuandika ni ngumu kidogo na kutenda ndio ngumu sana. Unafanya kosa kubwa sana kwa kutoandika malengo yako. Unaishia kuyasema tu, na kwa vile unakutana na mambo mengi kwenye maisha ya kila siku unajikuta unasahau ulichosema mwezi uliopita. Hivyo ni muhimu kuandika kwenye kijitabu kila lengo unalotarajia kufikia. Kwa kuyaandika malengo yako unakuwa umejiweka kwenye deni la kutimiza ulichoandika.(soma; ni muhimu sana kuandika)

3. Huweki muda wa ukomo wa kufikia malengo yako.

  Kitu chochote ambacho hakijawekewa mwisho ni vigumu sana kukitekeleza. Ndio maana sehemu yoyote unayofanya maombi unawekewa tarehe ya mwisho ya kufanya maombi hayo iwe ni maombi ya kazi, masomo na kadhalika. Kama malengo yako hutayawekea tarehe ambayo inabidi uwe umeyatekeleza itakuwa vigumu sana kwako kuyafikia. Kwa kuweka muda wa ukomo utajikuta unafanya juhudi za makusudi ili kukamilisha malengo kabla ya muda kuisha.

  Ni muhimu sana kuweka ukomo kwenye malengo yako, kama unasema mwaka ujao nanunua gari ni vyema useme mwezi na tarehe ambayo utakuwa umeshafanya ulichopanga.

4. Huyaelezi malengo yako vizuri na huweki mpango wa kuyafikia.

  Kusema nitanunua gari mwaka huu ni kitu kipana sana ambacho hakiwezi kukusukuma ili kutimiza. Ila ukisema(na kuandika) utanunua gari ya aina gani na utafanya nini ili uweze kununua gari hilo inakuwa na maana kubwa na inakusukuma kufikia lengo hilo.

  Usiweke malengo bila ya kueleza ni kitu gani hasa unataka na ni vitu gani unahitaji kufanya ili kufikia malengo yako. Eleza kila unachotaka kupata kwenye malengo yako na vitu ambavyo unahitaji kufanya ili kufikia malengo yako. Ni muhimu kuwa na mpango wa kufikia malengo unayojiwekea la sivyo utashindwa kuyafikia.

5. Huyapitii malengo yako mara kwa mara.

  Haitoshi tu kuandika malengo na kisha kuhifadhi kitabu ulichandikia na kuendelea na maisha yako kama kawaida. Ni muhimu sana kuwa na utaratibu wa kupitia malengo yako mara kwa mara. Weka utaratibu wa kupitia malengo yako kila mwezi, waweza pia kufanya kila wiki au hata kila siku. Jinsi unavyopitia malengo yako mara nyingi ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kujua kama upo kwenye njia sahihi ya kuyafikia na ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kuyafikia. Kama utayaandika na kuachana nayo ni vigumu sana kujua unakoelekea na ni vigumu kuyafikia.

 

  Acha kurudia makosa haya unayofanya kila mwaka wakati wa kuweka malengo. Ufanye mwaka 2014 kuwa wa tofauti na kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

  Tarehe 18/01/2014 itafanyika semina ya kuweka malengo na kubadili maisha dar es salaam. Kama bado unashindwa kuweka malengo na kuyafikia, utajifunza kwenye semina hii. Pia utajifunza jinsi ya kuchukua hatua juu ya maisha yako na uwe na maisha bora. Kama utahitaji kuhudhuria semina hii tafadhali bonyeza maandishi haya kisha ujaze fomu fupi itakayotokea. Ufanye mwaka 2014 kuwa mwaka wa mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, anza kwa kuhudhuria semina hii.

  Nakutakia kila la heri katika harakati zako za kuyabadili maisha yako na ya wanaokuzunguka. Tuko pamoja.