MAKALA HII IMEANDIKWA NA IMANI NGWANGWALU WA TANGA TANZANIA.

Kama wewe ni mfatiliaji mzuri wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA katika makala “Vitu 12 unavyotakiwa kuvifanya katika maisha yako” moja ya kitu muhimu tulichojifunza ili kujenga mafanikio ya kudumu ni lazima kufanya mambo ambayo yatatusogeza kwenye malengo yetu mara kwa mara.

Hii ikiwa na maana kuwa si kila kitu tunatakiwa kufanya katika maisha ni lazima kuna mambo tunatakiwa tuyaache ili tufanikiwe zaidi. Katika makala hii utajifunza mambo ambayo unatakiwa uyaache katika maisha ili usonge mbele. Mambo haya yamekuwa yakikuzuia kwa muda mrefu kusonga mbele katika maisha yako na pengine kukukwamisha kabisa.

Ili uweze kufanikiwa na kufanya mambo makubwa maishani mwako ni lazima uachane na mambo hayo mara moja. Ukibadili mtazamo wako na ukaamua kwa dhati kuachana na mambo hayo nakupa uhakika utafanikiwa. Kwa nini nakwambia utafanikiwa!! Ni kwa sababu utakuwa umeachana na mambo ambayo kwako yamekuwa kama tabia iliyokufikisha hapo ulipo na kukukwamisha kwa muda mrefu.

Yafuatayo ni mambo 12 ambayo hutakiwi kuyafanya katika maisha yako:-

1.Acha kufikiria vitu usivyo vitaka katika maisha yako.

Mawazo uliyo nayo yana nguvu kubwa sana ya kuumba kuliko unavyofikiria. Kama mawazo uliyo nayo yanazingatia kwa muda mrefu vitu usivyo vitaka utavipata hata kama hutaki.Kumbuka unakipata tu kile unachokizingatia katika ubongo wako.Unataka kufanikiwa weka nguvu ya uzingativu kwenye mambo mazuri unayoyataka na kweli utayapata. Achana na tabia ya kuwaza vitu hasi waza chanya tu.

clip_image002

2.Acha tabia ya kulalamika sana.

Ukiwa na tabia hii uwe na uhakika hautafanikiwa. Unapolalamika ndani mwako unakuwa unajenga ukuta wa kukuzuia kusonga mbele maana kila unachokifanya utakuwa unahisi kama unaonewa kumbe hakuna wa kukuonea. Achana na tabia hii ya kulalamika uking’ang’ania sana tabia hii utakufa maskini.Kumbuka siku zote watu wa AMKA MTANZANIA tunachukua hatua juu ya maisha yetu na sio kulalamika.(Unaweza ukasoma pia kama Unaendelea kufanya kosa hili utakufa maskini)

3.Acha kutumia muda wako hovyo.

Maisha ni mafupi sana. Hakikisha unatumia muda wako vizuri na watu sahihi, usikubali kupoteza muda wako.Thamani kubwa ya maisha yako ipo kwenye muda ukipoteza muda ni sawa na kupoteza maisha. Angalia usije ukajuta kwa kufanya kosa hili la kupoteza muda.

4.Acha tabia ya kulaumu wengine.

Wewe ndiye mtu pekee unayepaswa kuwajibika juu ya maisha yako. Achana na tabia ya kulaumu wengine au serikali ndio iliyofikisha hapo ulipo sasa na kufanya mambo yako kuwa mabaya. Jilaumu mwenyewe kwa kutoweza kuchukua hatua juu ya maisha yako kwani hapa Duniani zipo fursa nyingi sana ambazo zinaweza kukufanya wewe ukafanikiwa zaidi na kuwa tajiri.

5.Acha kufanya vitu vile vile kila siku.

Kama kuna vitu unavifanya kwa njia zile zile siku zote na haujaona mabadiliko makubwa katika maisha yako nakushauri achana navyo au badili namna ya kufanya kwa njia tofauti ambayo italeta matunda zaidi.Jaribu kubadili mbinu na mfumo wa utendaji wako yawezekana ndio unaokukwamisha na kukufikisha hapo ulipo. Fanya vitu vipya vitakavyoleta mabadliko chanya maishani mwako.

6.Acha kujidanganya wewe mwenyewe.

Una uwezo mkubwa sana wa kumdanganya kila mtu lakini achana na tabia ya kujidanganya wewe mwenyewe. Acha kujidanganya kwamba ipo siku mambo yatakuwa mazuri wakati umekaa tu huchukui hatua yoyote, hapo utakuwa unajidanganya. Utafanikiwa tu endapo utaachana na tabia hii ya kujidanganya na kuchukua jukumu la kusonga mbele.

7.Acha kujifananisha na wengine.

Ishi maisha yako acha kujifananisha na mtu mwingine. Wewe ni mtu wa pekee sana hapa duniani kwani hakuna mwingine ambaye yupo kama wewe.Kuwa wewe kama wewe hii itakusaidia kufanya mambo yako kwa ufanisi zaidi.Unapoiga elewa kabisa hautaweza fanikiwa sana kwa vitu ambavyo umeiga.

kitabu kava tangazo

8.Acha kufikiria sana mambo ya nyuma.

Kama kuna sehemu ulikosea, acha kufikiria sana hayo makosa yameshapita songa mbele. Hauna uwezo wa kurudi nyuma na kwenda kufuta hayo makosa yako zaidi ya kujirekebisha sasa na kuchukua hatua ya kuendelea mbele.Utafanikiwa tu endapo utaanza kufikiria mambo mapya na kuachana na ya zamani.

9.Acha kujiandaa sana.

Wengi wetu huwa tunapoteza fursa nyingi kwa kudhani bado hatujajiandaa vya kutosha.Tambua hautaweza kukamilika kwa asilimia mia moja ndiyo ufanye mambo yako. Kama utaendelea kujiandaa sana basi elewa hutafanya kitu kikubwa katika maisha utaendelea kusubiri sana. Linapokuja suala la fursa changamkia mapema acha kujiandaa sana.

10.Acha kuogopa sana kukosea.

Fanya kitu katika maisha yako, jitoe mhanga na usiogope sana kukosea hiyo ni hatua muhimu ya maisha ya mafanikio.Kama utakuwa unaogopa sana kukosea kufanikiwa kwako kutakuwa kudogo sana.Watu wenye mafanikio makubwa sana Duniani ni wale ambao wamewahi kukosea sana.Watu hawa hawakuogopa kukosea kwao zaidi ya kujifunza na kuchukua hatua ya kuendelea mbele. Fata ndoto zako na achana na woga wako huo hautakufikisha popote zaidi ya kukufanya kuwa maskini.

11.Acha kujielezea sana kwa watu wengine.

Kama una tabia hii ya kujielezea sana kwa wengine ili wajue mambo yako achana nayo. Hakuna mwenye haja sana ya kujua mambo yako wewe ni nani na ufanya kitu gani, utajulikana tu kwa mchango wako mkubwa unaogusa jamii.

12.Acha kuwa na kinyongo na watu wengine.

Kama rafiki yako au jirani yako amefanikiwa katika jambo fulani hutakiwi kumkasirikia. Ni vizuri ukampongeza kuliko ukanuna na kuwa na kisirani nae au kinyongo kwani yale ni maisha yake. Acha tabia ya kuwa na kinyongo itakufanya utashindwa kujifunzia mambo mengi ya mafanikio na utashangaa kwanini husogei.

Hayo ndiyo mambo ambayo unatakiwa uachane nayo sasa ili uweze kubadilika na kuboresha maisha yako zaidi.Chukua hatua dhidi ya maisha yako endelea kufatilia mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa mambo mazuri zaidi.

Nakutakia safari njema ya mafanikio TUPO PAMOJA.

UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII IMANI NGWANGWALU KWA 0767048035.

KAMA NA WEWE UNA MAKALA NZURI ULIYOANDIKA NA UNAFIKIRI INAWEZA KUWAAMSHA WATANZANIA TAFADHALI NITUMIE KWENYE amakirita@gmail.com

MAKALA ISIWE IMEWEKWA KWENYE BLOG AU CHOMBO KINGINE CHA HABARI, IWE IMETUMIA KISHWAHILI RAHISI NA KINACHOELEWEKA NA IWE NA MANENO KATI YA 500 NA 1000 KARIBU SANA.