Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Malengo ndiyo hatua ya kwanza ya kufika kwenye mafanikio yoyote unayoyataka. Hakuna mtu amewahi kupiga hatua kubwa bila kujua ni wapi anataka kufika na kupambana kufika hapo.
Pamoja na umuhimu huo mkubwa wa malengo, bado imekuwa ni mtego na kikwazo kikubwa kwa walio wengi. Wengi wamekuwa wanaweka malengo, makubwa na mazuri, lakini wamekuwa hawayafikii.
Mara nyingi, kila mwanzo wa mwaka watu wamekuwa wanaweka malengo ya nini wanataka kufanya na kupata kwenye mwaka huo. Wakati wa kuweka malengo hayo wanakuwa na moto mkubwa. Wanaweza hata kuanza kufanyia kazi malengo hayo. Lakini haiwachukui muda mrefu, wanakuwa wamerudi kwenye mazoea yao.
Wengi wamekuwa wanarudia zoezi la kuweka malengo kila mwanzo wa mwaka, lakini hawaendi mbali na malengo hayo. Wengine wamekuwa wanarudia malengo yale yale, lakini hakuna hatua ambazo wanapiga kwenye kuyafikia.
Tunachoweza kusema ni kwamba watu wengi wamechagua kuwa wajinga kwenye malengo. Hiyo ni kwa sababu ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile halafu kutegemea kupata matokeo ya tofauti. Ukiangalia jinsi ambavyo wengi wanaenda kwenye malengo, unaona wazi ni marudia yale yale ambayo yameshindwa.
Mimi rafiki yako sitaki ukwame kwa ujinga au sababu yoyote ile. Ndiyo maana nimekuwa nakushirikisha maarifa sahihi, ambayo ukiyafanyia kazi kwa vitendo, unapata matokeo.
Kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha kitu ambacho kimekuwa kinakukwamisha kufikia malengo ambayo umekuwa unajiwekea. Kitu chenyewe siyo rahisi sana kukigundua, kwa sababu siyo kitu kilicho wazi na kinachoweza kuonekana kwa wote.

1. Malengo Ni Ahadi Binafsi.
Tatizo la kutokufikia malengo linaanzia kwa watu kutokujua maana halisi ya malengo. Wengi wanapoweka malengo, wanachukulia kama ni kitu ambacho kitatokea baada ya kuwa wamekipanga. Hiyo ndiyo sababu ya wengi kuweka malengo na kujikuta wanarudi kwenye mazoea yao.
Maana halisi ya malengo ni ahadi binafsi ambayo mtu unakuwa umejiwekea. Ahadi inapowekwa, inapaswa kutimizwa ndiyo iweze kutokea, hivyo baada ya ahadi yoyote, utekelezaji unapaswa kufuata.
Lakini hivyo sivyo inavyokuwa kwa wengi wanapoweka malengo. Wengi huwa wanafurahia kuweka malengo makubwa na mazuri, bila kuangalia ni kwa namna gani wanaenda kuyageuza malengo hayo kuwa uhalisia.
Wapo ambao wanafurahishwa na ukubwa wa malengo yao kwa kuyaweka tu. Hawa huwa hawajisumbui kujua nini kinapaswa kufanyika ili malengo hayo yafikiwe.
Kinachofanya wengi wafurahie kuweka malengo hata kama hawajayafikia ni kufuata mkumbo. Pale watu wanapoona wenzao wameweka malengo, tena makubwa, na wao wanahamasika kuweka malengo pia. Wanafurahia tu zoezi la kuweka malengo, japo wanakuwa hawana mpango wa kuyafikia malengo hayo.
Kuondokana na kikwazo hiki cha maana ya malengo, unapaswa kujua malengo unayojiwekea ni ahadi kwako binafsi. Kutimia kwa malengo kunatokana na kutimiza ahadi hiyo unayokuwa umejiwekea mwenyewe. Kama wanavyosema kwamba ahadi ni deni, unapaswa kujua malengo unayojiwekea ni deni kwako binafsi.
2. Malengo Hayawekwi Mara Moja.
Kikwazo kingine cha kutofikia malengo ni kudhani malengo yanawekwa mara moja tu na kazi kuwa imeisha. Ndiyo maana mwanzo wa mwaka watu wengi wanaweka malengo, lakini mpaka mwezi wa kwanza unapoisha, wengi wanakuwa wameshaachana na malengo waliyojiwekea.
Hiyo ni kwa sababu waliweka malengo mara moja tu, tena kwa kujiambia na kazi ikawa imeishia hapo. Kwa jinsi watu walivyo na mambo mengi kwenye maisha yao, kuweka malengo mara moja na kuendelea na mambo mengine ni kujikwamisha kuyafikia.
Ili uweze kufikia malengo uliyonayo, unapaswa kuyaweka kila siku. Mwanzoni mwa malengo yako, unapaswa kurudia kuyaweka kila siku. Kila siku inakuwa ni siku mpya ya kujiwekea malengo uliyonayo. Na hapa siyo kwamba unabadili malengo, bali unayarudia malengo yale yale kila siku.
Ili iweze kuwa na nguvu, huishii tu kujiambia malengo hayo, bali unapaswa kuyaandika kabisa. Unapoandika kitu kwa mkono wako mwenyewe, unaiambia akili yako kwamba hicho kitu ni muhimu na kinapaswa kupewa kipaumbele.
Kuhakikisha huyasahau malengo yako na kurudi kwenye mazoea, unapaswa kurudia rudia kuyaweka malengo hayo kila siku. Kila siku rudia zoezi la kujiwekea malengo yako, kwa njia ya maandishi. Usiyazoee malengo uliyonayo, kila siku yaweke na jikumbushe ni ahadi yako na nafsi yako ambayo inapaswa kutimia.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK143; Hiki Ndiyo Kinachokukwamisha Kwenye Kufikia Malengo Unayojiwekea, Na Jinsi Ya Kukivuka