Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Huwa kuna kauli inayosema; ‘Mungu akikupa kilema anakupa na mwendo.’ Hiyo ni kauli inayoonyesha kwamba kwa kila mapungufu ambayo mtu anakuwa nayo, kuna namna anaweza kuyatumia kwa manufaa na upekee kwake.
Hili lipo kwenye maeneo yote ya maisha, hakuna upungufu ambao hauna mbadala wake na namna ya kutumia upungufu huo kwa manufaa. Lakini wengi wamekuwa wanakwama kwa sababu wanaangalia tu upungufu, hawahangaiki kuangalia upande wa pili wa upungufu huo, ambao una manufaa kwao.
Wengi wanasema wanataka kufanikiwa, ila wachache ndiyo wanaofanikiwa hasa. Ukiwauliza ambao hawajafanikiwa, moja kwa moja watakuambia kuhusu mapungufu waliyonayo. Watakuonyesha uwezo waliokosa wa kutumia fursa zilizopo ili kupata mafanikio.
Ukipokea majibu yao kwa haraka, unaweza kuamini ni kweli wamekwamishwa na mapungufu wanayokuwa nayo. Lakini ukipata muda wa kuyatafakari mapungufu hayo na ukaangalia upande wa pili, utaona fursa nzuri ambazo wameshindwa kuzitumia kupata mafanikio wanayotaka.
Hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa ambaye alianza akiwa na kila kitu alichokuwa anataka. Hakuna aliyeanzia kwenye ukamilifu ambao unaonekana kuhitajika kwenye mafanikio. Wote waliofanikiwa walikuwa na kila sababu ya kutokufanikiwa, walikuwa na kila aina ya mapungufu. Pamoja na hayo yote, bado walifanikiwa, kwa sababu walijua jinsi ya kutumia upande wa pili wa madhaifu waliyokuwa nayo.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza mwendo wa kipekee ulionao kwenye kilema cha mafanikio unachokuwa unaanza nacho. Madhaifu unayoona sasa yanakukwamisha kufanikiwa, yana upande wake mwingine ambao unaweza kuutumia kwa manufaa makubwa.

1. Mwendo Wa Kazi Kwenye Kilema Cha Kukosa Mtaji.
Ni kweli unaweza kuwa unakosa mtaji au pesa za kufanya kile ulichochagua kikupe mafanikio makubwa. Huenda umeona hicho ndiyo kilema chako, ambacho kimekuwa kikwazo kwako kupiga hatua.
Uzuri ni kwamba kilema hicho kina mwendo wake, ambacho ni mzuri kweli kweli. Ukiweka huo mwendo, watu watashukuru wewe kuwa na hicho kilema, kwa sababu utawapa burudani ambayo hawajawahi kuipata.
Mwendo wa kilema cha kukosa mtaji na pesa ni kazi. Kazi hapa ikimaanisha kutumia nguvu kama mbadala wa pesa. Pale pamapohitajika pesa ambazo wewe huna, weka nguvu. Angalia namna ambavyo unaweza kutumia nguvu zako kuleta matokeo ambayo yanahitaji fedha usizokuwa nazo.
Kukosa pesa, hasa pale unapokuwa unaanzia chini ni kitu ambacho wengi wanapitia. Wachache wanaokivuka na kupata mafanikio ni kwa kuchagua kuweka kazi kubwa sana ili kuvuka udhaifu huo wanaoanza nao.
Ikiwa unataka kufanikiwa na pesa huna, ni lazima uwe tayari kufanya kazi kama mtumwa. Ni lazima uweke kazi kubwa sana, kiasi cha wengine kukuonea huruma na kukuambia unajitesa. Hiyo ndiyo namna pekee ya kuvuka udhaifu wa kukosa pesa.
Huwa inanishangaza sana ninapokutana na wengi ambao hawajafanikiwa, na hawana pesa za kufika kwenye kile wanachotaka, ila pia wanatafuta njia ya mkato ya kufanikiwa ambayo haihusishi kazi. Huwa natikisa kichwa na kujiambia, hawa watu wanachekesha.
Wanaonishangaza zaidi ni wale wanaotaka mafanikio makubwa, hawana pesa za kuanzia, lakini pia wanataka wawe na maisha yenye mlinganyo. Wanakazana sana kuwa na mlinganyo kati ya kazi na maisha, kuhakikisha wanafaidi vyote. Kivipi yaani? Mlinganyo upi unakuwa unautaka unapoanzia chini?
Kama unaanzia chini kabisa na huna pesa ila unataka mafanikio makubwa, huna maisha. Wewe una kitu kimoja tu, ambacho ni kazi. Hicho ndiyo kinachopaswa kuwa kipaumbele pekee kwako. Ndiyo, haitakuwa sawa kwako na kwa wengine, lakini ndicho kinachohitajika ili ufanikiwe.
Kukosa pesa tayari ni kilema kwako, kuweka kazi kubwa sana hakuwezi kuwa kilema kingine, bali kunakuwa ni mwendo wa kipekee ambao utawavutia wengi. Jitoe kuweka kazi hasa, ndiyo njia pekee ya kupata matokeo makubwa unapokosa pesa unazohitaji kwenye kupata matokeo hayo.
2. Mwendo Wa Kujifunza Kwenye Kilema Cha Kukosa Elimu.
Kukosa elimu kubwa au kutokuwa na akili nyingi ni sababu nyingine ambayo watu wamekuwa wanaeleza kama kikwazo kwao kupata mafanikio makubwa. Wapo ambao mazingira yaliwazuia kupata elimu ambayo walitamani sana. Na wapo ambao walipata fursa lakini wakaichezea.
Wanapokaa na kujitafakari, wanaona kabisa kwamba kama wangepata elimu kubwa, au kama wangekuwa na akili nyingi, basi wangekuwa wamepiga hatua kubwa. Wanapoangalia mambo yote ambayo wameshahangaika kuyafanya, wanaona wazi kwamba wamekuwa wanarudia makosa yale yale na kuishia kujikwamisha.
Kukosa elimu au akili nyingi kunaweza kuonekana ni kilema, lakini kuna mbadala wake, mbadala ambao ni wa uhakika mno kwenye zama tunazoishi sasa. Mbadala huo ni kujifunza. Kwa zama tulizopo sasa, kila mtu anaweza kupata elimu ya aina yoyote ile anayoitaka, tena bila ya gharama yoyote.
Kipindi cha nyuma elimu ilikuwa na gharama, mpaka kukwa na usemi kwamba; ‘ukiona elimu ni ghali, jaribu ujinga.’ Lakini kwa zama hizi, elimu siyo ghali tena, elimu ni ya bure kabisa, lakini bado wengi wanahangaika na ujinga.
Kama kuna watu unaoona wamepiga hatua kuliko wewe na ukaona ni kwa sababu wao wana akili nyingi na wewe huna, ni kwa sababu tu hujaamua kujifunza. Hata kama unaona akili zako ni ndogo kiasi gani, ukijifunza, utaweza kufanya mengi wanayofanya wengine.
Na kama umekuwa unakazana sana lakini bado unakwama pale pale, ni kwa sababu kuna vitu ambavyo bado hujavijua. Ukichukua hatua ya kujifunza vitu hivyo, utaweza kuvuka pale ambapo umekuwa unakwama.
Kila mtu huwa anaanzia kwenye kilema cha ujinga, kwa sababu kuna vitu vingi anavyokuwa hajui. Na hata kwa wale wanaoonekana wamepiga hatua, bado kilema cha ujinga kipo ndani yao.
Mwendo wa kujifunza ni kitu ambacho kila mtu anapaswa kufanya kwenye maisha yake yote. Ujinga ni kilema cha kudumu, kadiri mtu unavyopiga hatua ndivyo unavyogundua vitu vingi ambavyo hukuwa unavijua. Kujifunza kunapaswa kuwa mwendo ambao unajulikana nao kwenye maisha yako. Kamwe usifike mahali na kuona tayari unajua kila kitu au hakuna kitu kipya cha kujifunza.
Siku unayoacha kujifunza ndiyo siku kilema cha ujinga kinakuondoa kabisa kwenye mafanikio unayojenga. Kilema cha ujinga ni kibaya sana, kwani kinaweza kuangusha kila kitu ambacho mtu umeshajenga.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK142; Tumia Huu Mwendo Wa Kilema Kujenga Mafanikio Makubwa Licha Ya Mapungufu Uliyonayo