Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Wengi wa wanaopambana kujenga mafanikio makubwa na kushindwa, wamekuwa wanatumia kukosa pesa kama kikwazo. Wanaweza kuonyesha jinsi ambavyo wamepambana sana ili wapate matokeo, lakini kwa kukosa pesa, kuna vitu ambavyo vimeshindikana.
Ni kweli kwamba mafanikio makubwa yanahitaji pesa. Lakini siyo kweli kwamba kukosa pesa kunaweza kumzuia mtu asipate mafanikio makubwa. Kuwa na pesa kunaweza kuirahisisha safari ya mafanikio, lakini kukosa pesa hakuwezi kuizuia kabisa.
Watu wanapenda kutumia kikwazo cha pesa kwa sababu ni rahisi kukitumia na kinaficha kikwazo kingine ambacho kikiwekwa wazi, watu watajiona ni wazembe. Kwa sababu watu hawapendi kujiambia ukweli kwamba wanajikwamisha wao wenyewe, wamekuwa wanakimbilia kutumia kisingizio cha pesa.
Na hata kama ni kweli kwamba kukosa pesa kumekuzuia kufanikiwa, kwa hiyo? Ina maana unakubali maisha yako yote yawe ya kukosa unachotaka kwa sababu tu unaanzia mahali ambapo huna pesa? Je umeshatumia kila njia nyingine zilizopo na zikashindikana kabisa?
Kama kweli unachotaka ni mafanikio makubwa, na kama kweli umejitoa kuyapata mafanikio hayo, hakuna chochote kinachoweza kukuzuia kuyapata. Unaweza kuchelewa kuyapata mafanikio, lakini huwezi kuyakosa kabisa.
Kuna aina fulani ya ujasiri ambao mtu unahitaji kuwa nao ndiyo uweze kupata mafanikio makubwa bila kukwamishwa na kitu chochote.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza ujasiri huo, ili uifanye dunia ikupe kila unachotaka, hata kama unakosa vile ambavyo umekuwa unadhani vinahitajika.

1. Furahia Kuanza Ukiwa Huna Pesa.
Kwenye safari ya kujenga mafanikio, unachofikiria ni kikwazo, kinapaswa kuwa ndiyo kichocheo. Wakati unaona kukosa fedha ni kitu kinachokuzuia kufanikiwa, unapaswa kufurahia hali hiyo, kwa sababu ndiyo itakufanya upate mafanikio unayoyataka.
Unaweza kuona nakuchanganya, iweje ufurahie hali ya kukosa pesa kwenye safari ya mafanikio? Sababu zipo wazi kabisa.
Unapokuwa huna pesa, unakuwa huna cha kulinda, hivyo unabaki na kitu kimoja tu, kushambulia ili upate matokeo. Ukiwa na pesa unajikuta ukihangaika kuzilinda na kuishia kupoteza pande zote mbili, hulindi na pia hushambulii vya kutosha.
Lakini pia ubunifu wako unakuwa mkubwa sana unapokuwa huna pesa. Ukiwa na pesa, kila tatizo utalitafutia suluhisho la kulipia pesa. Ukiwa huna pesa, matatizo mengi utayatatua kwa ubunifu, kitu kinachokupa matokeo mazuri zaidi.
Kuna sababu kubwa kwa nini teknolojia mpya huwa zinavumbuliwa na makampuni madogo au watu ambao hawana fedha nyingi. Kukosa fedha kunawasukuma kutumia ubunifu wao wote.
Uwepo wa pesa unadumaza ubunifu, kwa sababu matatizo mengi yanatatuliwa na pesa. Wakati mwingine pesa zinatengeneza matatizo ambayo yanakuwa usumbufu kwa mtu kuweka umakini kwenye kile anachotaka.
Kwa manufaa haya ya kutokuwa na pesa kwenye safari ya mafanikio, hata unapoanza kuzipata, ziondoe haraka. Mara zote kuwa kwenye hali ya kufulia kimkakati. Unapopata pesa wekeza yote ili ubaki bila pesa. Hilo litakusukuma utumie akili na ubunifu wako kupata pesa zaidi.
Ukitaka mapambano yako ya mafanikio yasipungue nguvu, hakikisha kila wakati unakuwa kwenye hali ya kukosa pesa. Hali hiyo itakusukuma utumie akili, ubunifu na nguvu zako kupata matokeo unayoyataka. Kwa kupitia hilo unaleta matokeo makubwa na yanayokupa mafanikio.
2. Vipi Kuanza Na Ulichonacho?
Najua umeshasikia sana hili mpaka umeona kama ni mazoea. Unapokuwa huna pesa unaambiwa anza na ulichonacho, anza na kidogo na utakua kadiri unavyokwenda. Lakini wewe unaona hata hicho kidogo huna, unaona huna kabisa cha kuanza nacho. Na ndiyo maana umekuwa unasubiri mpaka upate kile unachoona unaweza kuanza nacho.
Iko hivi rafiki, kitu pekee unachohitaji ili upate mafanikio makubwa ni kuwa hai. Mengine yote ni ya ziada tu. Ukiwa hai, unaweza kupambana kwa kila namna na ukafanikiwa. Ukipoteza uhai ndiyo unakuwa huna tena nafasi ya kufanikiwa.
Kama unaona huna kabisa pa kuanzia, unachokosa ni uthubutu wa kuanzia hapo hapo ulipo. Unatafuta urahisi au wepesi wa kupata matokeo bila kuweka kazi na muda unaohitajika. Hutaki kujiumiza wala kujitesa, unataka mambo yawe rahisi.
Lakini mambo hayawezi kuwa rahisi kwako, hasa pale unapokuwa unaanzia chini. Unapokuwa huna chochote, unapaswa kuwa tayari kufanya chochote kinachohitajika kufanya ili uweze kupata kile unachotaka.
Hakuna unachoshindwa kufanya kama uko hai. Ni wewe tu uache kujionea huruma na ufanye yale yanayopaswa kufanika ili upate unachotaka kupata.
Anzia popote ulipo, fanya chochote kinachohitajika kufanya na usijionee huruma sana. Mafanikio unayoyafikiria yanawezekana kwako, ndiyo maana umeweza kuyafikiria. Kinachopaswa kufanyika kipo ndani ya uwezo wako kukifanya, ni wewe uwe tayari kufanya.
Ukiangalia muda ambao watu wengi wamekuwa wanasubiri mpaka wapate mahali pa kuanzia, kama wangeanzia popote walipo, tayari wangekuwa wamepiga hatua. Mtu anayesubiri miaka 10 kupata mtaji mkubwa wa kuanzisha biashara, angeanza hata na kuuza tu vitu vya wengine, kwa miaka hiyo 10 angekuwa amepiga hatua kubwa zaidi.
Kitu chenye gharama kubwa kwako ni muda unaopita bila wewe kufanyia kazi mafanikio unayoyataka. Kila muda unaopita unakuwa umeupoteza na kamwe huwezi kuupata tena. Hata kama utakuja kupata ulichokuwa unasubiri, muda uliopoteza una thamani kubwa kuliko chochote unachokuja kupata.
Usikubali tena kuendelea kupoteza muda kwa kusubiri kitu chochote kile. Kila wakati fanya kile kilicho mbele yako ili kusogea karibu zaidi na mafanikio yako.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK140; Kinachokuzuia Kufanikiwa Siyo Kukosa Pesa, Bali Kukosa Huu Uthubutu