Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Inapokuja kwenye mafanikio, watu wamekuwa wanaambiwa sana kuhusu ung’ang’anizi na kutokukata tamaa. Ni kauli nzuri na ambazo zinafariji sana, hasa nyakati zinapokuwa ngumu.

Lakini pamoja na uwepo wa kauli hizo nzuri za kutia moyo, bado watu hufika hatua na kuona hawawezi kuendelea tena. Watu wamekuwa wanafikia hatua ya kukata tamaa na kuiacha safari yao ya mafanikio.

Na kwa bahati mbaya sana, watu huwa wanakata tamaa wakiwa wamekaribia kupata matokeo mazuri. Wanakuwa wamevumilia vipindi vigumu kwa matarajio ya mambo kuwa mazuri, lakini muda unapokwenda bila mambo kuwa wanavyotegemea, wanashindwa kuendelea kuvumilia.

Wachache sana ambao wamekuwa wanavumilia na kuendelea kung’ang’ana mpaka kupata matokeo siyo kwamba wana tofuati sana na wengine. Wengi wanaoendelea licha ya magumu wanayokutana nayo ni wanakuwa hawana namna nyingine bali kuendelea. Kuacha inakuwa siyo moja ya machaguo waliyonayo.

Kwa walio wengi, wamekuwa wanajikuta kwenye mazingira ambayo wanashindwa kuendelea, licha ya kutamani sana kuendelea. Wanafika kwenye hatua hii kwa sababu kuna ukweli ambao wanakuwa hawajaujua kuhusu safari ya mafanikio.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujua ukweli huo ili uweze kubaki kwenye safari yako ya mafanikio bila kukatishwa tamaa na hali au kitu chochote kile.

1. Vitu Havitokei Tu.

Tulipokuwa watoto, tulikuwa tunadhani vitu huwa vinatokea tu. Tulipoangalia vitu vyote ambavyo vimetuzunguka, tulidhani vilitokea tu, tena kwa urahisi. Iwe ni majengo, mali na taasisi mbalimbali, tulidhani vimekuwepo hapo kama vinavyokuwepo vitu vingine kama milima, mito n.k.

Kwa fikra zetu za utoto, kila kitu ni rahisi. Na ndiyo maana hata mtoto mdogo anapoulizwa anataka nini au anataka kuwa nani, kutaja vitu vikubwa inakuwa ni rahisi kwao.

Tulipokua ndiyo tuligundua kwamba vitu havitokei tu, tulipata uelewa kwamba kuna watu walifanya vitu vinavyotuzunguka kutokea. Watu ambao walichukua hatua na kujenga vitu hivyo. Hii ni hatua katika utambuzi wetu, lakini bado haikutupa picha kamili.

Kujua kwamba vitu vilivyopo havijatokea tu bali vimejengwa na watu, bado haileti ukweli wote. Kwani tunaona ni rahisi kwa vitu hivyo kuletwa na tunaweza kuamini tunaweza kufanya zaidi ya kile ambacho kimefanyika.

Tukiwa watoto, tuliona yale ambayo wengine wameyajenga ni rahisi na sisi tunaweza kujenga zaidi ya hayo. Upande wa kuweza kujenga ni wa kweli, lakini upande wa rahisi siyo wa kweli kabisa.

Ni mpaka pale tunapojaribu kujenga vitu kama ambavyo vinaonekana ndiyo tunakutana na huo ukweli kwamba mambo siyo rahisi kama tulivyokuwa tunadhani. Na hapo ndipo ukweli kuhusu safari ya mafanikio unapojidhihirisha kwa wale wanaoijaribu.

2. Ni Mapambano Makali Kufanya Kitu Kutokea.

Tunapoona vitu kwa nje, tunaona kuvijenga ni rahisi. Ni mpaka pale tunapoingia kujenga ndiyo tunakutana na ukweli ambao hatukuwa tunaujua. Na ukweli huo ni kwamba kila kitu kinahitaji mapambano makali sana ndiyo kiweze kutokea. Hata kama kwa nje kitu kinaonekana ni rahisi kiasi gani, kwa ndani kuna kazi na mapambano makali sana yanayofanyika kukileta kwenye uhalisia.

Chukua mfano wa mtu aliyeanziasha biashara inayoonekana kwenda vizuri. Kwa nje unaweza kuona ni rahisi kuanzisha biashara kama hiyo na ukapata matokeo mazuri. Kwamba unahitaji kuwa na bidhaa/huduma na kuiuza kwa bei rahisi na utapata wateja wengi.

Lakini unapoingia ndani ndiyo unakutana na ukweli kuhusu mapambano ambayo mtu anakuwa amepitia mpaka biashara ikaweza kutokea. Mtu anakuwa amepambana sana kupata mtaji wa kuweza kuanza biashara. Huenda mtu alijinyima na kujenga akiba ambayo amekuja kuingia nayo kwenye biashara.

Alipoingia kwenye biashara, mwanzo alifanya makosa mengi. Aliweka bidhaa au huduma ambazo watu hawana uhitaji nazo, zikawa zimeshikilia mtaji kidogo alionao na hakuna na namna ya kuziuza. Wateja hawakuwa tayari kuja kununua kwake, licha ya kuweka bei ndogo kuliko washindani. Na hata wateja walipokuja mara moja, hawakurudi tena kununua, hivyo kila wakati ikawa ni kutafuta wateja wapya.

Kwa kutaka sana mafanikio, mtu aliendelea kung’ang’ana mpaka wateja wakaanza kuamini na kukubali kununua. Mauzo yakaanza kuonekana na kuhitaji wafanyakazi zaidi ili kuhudumia wateja vizuri. Lakini kupata watu sahihi nako kukawa kazi kubwa. Watu wakipatikana wanataka malipo makubwa ambayo biashara haiwezi kumudu. Wanaokubali malipo madogo wanaleta ubadhilifu kwenye biashara.

Bado mtu anang’ang’ana na kuendelea, anapata watu sahihi na wanaoleta matokeo mazuri. Na bado mambo hayapoi, mamlaka za kiserikali nazo zinaanza kutaka sheria ya taratibu zifuatwe. Hapo ni kuanzia kwenye mamlaka za kodi, leseni na vibali mbalimbali. Inahusisha gharama mbalimbali kuweza kutimiza taratibu hizo.

Hapo bado ushindani unaotoka kwa wengine, baada ya kuona matokeo yameanza kuwa mazuri. Bado kusumbuliwa na watu mbalimbali kwa sababu ya matokeo mazuri ambayo mtu unakuwa umeyapata. Bado magumu ambayo mtu anakuwa ameyapitia ya kufikia hatua za kukaribia kukata tamaa kwa kukosa fedha za kuendelea.

Kuna mengine magumu ambayo watu wanapitia na yanaweza yasionekane moja kwa moja. Mahusiano yanaweza kuathiriwa sana wakati mtu anakazana kujenga biashara. Afya ya mtu inaweza kuathirika sana na msongo wa kujenga biashara mpaka ikatokea. Na mtu anaweza kupoteza mali zake nyingi kwenye kukazana kujenga biashara yake.

Ukweli ni kwamba, licha ya urahisi wa kujenga kitu unaoonekana kwa nje, kwa ndani mambo ni tofauti kabisa. Kila kitu unachokiona, jua kimepambaniwa sana mpaka kutokea. Kuna watu wamejitoa kweli kweli, wakapambana hasa na ndiyo kikatokea.

Hakuna kitu chochote ambacho kimeweza kutokea kirahisi kama kinavyoweza kuonekana kwa nje. Ni muhimu sana kila mtu akajua hili, hasa kabla ya kuanza, ili kutokukata tamaa pale mambo yanapoonekana magumu kuliko yalivyotarajiwa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK144; Ukweli Mchungu Unaopaswa Kuujua Kuhusu Mafanikio Ili Usikate Tamaa Kamwe