Ukiwauliza watu maisha ni nini utapata majibu mengi sana. Kila mtu ana tafsiri yake juu ya maisha. Kuna watakaokwambia maisha ni safari, wengine watasema maisha ni mapigano, wengine maisha ni mchezo na mengine mengi. Haijalishi wewe binafsi unayaelezea vipi maisha, ila kuna vitu muhimu vinatokea kwenye kila maisha ya binadamu.

  Tafsiri yetu tuliyonayo juu ya maisha inatokana na mtazamo tulioujenga kulingana na mazingira tuliyoishi na tunayoendelea kuishi. Kutokana na mitizamo hii imefanya baadhi ya watu kuwa na maisha ya furaha sana na yenye mafanikio na wengine kuwa na maisha magumu sana na yenye mikosi.

not fair

  Watu wengi wamekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali kwenye maisha. Kutokana na mtazamo walionao juu ya maisha inawapelekea kuchukulia vikwazo hivyo kwa utofauti sana na kujikuta wanaharibu maisha yao wenyewe.

  Kutokana na mtizamo na kutokujua vitu muhimu kuhusu maisha imepelekea watu wengi kuyaharibu maisha yao na wengine hata kuyakatisha. Inawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao wameshayaharibu maisha yao kutokana na mambo mbalimbali unayokutana nayo kwenye maisha. Yawezekana umeshakata tamaa na maisha na kuamua kuyaacha yaende tu. Kitu kizuri nachotaka kukuambia leo ni kwamba kama bado uko hai na unaweza kusoma hapa bado unayonafasi kubwa ya kuyafanya maisha yako vile unavyotaka.

  Kuna vitu vingi sana ambavyo huwa vinaadhiri maisha ya kila binadamu bila ya kujali umri, kabila, jinsia, dini au rangi. Hapa nitazungumzia vitu viwili tu ambavyo ni lazima uvijue kama kweli unataka kuyasimamia maisha yako(kumbuka wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako). Kwa kuvijua vitu hivi viwili unaweza kubadili mtizamo wako juu ya maisha na kuanza kuishi maisha unayoyataka.

1. Ni lazima utakutana na vikwazo kwenye maisha. Haijalishi familia unayotokea ama rangi ama kabila, vikwazo ni sehemu ya maisha. Vinaweza kuwa vikwazo vikubwa ama vikwazo vidogo ila kwa namna yoyote ile ni lazima utakutana na vikwazo ama changamoto kwenye safari yako ya maisha.

  Unaweza kumuamini mtu akakuangusha, unaweza ukafanya biashara ukapata hasara, unaweza kusoma shule ukafeli mitihani, unaweza kuwa na kazi ukafukuzwa, na mengine mengi. Hata ujiandae kwa kiasi gani bado kuna vikwazo vitatokea ambavyo hukuvidhania.

  Kwa wewe kujua kwamba vikwazo ni sehemu ya maisha, na kwamba hata ujiandae vizuri bado kuna vikwazo utakutana navyo inakusaidia wewe kuweza kufanya maamuzi sahihi unapokutana na vikwazo hivyo. Inakufanya wewe kuyaendesha maisha badala ya kuendeshwa na maisha. (Kumbuka changamoto za maisha ndizo zinatufanya tufurahie maisha)

  Katika jambo lolote unalofanya iwe ni kazi ama biashara na hata kwenye maisha ya kawaida jiandae kukabiliana na vikwazo ambavyo lazima utakutana navyo, japo kwa sasa huvijui. Wakati mwingine ni vyema kuwa na mpango mbadala(plan B) ili pale mambo yanapokwenda hovyo usitetereke sana.

2. Maisha hayako sawa, dunia haina huruma. Kitu cha pili cha muhimu unachotakiwa kujua kuhusu maisha ni kwamba maisha hayako sawa na dunia haina huruma. Mara nyingi tunakutana na vikwazo mbalimbali kwenye maisha tunaishia kulaumu ni jinsi gani dunia haitutendei haki. Ni kweli kabisa kwamba dunia haiko sawa na wala haina huruma.

not fair2

  Kuna wakati unaweza kufanya kila unachotakiwa kufanya na kwa usahihi kabisa ila mwisho wa siku hupati majibu uliyotegemea.

  Unaweza kufanya kazi kwa juhudi na ubunifu mkubwa mwingine akachukua zawadi kupitia kazi yako hiyo na wewe usitambulike kwa lolote.

  Unaweza kujitahidi kuwa mtu mwema, kusaidia watu na kuwa mwaminifu lakini bado watu wasiuone mchango wako au hata wengine wakaudharau kabisa.

  Unaweza kuwa umesoma sana, una uwezo mkubwa na una juhudi kwenye kazi ila mtu uliyemzidi kwenye vyote hivyo ndio akawa msimamizi wako wa kazi(bosi) na mbaya zaidi akawa haudhamini mchango wako.

  Unaweza kuwa una vigezo vyote vya kuajiriwa lakini hupati kazi na wakati huohuo kuna mtu unamfahamu ambae hana hata nusu ya vigezo ulivyonavyo ila ana kazi.

  Ndivyo dunia ilivyo, badala ya kuumia sana na mambo kama hayo ni vyema ukayachukulia yalivyo na kisha ukaendelea na mipango yako ya maisha.

  Ukisema dunia haikutendei haki, wewe ndio huitendei haki dunia, kwa kuwa wewe uliikuta dunia. Wewe unatakiwa kuwa chanzo cha mabadiliko duniani na sio dunia ikubadili wewe.

  Kwa kujua mambo hayo mawili kuhusu maisha na kuyaelewa vizuri kutakusaidia sana kubadili mtazamo wako juu ya maisha. Itakusaidia uweze kufanya maamuzi sahihi pale unapokutana na vikwazo mbalimbali.

  Kinachopelekea watu kujiua hasa wanapokutana na matatizo ni kutojua jinsi gani maisha yanavyokwenda.

  Chukua hatua dhidi ya maisha yako, IBADILI DUNIA NA USIKUBALI DUNIA IKUBADILI WEWE. Ungana na watanzania wenzako waliochukua hatua dhidi ya maisha yao kwa kujiunga na kundi hili SAA KUMI NA MOJA ALFAJIRI TANZANIA(bonyeza hayo maandishi)

  Usambaze ujumbe huu uwafikie watanzania wengi zaidi kwa kushare kwenye mitandao ya kijamii.