Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Mara nyingi nimekuwa nakuambia hakuna siri za mafanikio, siri zilizofichwa ambazo wachache ndiyo wanazijua na kuzitumia. Nimekuwa nakuambia hivyo kwa sababu nimekuwa naona jinsi ambavyo watu wanapoteza muda na nguvu zao kwa kuhangaika na vitu ambavyo vipo wazi kabisa.

Lakini sasa nashawishika kwamba huenda siri ipo, lakini siyo siri kama ambavyo watu wanaitafuta. Yaani siyo siri moja ambayo wachache wanaijua na kuitumia huku wengi wakiwa wamefichwa.

Badala yake, siri ya mafanikio ni kile ambacho kipo ndani ya mtu mwenyewe, ambacho amekuwa hakioni wazi. Na ndiyo maana hata watu wanapowaiga wengine waliofanikiwa, wamekuwa hawapati mafanikio kama ya hao wanaowaiga.

Kwenye kitabu cha The Alchemist, kinaelezea safari ya mtu aliyeyaacha maisha yake na kwenda safari ndefu na ya mateso ya kutafuta hazina ya maisha yake. Baada ya mahangaiko ya miaka mingi, anakuja kugundua hazina yake ilikuwa pale alipotoka.

Kitabu hicho kimebeba uhalisia mkubwa sana wa maisha. Tumekuwa tunayapoteza maisha yetu, kwa kuhangaika kutafuta vitu, ambavyo tayari vipo ndani yetu. Kama tu tungepata nafasi ya kujitambua sisi wenyewe, tungeweza kupunguza upotevu wa muda na nguvu kwenye mambo yasiyo na tija.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kuona kile ambacho tayari kipo ndani yako na kinaweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka bila kuhangaika na mengi ambayo unahangaika nayo sasa.

1. Tambua Kazi Ya Maisha Yako.

Namna tunavyoyapokea maisha na kuyaishi, ni tofauti kabisa na kusudi la sisi kuwa hapa duniani. Kwa sababu tunazaliwa bila ya maelekezo ya nini tunaweza au kupaswa kufanya, tumekua tunaiga kile ambacho tumekuta wengine wanafanya kwenye maisha.

Maisha yetu kwa mazoea yanaangukia kwenye vipindi vitatu, kipindi cha utoto ambacho wajibu mkubwa ni kujifunza, kipindi cha ujana na utu uzima ambapo wajibu ni kujenga maisha na kipindi cha uzee ambacho ni cha kustaafu na kufa.

Kwa bahati mbaya sana, katika vipindi vyote vitatu, watu wengi wamekuwa hawaishi maisha yao, badala yake wamekuwa wanajiandaa kuishi. Wakiwa watoto wanaona wanajiandaa na ujana na utu uzima ndiyo wawe na maisha. Wakifika ujana na utu uzima wanakuwa wanajiandaa na kujenga maisha na mali. Wakifika uzee na kustaafu wanakufa.

Katika kipindi chote cha maisha, watu wamekuwa wanahangaika na kukimbizana na vitu vingi. Na sehemu kubwa ya vitu ambavyo wanakimbizana navyo havina tija kabisa kwenye maisha yao. Yaani ni vitu wanafanya, lakini haviwanufaishi kwa namna yoyote.

Kwa watu kutokujitambua, wanaishia kupoteza muda na nguvu kwa mambo ambayo hayawahusu kabisa. Kuna wachache ambao kwa bahati wanajitambua na kutumia maisha yao vizuri. Lakini wengi wamekuwa hawajitambui kwa kipindi chote cha maisha yao.

Kila maisha hapa duniani yana kazi maalumu, kazi ambayo maisha hayo yameletwa ili kuitimiza. Wanaopata mafanikio makubwa ni wale wanaoitambua kazi ya maisha yao na kuifanya kwa namna inavyopaswa kufanyika.

Wanaohangaika na kila fursa na bado hawafanikiwi, ni kwa sababu wanayohangaika nayo yanakuwa siyo kazi ya maisha yao. Wanakazana kuiga kazi za maisha ya wengine, lakini kwao haifanyi kazi kabisa.

Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni mtu utajuaje kazi ya maisha yako? Na hilo ni swali la ziada, swali la msingi ni nini maana ya kazi ya maisha yako?

Kazi ya maisha yako ni; “Harakati ya maisha yako yote ya kujenga kitu kwa ajili ya wengine, ambacho kinaakisi wewe ni nani.”

Maana hiyo ya kazi ya maisha yako ndiyo inakuonyesha nini kazi ya maisha yako wewe. Kwa sababu tayari hivyo vinavyoelezwa vipo ndani yako, huhitaji kwenda mahali fulani au kufanya vitu fulani ndiyo uvipate.

Kwenye hatua zinazofuata, tutaangalia sehemu tatu za maana ya kazi ya maisha yako na jinsi ya kuijua kwenye maisha yako.

2. Harakati Ya Maisha Yako Yote.

Sehemu ya kwanza ya maana ya kazi ya maisha yako inaeleza kwamba ni harakati ambayo mtu utaifanya kwa kipindi chote cha maisha yako. Hapa ni mahali muhimu pa kuanzia, kwa sababu tumeiga kuishi maisha ya kujiandaa, kama vile tukimaliza maandalizi hayo tunapewa ushindi na kuwa tumemaliza.

Ni kama ambavyo tunapokuwa shuleni na kusoma kwa bidii, tukisubiri kwa hamu siku ya kuhitimu na kusema tumemaliza shule. Tunadhani maisha nayo ni kitu cha kupambania kwa kipindi fulani na kuwa tumemaliza.

Ukweli wa maisha ni kinyume na mtazamo huo wa kumaliza kitu kwa kipindi fulani. Kazi ya maisha ni harakati, msako na mapambano ya kipindi chote cha maisha yako. Ni kuendelea kuifanya kazi kwa ubora zaidi kadiri unavyokwenda.

Huwezi kuelewa hili mpaka pale unapokuwa umefika kwenye kilele ulichokuwa unapambania. Kama ulivyokuwa shule na kusubiri kwa hamu siku ya kuhitimu, lakini baada ya kuhitimu unakumbuka siku za shule.

Kuna watu wanapambana sana kwa kipindi kifupi, ili wapate matokeo makubwa na waache kabisa kupambana. Ni mpaka pale wanapopata wanachotaka na kuacha kupambana ndiyo wanagundua maisha yao yanakosa maana kabisa.

Ukiona unapambana na kitu ili ukimaliza uachane nacho kabisa, hiyo siyo kazi ya maisha yako. Kazi ya maisha yako inatokana na kitu ambacho hutaacha kukifanya kwa maisha yako yote.

Wakati wengine wanafanya kitu ili wapate pesa na wakishapata wanaacha, anayefanya kazi ya maisha yake hatakubali kuacha hata kama angelipwa asifanye. Yaani anakuwa tayari hata yeye ndiyo alipe, ili tu aendelee kufanya.

Ni kitu gani kwenye maisha yako ambacho huhitaji msukumo wowote wa nje ndiyo ukifanye? Kitu gani ambacho hata ukiwa na fedha na kila unachotaka, bado utaweka juhudi kubwa kwenye kukifanya?

Ni muhimu sana utambue hicho mapema, na hata kama huwezi kukifanya kuwa kitu kikuu kwako kwa sasa, uanze kukijenga kwa hatua ndogo ndogo wakati unaendelea kujenga maisha mengine.

Maisha yako yanakuwa na maana pale unapokuwa na kitu unachofanya bila ya kutegemea msukumo wowote wa nje. Pale unapofanya kitu kwa sababu ndiyo maisha yako, kunakupa hali kubwa ya kuridhika, ambayo huwezi kuipata kwa njia nyingine yoyote.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK139; Unayapoteza Maisha Yako Kwa Kuhangaika Kutafuta Kitu Ambacho Tayari Unacho