Linapokuja swala la uwekezaji duniani, jina Warren Buffet huwa halikosekani. Ni mmoja wa wawekezaji wenye mafanikio makubwa sana. Kwa miaka kadhaa amewahi kuwa tajiri namba moja duniani na kwa miaka zaidi ya 20 iliyopita, amekuwa kwenye tano bora ya matajiri wakubwa duniani.

Warren Buffett ni mmoja wa matajiri wachache ambao utajiri wao unatokana na uwekezaji kwa sehemu kubwa. Matajiri wengine wengi, utajiri wao unatokana na teknolojia au uzalishaji, lakini Buffet amekuwa na mafanikio makubwa kupitia uwekezaji.

Warren Buffet amekuwa kwenye uwekezaji kwa zaidi ya miaka 70 sasa, alianza uwekezaji wake wa kwanza akiwa na miaka 13 pekee, akaendelea kujifunza na kuwekeza na mpaka sasa ni mwenyekiti wa kampuni kubwa na yenye mafanikio kwenye uwekezaji inayoitwa Berkshire Hathaway, kampuni kubwa inayojihusisha na uwekezaji na kumiliki biashara nyingi.

Kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya maisha, watu wanaofanikiwa, kuna vitu wanavifanya tofauti na wanavyofanya wengine. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa Warren Buffett, yapo mambo anayoyafanya, ambayo ni tofauti kabisa na wawekezaji wengine, na haya ndiyo yamempa mafanikio makubwa.

Mwandishi Robert Hagstrom anatushirikisha mambo haya kupitia misingi 12 ambayo Buffet huwa anaifuata katika uwekezaji. Kwa kuijua misingi hii 12 na kuifanyia kazi, tunaweza kuwa wawekezaji bora na wenye mafanikio makubwa.
 
 

Kupitia uchambuzi huu wa kitabu nitakushirikisha misingi hii 12 ya uwekezaji inayotumiwa na Warren Buffet.

Lakini kabla hatujaanza uchambuzi wa kitabu hichi, Warren Buffett amekuwa akishauri watu wanaotaka kuwa wawekezaji bora basi wasome kitabu kinachoitwa THE INTELLIGENT INVESTOR. Anasema hichi ni kitabu kilichompa yeye misingi muhimu ya uwekezaji ambayo anaifuata mpaka leo.

Karibu kwenye uchambuzi huu tujifunze kwa pamoja na tuweze kuwa wawekezaji wenye mafanikio makubwa.

1. Watu wanne waliokuwa na ushawishi mkubwa kwa Warren Buffett.

Mafanikio makubwa kwenye uwekezaji ambayo Warren Buffett ameweza kuyatengeneza, yanachangiwa na mambo mengi. Moja ya mambo hayo ni watu ambao wamekuwa na ushawishi kwake. Wapo wengi, ila wanne wamekuwa na ushawishi mkubwa kwake, wamemfundisha na kumhamasisha sana kuwa mwekezaji bora.

Wa kwanza ni Benjamin Graham, mwandishi wa kitabu cha The Intelligent investor na aliyekuwa mwalimu wa Buffet, huyu alimfundisha jinsi ya kuchagua uwekezaji mzuri kwa kutumia akili na siyo hisia.

Wa pili ni Phil Fisher, huyu pia alikuwa mwalimu wake, alimfundisha jinsi ya kupanga uwekezaji wa muda mrefu, na kuchagua kampuni chache bora za kuwekeza badala ya kampuni nyingi za kawaida.

Wa tatu ni John Burr Williams ambaye alikuwa mwandishi wa jinsi ya kujua thamani ya uwekezaji, na hilo ndilo Buffet alijifunza kwake.

Wa nne ni Charles Munger, huyu ni makamu mwenyekiti wa kampuni ya Berkshare, ambaye amekuwa mshirika wa uwekezaji wa Buffet kwa zaidi ya miaka 50 sasa. Wamekuwa karibu na kila kitu wanafanya kwa kushirikiana.

Kuwa bora kwenye jambo lolote, unahitaji kuwa na watu ambao wanakufundisha na hata kukupa hamasa ya kupiga hatua zaidi.

2. Sheria kuu mbili za uwekezaji.

Warren Buffett anasema zipo sheria kuu mbili za uwekezaji ambazo amejifunza kutoka kwa Benjamin Graham, ambazo anazifuata mpaka leo.

Sheria ya kwanza ni usipoteze fedha unayowekeza.

Sheria ya pili ni usisahau sheria ya kwanza.

Katika kuwekeza, lazima ufanye kazi yako vizuri, kwa kufanya utafiti wa kina na kupata uhakika kwamba fedha unayowekeza haiendi kupotea. Unahitaji sana kulinda mtaji wako. Hili limemwezesha Buffett kufanikiwa sana kwenye uwekezaji.

3. Hisia siyo rafiki wa uwekezaji.

Warren Buffet amekuwa anasema mara kwa mara ya kwamba, ukifanya maamuzi ya uwekezaji kwa hisia, lazima utapata hasara. Lakini bado kila siku watu wanafanya maamuzi ya uwekezaji kwa hisia.

Zipo hisia kuu mbili zinazowasukuma watu kwenye uwekezaji;

Hisia ya kwanza ni tamaa ya kupata zaidi. Hapa watu wanasukumwa kuwekeza kwa kuona watapata faida kubwa sana, wanakimbilia kununua uwekezaji, bei ya uwekezaji huo inapanda na kujikuta wanatumia fedha nyingi kuliko uhalisia.

Hisia ya pili ni hofu ya kupoteza. Pale uwekezaji unapokuwa unashuka thamani, watu huhofia kupoteza mtaji waliowekeza na hivyo kukimbilia kuuza. Kadiri wengi wanavyouza, ndivyo bei ya uwekezaji inashuka na wanauza kwa hasara.

Warren Buffet anachotuambia ni tuende kinyume na hisia hizo mbili, wakati kila mtu anakimbilia kuuza, basi wewe nunua, na pale kila mtu anakimbilia kununua wewe uza. Usiruhusu hisia zikutawale na ushindwe kufanya maamuzi sahihi kwenye uwekezaji.

4. Wekeza kwenye vitu na maeneo ambayo unayajua vizuri.

Warren Buffett ana kitu anaita Circle Of Competence, huu ni mduara wa yale maeneo ambayo anayafahamu kwa kina, na hayo tu ndipo anapowekeza. Mara zote amekuwa anawekeza na kununua biashara ambazo anaelewa vizuri mfumo wake wa biashara. Hizi ni zile biashara ambazo anajua historia yake vizuri na anaweza kutabiri zaidi ya miaka mitano ijayo kwenye biashara hizo.

Wawekezaji wengi wamekuwa wakipoteza kwa kuwekeza kwenye maeneo ambayo hawayajui vizuri. Wanakimbilia kununua ili kupata faida, lakini mara nyingi wanapata hasara.

Msimamo huu wa Buffett umempa hasara, kwa mfano hajawahi kuwekeza kwenye kampuni yoyote inayohusu teknolojia, na hii ni kwa sababu haelewi vizuri na kwa undani mfumo wa biashara zinazohusu teknolojia na hawezi kutabiri miaka mitano ijayo kwenye kampuni za aina hiyo. Hivyo hata kwa makampuni ambayo yamefanya vizuri, hajaweza kuwekeza. Lakini pamoja na kukosa makampuni hayo mazuri, bado msimamo wake umemwokoa asipate hasara ambazo wawekezaji wengi wamekuwa wanapata kwa makampuni ya teknolojia yanayokufa haraka.

Wekeza kwenye maeneo ambayo unayajua vizuri na unaweza kuyafuatilia.

5. Sifa mbili za uwekezaji mzuri.

Kupitia Benjamini Graham, Buffet amejifunza sifa mbili za kuangalia kwenye uwekezaji anaotaka kufanya ili kujua kama ni mzuri au la.

Sifa ya kwanza ni usalama wa mtaji anaowekeza. Je mtaji utakuwa salama? Hapa utakumbuka zile sheria mbili, ambapo kikubwa ni usipoteze mtaji wako.

Sifa ya pili ni marejesho mazuri. Kwa kila kiasi cha fedha unachowekeza, je ni faida au riba kiasi gani ambayo unapata? Unahitaji kuwekeza maeneo ambayo yana marejesho mazuri kwa faida au riba.

Ukitumia sifa hizi mbili katika kuchagua uwekezaji, utaweza kupata uwekezaji bora sana kwako.
 

6. Unahitaji kuwekeza maeneo machache mazuri.

Watu wengi wamekuwa wanakazana kufanya uwekezaji kwenye maeneo mengi, na mengi yanakuwa kawaida hivyo hawanufaiki sana.

Warren Buffet, kupitia mwalimu wake Fisher, amejifunza kuchagua maeneo machache ya kuwekeza ambayo ni mazuri hasa na yanampa faida kubwa.

Ukichagua kampuni au biashara chache ambazo zinaendeshwa vizuri na kufanya vizuri, utanufaika sana na kuondokana na changamoto nyingi.

7. Zingatia sana misingi ya biashara kwenye uwekezaji.

Moja ya kitu ambacho kimewawezesha Warren Buffett na Charlie Munger kuweza kushirikiana kwenye uwekezaji kwa muda mrefu, ni kupenda kwao kusimamia misingi sahihi ya biashara. Wamekuwa ni watu ambao hawatafuti njia ya mkato katika kufanikiwa. Hata katika miaka ambayo makampuni makubwa yalikuwa yanapata kashfa ya kupika mahesabu, wao walizingatia misingi sahihi ya biashara katika kampuni yao na hata kwenye biashara wanazowekeza au kununua.

Uaminifu ni kitu ambacho wanakiangalia na kukitukuza sana, na umewawezesha kuwa na mafanikio makubwa bila ya kuchafuliwa majina na sifa zao.

8. Tumia muda mwingi kuchunguza na kutafiti kampuni kabla ya kuwekeza.

Siri kubwa ya Warren Buffett ni kwenye kufanya utafiti. Warren amekuwa akinukuliwa akisema asilimia 80 ya muda wake anautumia kusoma ripoti za biashara na makampuni mbalimbali. Kabla hajawekeza au kununua biashara, Buffett huhakikisha anaijua biashara nje ndani, huwa anasoma ripoti za kampuni husika, halafu anasoma ripoti za kampuni shindani, halafu anasoma magazeti na machapisho yanaandikaje kuhusu kampuni hiyo. Anatumia kila njia kuhakikisha ana taarifa sahihi kabla hajawekeza.

Mwanafunzi mmoja amewahi kumwuliza Warren Buffett afanye nini ili na yeye awe mwekezaji mwenye mafanikio kama Buffett, Buffett alishika karatasi akamwambia soma kama hizi 500 kila siku.

9. Warren Buufett siyo mwekezaji tu, bali pia ni mwamuzi kwenye biashara.

Japokuwa kwa nje watu wengi humwona Buffet kama mwekezaji kwa kununua hisa za makampuni mbalimbali, Buffet anaenda mbali zaidi. Huwa haishii kuwa mwekezaji tu kwa kununua hisa na kusubiri mambo yaende vizuri. Badala yake amekuwa anaangalia makampuni mazuri, ambayo hayaongozi vizuri, ananunua hisa nyingi na hilo linampa nafasi ya kuwa mwamuzi kwenye kampuni hiyo. Anamiliki kampuni hiyo na kuweka uongozi mzuri ambao unaiwezesha kampuni kufanya vizuri na hivyo kupata faida kubwa kuliko kutegemea faida ya hisa pekee.

Pia kampuni yake imekuwa inanunua biashara nyingi na kuzimiliki kwa silimia 100, pamoja na kuwa na makampuni ya bima ambayo yamemwezesha kuwa na mtaji mkubwa wa kuwekeza. Ambacho amekuwa anafanya ni kuuza bima kubwa, kisha kutenga sehemu ya fedha kwa ajili ya kufidia na ile inayobaki anaiwekeza.

10. Uwekezaji ni biashara.

Warren Buffett amekuwa akiangalia kila uwekezaji anaoufanya kama biashara. Hivyo hutumia vigezo vyote vya kibiashara katika kufanya maamuzi ya uwekezaji. Huhakikisha anaelewa uwekezaji vizuri, anaona ukuaji wake na usalama wa mtaji anaowekeza. Pia anaendelea kuyafuatilia makampuni kwa karibu baada ya kuwekeza, ili kujua wakati gani sahihi wa kutoka au kuendelea kuwepo kwenye uwekezaji huo.

Watu wengi huchukulia uwekezaji kama kitu cha kufanya mara moja na kusahau, hilo huwapelekea kupata hasara kubwa.

MISINGI 12 YA UWEKEZAJI AMBAYO ANAITUMIA WARREN BUFFETT.

11. Msingi wa kwanza; biashara rahisi na mfumo unaoeleweka.

Warren Buffet amekuwa akiwekeza kwenye biashara ambazo ni rahisi na mifumo yake inaeleweka kwa urahisi. Amefanya hivi kwenye makampuni kama Coca Cola, ambayo ni kampuni ya vinjwaji, Gillette ambayo ni kampuni ya viwembe, Well Fargo ambayo ni benki na nyingine za aina hiyo. Amekuwa anaepuka sana mifumo ya biashara ambayo haielewi, hata kama wengine wanapata faida kubwa.

Msingi huu umemsaidia kuepuka hasara za uwekezaji ambazo wengi wamekuwa wanapata, hasa pale makampuni mapya yanapokufa au kupata hasara na kufilisika.
 
12. Msingi wa pili; historia ya ufanisi wa biashara.

Warren pia huwa anaangalia historia ya ufanisi wa kampuni kabla hajawekeza au kununua. Anachukua muda na kupitia hesabu za kampuni kwa miaka mingi ya nyuma, kuangalia ufanisi wake, na namna inavyoongozwa. Hii ndiyo sababu huwa anaepuka sana kuwekeza kwenye makampuni mapya ambayo hana historia yake.

13. Msingi wa tatu; mipango ya muda mrefu ya biashara.

Kitu kingine ambacho Buffett anakiangalia kwa karibu sana ni mipango ya muda mrefu ya kampuni na uwezo wa kampuni kuwepo kwa miaka zaidi ya mitano ijayo.

Warren Buffet amekuwa hawekezi kwenye kampuni ambayo hawezi kuiona kwa zaidi ya miaka mitano ijayo. Kwa mfano kwa Coca Cola anasema watu wataendelea kupata vinywaji baridi kila siku, hivyo uongozi ukiwa mzuri, kampuni itaendelea kukua.

14. Msingi wa nne; ubora wa uongozi.

Hili ni eneo muhimu sana ambalo huwa analiangalia kwa karibu, na ndipo anapopatumia kufanya maamuzi sahihi. Huwa anaangalia maamuzi ambayo uongozi wa kampuni unafanya. Ikiwepo namna fedha zinavyotumiwa na uwekezaji unavyofanywa.

Kwa mfano kampuni inatumiaje fedha za wawekezaji? Na je kampuni inapopata faida, inawanufaishaje wawekezaji? Je inawapa gawio au inaongeza thamani ya hisa? Mara zote amekuwa anapendelea kampuni zinazotoa gawio, japo kampuni yake binafsi haitoi gawio kwa wawekezaji wake.

15. Msingi wa tano; uaminifu wa uongozi.

Warren Buffet anasema kwamba, katika kufanya kazi na mtu huwa anaangalia vitu vitatu, uaminifu, akili na nguvu, lakini kama cha kwanza (uaminifu) hakipo, basi hivyo viwili vitakumaliza.

Amekuwa akijali sana uaminifu. Anaamini uongozi wa kampuni ambao unasema ukweli hata kama mambo ni mabaya, ndiyo unaofaa kuwekeza na kufanya nao kazi. Anakataa kuwekeza kwenye makampuni ambayo mambo muhimu yanafichwa na wawekezaji hawawezi kuyajua.

16. Msingi wa sita; uongozi na mwenendo wa biashara.

Warren Buffett amejifunza kitu kimoja kwenye biashara na uwekezaji, kwamba uongozi wa makampuni mbalimbali huwa na tabia ya kufanya yale ambayo makampuni mengine yanafanya. Hii huwa inapelekea makampuni kuwa na matokeo ya kawaida na kukosa fursa nyingi.

Buffet amekuwa anaangalia kampuni ambazo viongozi wake wanafanya maamuzi yao wenyewe na siyo kuangalia wengine wanafanya nini na kuiga.

17. Msingi wa saba; marejesho kwenye mtaji uliowekezwa.

Warren Buffett amekuwa anaweka mkazo sana kwenye faida ambayo mtu anapata kwa kila kiasi cha fedha ambacho anawekeza. Na siyo tu kuangalia ukuaji wa kampuni au mzunguko wa fedha, yeye anaangalia kila mwekezaji anatengeneza kiasi gani?

Hichi ni kipimo muhimu cha kujua faida hasa ambayo mtu anaipata.
 

18. Msingi wa nane; kipato ambacho wamiliki wanatengeneza.

Warren Buffet pia amekuwa akiangalia sana viongozi na wamiliki wa kampuni wanatengeneza kipato kiasi gani na kujilipa kiasi gani. Hapa pia huangalia uhalisia wake na faida ambayo wawekezaji wanapata. Kama viongozi na wamiliki wanatengeneza kipato kikubwa na wanahisa hawapati faida nzuri, huo siyo uwekezaji mzuri.

19. Msingi wa tisa; kiasi cha faida inayotengenezwa.

Watu wengi wanapoangalia kampuni au biashara ya kuwekeza, huishia kuangalia mapato ya biashara husika. Kama mapato ni makubwa basi ni ishara kwamba biashara inafanya vizuri.

Warren Buffett amekuwa anakazana kuangalia eneo moja muhimu, je ni kiasi gani cha faida ambacho biashara inatengeneza? Na hapa amekuwa anaangalia eneo moja muhimu sana, namna gani biashara inapunguza na kudhibiti matumizi.

Warren Buffet amekuwa ananukuliwa akisema kampuni ikitangaza kwamba inaanza mpango wa kupunguza gharama, hiyo siyo kampuni makini, kampuni yoyote makini inapaswa kuwa na mpango wa kupunguza gharama unaofanya kazi kila siku.

20. Msingi wa kumi; thamani iliyozalishwa kwa kila dola moja iliyowekezwa.

Warren Buffett amekuwa anaangalia kigezo kimoja muhimu kwenye ufanisi wa kampuni katika fedha, kila dola moja iliyowekezwa, kampuni iweze kuzalisha thamani ya dola moja zaidi sokoni. Kama kampuni haiwezi kuzalisha thamani ya aina hiyo, siyo uwekezaji mzuri.

21. Msingi wa kumi na moja; thamani ya kampuni.

Kabla ya kuwekeza kwenye kampuni yoyote, Warren Buffett huwa anatafuta kwanza thamani ya kampuni hiyo. Na kanuni anayotumia kutafuta thamani siyo mapato ya mwaka kama wengi wanavyotumia, bali yeye huangalia mapato yote ya kampuni kwa kipindi chote ambacho atawekeza. Kama anapanga kuwekeza kwa miaka kumi, basi anaangalia mapato ya kampuni hiyo kwa miaka kumi ijayo. Hii ndiyo thamani halisi ya kampuni.

Hapo anahitaji kuangalia vigezo mbalimbali na mwenendo wa uchumi. Japo haiwezi kuwa sahihi kwa asilimia 100, huwa anapata picha ya kumwezesha kufanya maamuzi sahihi.

22. Msingi wa kumi na mbili; kununua kwa bei ya punguzo.

Kwa kiasi kikubwa, Warren Buffett hununua hisa au kampuni ambayo ameshajua thamani yake halisi, lakini inauzwa kwa bei ya punguzo. Na punguzo yale hulenga theluthi moja ya thamani halisi. Yaani kama thamani ni elfu moja, basi huwa tayari kununua iwapo inauzwa kwa mia sita mpaka mia saba.

Kwa njia hii, hata pale thamani inaposhuka, bado anakuwa upande wa faida kwa kiasi kikubwa. Lakini akinunua kwa bei ambayo ni sawa na thamani, thamani inaposhuka anakuwa amepoteza.

23. Msingi mkuu wa uwekezaji tunaoweza kujifunza kwa Warren Buffet ni huu;

Tafuta kampuni ambayo ni bora, inayoendeshwa na watu waaminifu na wenye uwezo mkubwa na ambayo inauzwa kwa bei ambayo ni ndogo ukilinganisha na thamani yake kisha uinunue au kununua hisa zake.

Ni msingi ambao unaonekana rahisi kusema kuliko kutekeleza, lakini ukifuata misingi 12 tuliyojifunza hapa, utaweza kufanya maamuzi mazuri sana katika uwekezaji.

Kama unataka kuwa mwekezaji bora, nakusihi sana usome kitabu hichi cha The Warren Buffett Way. Unaweza kukipata bure kabisa kwa kujiunga na kundi la Telegram la AMKA MTANZANIA, bonyeza maandishi haya kujiunga.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,