Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwenye maeneo matatu ambayo tumechagua kuyapa umakini mkubwa kwenye safari yetu ya mafanikio, eneo la biashara ndiyo limekuwa halieleweki na wengi. Hiyo ni kwa sababu kila anayenunua na kuuza na kupata faida, tayari anaona amefanikiwa kwenye biashara.
Lakini pale anapopata changamoto binafsi na ikamzuia kutekeleza majukumu aliyonayo kwenye biashara, biashara nayo inapata changamoto hiyo hiyo. Kwa kifupi, biashara inaweza kuwa inatengeneza faida kubwa, ina wafanyakazi na wateja wengi, lakini bila uwepo wa mwanzilishi, haiwezi kwenda.
Biashara ambayo ipo kwenye hali hiyo haiwezi kuchukuliwa kwamba imefanikiwa. Inakuwa haina tofauti na mtoto ambaye bado anategemea ziwa la mama ndiyo aishi licha ya umri kwenda, hawezi kuchukuliwa yuko sawa.
Mafanikio ya biashara yamekuwa na mtego ambao wengi wamekuwa wanashindwa kuuona na kuukwepa. Wakati biashara inaanza, mtu anaona ni ndogo hivyo inapaswa kumtegemea kwa kila kitu. Wakati biashara inafanya vizuri, mtu anabweteka na kuona hana haja ya kufanya mambo yatakayompa uhuru kwenye biashara hiyo. Na wakati biashara inafanya vibaya, mtu anakuwa hana subira ya kuijenga kwa namna ambayo haitamtegemea.
Huo mtego umewafanya wengi wanaoingia kwenye biashara kujikuta kwenye gereza ambalo ni gumu kutoka. Wanaweza kuzalisha matokeo makubwa, lakini kwa kushindwa kuijenga biashara kuweza kujiendesha bila wao, wanajikuta wakikosa kabisa uhuru, ambacho ndiyo kiliwasukuma kuingia kwenye biashara.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza maeneo matatu unayopaswa kuhakikisha yanafanya kazi bila kukutegemea ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio. Na biashara yenye mafanikio ni ile inayoweza kujiendesha bila kukutegemea moja kwa moja.

1. Tatizo Kubwa La Biashara Linaanzia Kwenye Vipimo Vya Mafanikio Visivyo Sahihi.
Hivi karibuni nilikuwa nazungumza na mfanyabiashara ambaye anazalisha bidhaa zake mwenyewe. Japokuwa bado hawafi vizuri sana kwenye mauzo, nilimsifia kwa kuchagua njia hiyo ya kuzalisha bidhaa zake mwenyewe.
Alichonijibu yeye ni kwamba anaona kama amekosea njia. Kwa sababu wale wanaofanya biashara ya kununua na kuuza, wanapata mauzo na faida kubwa kuliko yeye.
Nilimwambia ni sahihi, wengine wanaweza kuonekana kupata pesa kwa haraka, lakini hilo halimaanishi biashara zao zimefanikiwa. Bado hakuridhika na jibu hilo, yeye aliona mafanikio ya kwanza kwenye biashara ni mauzo na faida kubwa.
Hapo ndipo nilipogundua kwamba tatizo kubwa linalopelekea biashara kutokupata mafanikio makubwa ni vipimo vya mafanikio visivyokuwa sahihi.
Ni kweli kwamba watu wanaingia kwenye biashara ili wafanye mauzo na kupata faida. Lakini kama hivyo ndiyo vitakuwa vipimo pekee vya mafanikio, kamwe watu hawatapata uhuru ambao ndiyo kilichowasukuma kuingia kwenye biashara.
Anayeanzisha biashara huwa anakuwa ndiye mtu anayeweza kuuza kwa urahisi na ukubwa kuliko wengine wote. Kwa sababu kuna msukumo fulani uliopo ndani yake, utakaomfanya apambane mpaka auze.
Kama mafanikio ya biashara yatapimwa kwa mauzo na faida pekee, mwanzilishi atafanya kazi sana ili hilo litokee. Na hata kama atakuwa na wafanyakazi anaowapa majukumu, bado uwepo wake utahitajika mara zote ndiyo mambo yaweze kwenda.
Mafanikio sahihi ya biashara yanaanzia kwenye kubadili kile ambacho kinapima mafanikio. Badala ya kupima mafanikio ya biashara kwa matokeo ya eneo moja moja, yanapaswa kupimwa kwa uwezo wa kujiendesha bila kumtegemea mmiliki au mwanzilishi.
Na hilo linapaswa kuanza kufanyiwa kazi tangu biashara inapoanza. Maana wengi huona mwanzoni hawapaswi kulipa hilo uzito, hivyo kusubiri mpaka biashara ipige hatua na hapo kujikuta wameshachelewa.
Wakati wa kuanza biashara, inakuwa inaonekana ni ndogo na mambo ya kujenga mifumo na watu hayawezi kufanikiwa. Yanaonekana kuwa ni mambo mengi na biashara kushindwa kuyamudu mwanzoni.
Lakini hilo siyo kweli, kwenye ngazi yoyote ile ya biashara, eneo la uhuru linaweza kufanyiwa kazi. Hata kama mtu yuko peke yake kwenye biashara, bado kuna mambo anaweza kuyafanya na baadaye yakampa uhuru mkubwa.
Kwa biashara zinazoanzia chini au zisizopenda mambo mengi, kuna maeneo matatu yanayopaswa kufanyiwa kazi ili biashara iweze kufanikiwa. Maeneo hayo ni Kutengeneza, Kutangaza na Kusimamia. Vipengele vinavyofuata tutayaangalia maeneo hayo kwa kina.
2. Kutengeneza; Kuwapa Watu Kitu Cha Kipekee.
Biashara inajengwa kwa kuwa na kitu chenye thamani ambacho inatoa kwa watu wanaokuwa wanakihitaji. Kitu hicho kinaweza kuwa ni bidhaa au huduma ambayo inatatua changamoto au kutimiza mahitaji ambayo watu wanayo.
Bila kuwepo kwa hii thamani, hakuna biashara. Na kama thamani hiyo ipo, lakini haina namna ya kujitofautisha na wengine wanaoitoa, pia hakuna biashara. Kuwepo kwa kitu cha kipekee kinachouzwa na watu kuwa na uhitaji nacho ni eneo muhimu sana kwenye biashara.
Biashara inapokuwa inaanza, mwanzilishi anakuwa na maono ya kitu cha kipekee ambacho kinahitajika na watu. Kwa maono hayo, anakuwa na namna ya kipekee ya kuwapa watu kitu hicho, kiasi cha wao kupenda kukipata kwake, hata kama kuna wengine wanaokitoa.
Kwa waanzilishi kujifunza kwamba wao ndiyo wanaoweza kutoa vizuri kile wateja wanakitaka, wanajikuta wakiwa wanategemewa mara zote kwenye kutoa kitu hicho. Biashara inaweza kufanya mauzo makubwa, kwa sababu ya upekee wa mwanzilishi kwenye kutoa thamani aliyochagua. Lakini biashara haiwezi kufanikiwa kwa njia hiyo.
Biashara inafanikiwa pale inapoweza kutengeneza na kutoa kile ambacho kinauzwa, bila kumtegemea kabisa mwanzilishi. Ni pale biashara inapoweza kuandaa na kutoa thamani bila kumtegemea mwanzilishi ndiyo inakuwa imefanikiwa.
Chukua mfano wa mpishi, ambaye anasifiwa kwa kupika vizuri. Anaona fursa ya kufungua mgahawa wake mwenyewe, na kwa sababu yuko vizuri kwenye mapishi, yeye ndiye anakuwa mpishi mkuu. Anapika chakula kitamu sana na watu wanatoka mbali kuja kula kwake, kitu kinachofanya mauzo kuwa makubwa.
Lakini siku ambayo mtu huyo anaumwa na hawezi kwenda kwenye biashara, ndiyo siku ambayo anagundua hakuwa na biashara. Kwa sababu biashara inashindwa kuzalisha aina ya chakula ambacho yeye amekuwa anazalisha.
Pamoja na upekee ambao mtu anaweza kuwa nao kwenye kuleta matokeo ya aina fulani, bado anaweza kuweka mfumo wa matokeo hayo kupatikana bila kumtegemea yeye moja kwa moja. Hasa pale kinapokuwa ni kitu cha kujirudia rudia, ni lazima sana kiweze kufanyika bila kumtegemea mtu yeyote mmoja.
Wengi wamekuwa hawapo tayari kuwafundisha wengine kuzalisha kile wanachozalisha kwa sababu wanaona watatoa siri ya matokeo ya kipekee wanayopata. Lakini hilo siyo kweli, bado kuna njia bora za mtu kutunza siri hata baada ya kuwafundisha wengine kuzalisha kile unachouza.
Wajibu wako; Unapokuwa kwenye biashara, hakikisha umeandaa miongozo na kuwafundisha watu jinsi ya kutengeneza kile kinachouzwa. Hakikisha kinachouzwa kinaweza kupatikana bila kukutegemea wewe moja kwa moja. Hata kama ndiyo kitu unachopenda kufanya, fanya kwa mapenzi lakini siyo kwa kutegemewa.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK141; Maeneo Matatu Ya Kuhakikisha Yanafanya Kazi Ili Biashara Ifanikiwe