Napenda kukupa hongera sana wewe rafiki kwa hatua na juhudi mbalimbali unazoendelea kuchukua katika kuboresha maisha yako binafsi na jamii inayokuzunguka.  Ni ukweli kuwa hatua unazopitia katika kufikia malengo yako siyo rahisi kama wengine wanavyo kutazama. Kuna machozi, jasho na damu zilizotiririka kwenye mwili wako na bado ukaendelea mbele na kufika hapo ulipo sasa, hongera sana na endelea mbele zaidi hata kama wengine hawakuelewi wala kuthamini kile unachofanya, jiamini na ipo siku watakuelewa. Ukweli ni kwamba tofauti ya wewe na wao ipo katika kufikiri na kutenda, haiwezekani wote mkawa sawa ikiwa mtazamo wenu ni tofauti juu ya jambo moja linalohusu mafanikio.

Kumekuwepo na juhudi kubwa kwa kila mmoja wetu kuhakikisha anakuwa na nyumba nzuri na bora ili kukidhi mahitaji yetu ya kimakazi na biashara. Katika kufikia malengo yetu ya kuwa na nyumba bora, kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa ujenzi ambazo kwa namna tofauti zinatufanya baadhi yetu tujutie na kutofurahia juhudi zetu kutokana na kutofikia lengo halisi tofauti na tulivyotarajia. Changamoto nyingi zinazojitokeza zimetokana na makosa yetu ya kukosa maarifa muhimu ambayo yangetusaidia katika kufanya maamuzi sahihi na kufikia malengo kama tunavyotarajia. Leo nitazungumzia hatua tano muhimu unazopaswa kuzingatia kabla hujaanza ujenzi wa nyumba yako ili kuepuka baadhi ya changamoto ambazo ni rahisi kuepukika.

182df-majengo

Tengeneza Mpango Kazi Wa Ujenzi

Kuweka mpango kazi ni hatua ya awali kabla ya kuanza ujenzi wa nyumba yako. Hii ni hatua muhimu sana ambayo hutumika kama dira ya kila maamuzi yatakayofanyika na kutekelezwa wakati wa ujenzi. Katika kufikia lengo kuu la nyumba unayotaka kuijenga, ni muhimu sana ukatengeneza mpango kazi ambao utakuwa dira ya maamuzi na utekelezaji katika kufikia lengo kuu la ujenzi na aina ya nyumba uliyoitarajia. Mbinu gani zitatumika kwenye ujenzi wako, malighafi zitapatikana wapi, wajenzi watapatikana wapi, muda gani utatumika kukamilisha nyumba yako, ulinganifu wa makadilio na mchanganuo wa gharama za ujenzi, upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wajenzi, ulinzi na usalama wa malighafi, aina gani ya wajenzi wanaohitajika, mchanganuo wa malipo kwa wajenzi na gharama za ziada, mbinu za mawasiliano na usimamizi, haya na mengine mengi ni muhimu sana yakaainishwa mapema ili ujenzi unapoanza kila mshiriki aweze kufahamu na kutambua nini cha kufanya na wakati gani jambo fulani linapaswa kufanyika. Kutokuweka mpango kazi mapema kutakusababishia migogoro na migongano ya mawazo yasiyo na ulazima ambayo kwa namna tofauti yatakunyima furaha na amani katika kutimiza ndoto zako.

SOMA; Hizi Ndizo Mbinu Bora Za Kuepuka Majanga Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Mfahamu Mjenzi Wa Nyumba Yako

Wakati tulionao sasa ni wakati ambao mfumo wa soko huria ndio unaamua na kuathiri mbinu mbalimbali zitakazokusaidia namna ya kumpata mjenzi mahiri na mwenye uwezo usiotia shaka kuhusu kile unachokusudia kujenga. Si kila anayejitambulisha kuwa yeye ni mjenzi aliyebobea na wewe kweli ukaamini kwa kila alichokuelezea pasipo na shaka ya aina yoyote, utajiweka kwenye hatari usiyoijua, maneno na vitendo ni mambo mawili yenye utofauti mkubwa, umakini na umahiri wako wa kuchagua mjenzi ndio utakaokufanya ufurahie au uchukie maamuzi yaliyofanyika ikiwemo kujutia uchaguzi wako. Weka ulinganifu wa uadilifu, ubora, uzoefu, gharama, uaminifu, utashi binafsi, na uzingativu wa muda kama vigezo vya kufanya uchaguzi wa awali kwa mjenzi wako. Ni muhimu sana ukafahamu historia yake ya ujenzi kabla hujampa kazi yako. Nyumba yako si uwanja wa wajenzi kujifunzia, itakugharimu sana fedha na muda endapo hautakuwa makini kwenye maamuzi yako. Epuka migogoro isiyo na ulazima wakati wa ujenzi kwa kuainisha taratibu na makubaliano yako na mjenzi kabla ya ujenzi kuanza ili kila mmoja awajibike kwa nafasi yake kwa uhakika na ukamilifu.

Tengeneza Mpango Mkakati Wa Muda Na Fedha

Hii ni hatua muhimu sana ambayo haipaswi kupuuzwa hata kwa nukta, haijalishi kuwa utaweka sababu zote ulizonazo ili kubariki uzembe unaotokana na fedha au muda. Ni muhimu sana kuweka makadilio na mnyumbulisho wa gharama za ujenzi kabla ya kuanza rasmi ujenzi, ni vizuri ukawapata na kuzungumza na wauzaji mbalimbali wa malighafi, wasimamizi na wajenzi wako ili kuweza kujitathmini uwezo wako kifedha na muda wa kuweza kufanikisha ujenzi wako.  Hapa ndipo utakapoamua kuwa ujenge kwa hatua, uongeze au upunguze ukubwa wa nyumba, aina gani za malighafi utakazotumia, mbinu na zana gani za ujenzi zitakazo tumika wakati wa ujenzi, wakati mwingine utagundua kuwa unahitaji muda wa ziada ili kukamilisha baadhi ya mapungufu kabla hujaanza rasmi ujenzi.  Hatua hii itakusaidia kuepukana na ujenzi wa maboma badala ya nyumba, matumizi mabaya ya rasilimali fedha na muda, migogoro ya kimalipo na utendaji wa wasimamizi na wajenzi wako.

SOMA; Hatari Tatu Zinazoukabili Uwekezaji Wako Wa Majengo Na Namna Ya Kuepukana Nazo.

Weka Mkakati Wa Usimamizi, Ulinzi Na Usalama

Miongoni mwa changamoto kuu kwenye mradi wa ujenzi  ni haya mambo matatu ambayo ni usimamizi, ulinzi na usalama wa mali na watu kabla na wakati wa ujenzi. Ni kosa kufanya ujenzi bila usimamizi imara wenye uhakika, usimamizi bora na imara utakufanya ufanye maamuzi sahihi na bora wakati wote wa ujenzi na utafanikiwa kama ulivyotarajia katika kutimiza malengo yako ya kuwa na nyumba uipendayo. Mikakati madhubuti kuhusu ulinzi na usalama wa malighafi wakati wa ujenzi inapaswa kuwekwa mapema ili kudhibiti aina yoyote ya ubadhirifu na wizi. Tathmini sana usalama wa wajenzi wako, angalia changamoto zinazo hatarisha usalama wao na kuzitatua haraka sana. Tathmini huduma muhimu za kijamii kama zinawafikia kwa urahisi, waondoe haraka walevi, wezi, wasio waadilifu na waaminifu kabla hawajasababisha hatari ya aina yoyote. Kutokuweka mazingira mazuri wakati wa ujenzi ni kutengeneza changamoto nyingine zisizojulikana, uhifadhi wa malighafi hatari unapaswa kufuatwa kutokana na aina tofauti za mbinu za uhifadhi ili kuepuka madhara kwa wajenzi na kwenye nyumba.

Zingatia Sheria Na Taratibu Za Ujenzi

Zipo sheria, sera na taratibu mbalimbali zinazoratibu ujenzi hapa nchini ili kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinakidhi viwango halisi kwa matumizi husika, mipango miji na vijiji inazingatiwa, miundombinu haiathiriwi, uhifadhi wa mazingira unazingatiwa na usalama wa wajenzi wakati wa ujenzi. Jitahidi sana kupata nyaraka zote zinazopaswa na kufanya ujenzi wako kwa mujibu sheria na taratibu za eneo husika. Hii itakufanya ujenge nyumba yako pasipo na hofu ya aina yoyote, epuka sana ujenzi holela na usiofuata taratibu rasmi za ujenzi ili kuepukana na hatari zisizojulikana. Ni muhimu sana ukafanya utafiti na uhalali wa kila kinachofanyika au kuhitajika katika ujenzi wako ili kuepuka baadhi ya majanga yanayowakumba baadhi ya marafiki zetu. Ni vema ukawatembelea wataalamu na washauri wa ujenzi ili wakupe ushauri na muongozo rasmi utakao kuongoza kwenye mafanikio yako. Mafanikio ya kweli kwenye uwekezaji wa majengo ni wewe kuwa na amani na furaha wakati wote wa maisha yako.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

 

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com