Rafiki yangu mpendwa,
Pale maisha yetu yanapokuwa hayaendi vile tunavyotaka yaende, huwa kuna mahali tunakuwa hatujafanya sawa.
Na moja ya vitu ambavyo vinakwamisha maisha yetu kutokwenda sawa, ni kwenda kinyume na asili yetu sisi binafsi.

Kwa Falsafa ya Ustoa, asili yetu binadamu ni kufanya maamuzi kwa kufikiri. Hicho ndiyo kinachotutofautisha sisi binadamu na viumbe wengine wote.
Utagundua matatizo mengi kwenye maisha yako huwa yanaanzia kwenye kutokufikiri kwa usahihi. Ni pale unaposhindwa kufanya maamuzi yako kwa kufikiri ndiyo unaishia kufanya maamuzi mabovu kwako.
Ndiyo maana kwa falsafa ya Ustoa, dhambi ni kwenda kinyume na asili. Pale unapoenda kinyume na asili yako, unapofanya mambo ambayo hupaswi kufanya, ndiyo dhambi yenyewe.
Ubaya wa dhambi hii ya kwenda kinyume na asili, huwa inakuumiza wewe mwenyewe zaidi kuliko inavyowaumiza wengine. Kwa kufanya kinyume na asili yako, unayavuruga maisha yako wewe mwenyewe.
Kwenye maisha ya kawaida, watu wanaposikia dhambi, hufikiria ni kitu ambacho adhabu yake ni mpaka siku za mwisho. Lakini kwa falsafa ya Ustoa, dhambi ni chochote kinachokuzuia usiishi maisha yako ya hapa duniani kwa ubora.
SOMA; Tumia Falsafa Ya Ustoa Kuwa Na Fikra Sahihi Na Dhamira Safi.
Kuna dhambi nyingi za kwenda kinyume na asili yetu binadamu, lakini kuna kubwa nne ambazo wengi tumekuwa tunazifanya bila kujua na zimekuwa zinatukwamisha sana. Karibu ujifunze kuhusu dhambi hizo na hatua za kuchukua ili zisikukwamishe.
Moja ni kutenda kinyume na haki.
Pale unapoenda kinyume na haki, unatenda dhambi. Unapofanya chochote kwa kuvunja haki yako na ya wengine, unajiweka kwenye nafasi ya kuwa na maisha yenye changamoto zinazokukwamisha.
Kuepuka hili, mara zote fanya kile kilicho haki.
Mbili ni kusema uongo.
Kusema uongo ni dhambi ambayo imekuwa kikwazo kwa wengi kuwa na maisha bora. Kusema uongo kunampotosha msemaji na hata anayeambiwa. Hivyo wote wanaishia kuumia.
Kuepuka hilo, mara zote sema ukweli, kwa sababu ukweli ndiyo asili na unakuweka huru mara zote.
Tatu ni kutokutimiza wajibu wako.
Kama binadamu, kuna wajibu unao wa kutimiza hapa duniani. Kuna kusudi la wewe kuwa hapa duniani na unapaswa kulitimiza. Kuyaishi maisha yako kwa kukwepa kutimiza wajibu wako, ni dhambi. Unajipunja wewe mwenyewe na unawapunja wengine.
Kuepuka hilo, jua kusudi la maisha yako na liishi wakati wote. Usitafute njia za mkato za kuepuka kufanya kazi, weka kazi ukijua unatimiza wajibu wa wewe kuwa hapa duniani.
Nne ni kuendeshwa na hisia.
Kuendeshwa na hisia kwenye kufanya maamuzi ni dhambi kubwa, kwa sababu unafifisha uwezo wako mkubwa wa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Hisia zinapokutawala, huwa huwezi kufanya maamuzi sahihi na matokeo yake ni kupata matokeo mabaya.
Kuepuka hilo, hakikisha hufanyi maamuzi makubwa ukiwa umetawaliwa na hisia. Na pale unapokuwa na hisia, jizuie kuchukua hatua. Subiri hisia zitulie na fikra kurudi ndiyo uweze kuchukua hatua. Kwa kufanya hivyo utaepuka matatizo mengi.
Ukiacha kuchukulia dhambi kama kitu kinachoadhibiwa baadaye na kuona ni kitu kinachokwamisha maisha yako kuwa bora na ukachukua hatua sahihi, utaweza kuyaboresha sana maisha yako. Zingatia haya uliyojifunza hapa na utaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeshirikisha mafunzo mengine kutoka falsafa ya Ustoa na pia tumekuwa na mjadala mzuri juu ya somo hili. Karibu uendelee kujifunza, uwe imara na ufanye makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.